26.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Wanamitindo wafunguka miaka 15 ya Swahili Fashion Week

NA JEREMIA ERNEST

TASNIA ya mitindo ni moja ya sekta inayokuwa kwa kasi hapa nchini na Afrika kwa ujumla hadi kufikia hatua ya kutoa ajira nyingi kwa watu mbalimbali wa jinsia zote.

Hali hiyo imechangiwa na wabunifu wenyewe kwa kufanya kazi nzuri na kutanua wigo wa kazi zao na kuzitangaza Kimataifa.

Miongoni mwa wabunifu wa mitindo ambao majina yao wamekuwa makubwa na kutoa fursa kwa wengine ni Mustapha Hasanali, kupitia tamasha lake la Swahili Fashion Week.

Tamasha hilo ni jukwaa la mavazi ambalo linakutanisha wabunifu, wanamitindo na wadau tofauti wa mitindo kutoka nchi mbalimbali, wakionesha na kuuza bidhaa zao kwa siku tatu mfululizo.

Swahili Fashion Week ilianzishwa rasmi mwaka 2007, hivyo mwaka huu linatimiza miaka 15, muasisi wake akiwa ni Hassanali kupitia kampuni yake ya 361 Degreee.

Hassanali anaelezea nini kilimfanya akaanzisha tamasha ambapo anasema ni baada ya kushiriki matamasha ya mitindo yaliyokuwa yanafanyika nje ya nchi.

“Kila mwaka nilikuwa naenda kwenye matamasha ya mavazi ya nchi nyingine, hivyo siku moja muandaji mmoja akanambia kila siku unakuja kushiriki ungeanzisha kitu kama hiki nchini kwako ili kukuza tasnia ya mitindi, ndipo nikafikiria nikaona ni wazo zuri nikabuni jina nikaenda kusajili ,” anasema Hassanali.

Katika kuadhimisha miaka 15, Swahili Fashion Week, tayari emeanza usajili kwa wabunifu wanaohitaji kushiriki mwaka huu, mwisho wa usaili huo ni Mei 30,2022.

Mtanzania Digital, imepata nafasi ya kufanya mahojiano na wabunifu pamoja na wanamitindo waliowahi kishiriki Swahili Fashion Week, kila mmoja akielezea mtazamo wake juu ya jukwaa hilo kwa miaka iliyopita na mwaka huu.

Martin Kadinda ni mbunifu wa mavazi hapa nchin ambaye hadi sasa ameshiriki jumla matamasha tisa ya Swahili Fashion Week.

Anasema yeye kama mbunifu wa mavazi, jukwaa hilo limemnufaisha kwa kupanua wigo wa kibiashara, kujitangaza kimataifa na kumfungulia milango ya kufanya maonesho ya majukwaa ya kimataifa, akijifunza kutoka kwa wabunifu wachanga na wakimataifa.

Anasema katika kuadhimisha miaka 15, ametamani kufanyike maboresho hasa kwa wanamitindo wanaopita katika usaili.

“Wanamitindo wanaopita katika usaili ndiyo hao watumike kwa kuonyesha mavazi, wale wanaojitolea wapewe kazi zingine kujenga ujuzi, uzoefu na sio kupanda moja kwa moja jukwaani ili wanamitindo wazoefu wafanye shoo nzuri kwa sababu thamani ya jukwaa inakuwa zaidi kulingana na ubora wa wabunifu na wanamitindo,” anasema Kadinda.

Anawashauri wabunifu ambao bado hawaja shiriki jukwaa hilo kufanya hivyo ili kukutana na wabunifu wakubwa wa kimataifa waweze kujipima nafasi zao katika tasnia.

Naye Dk. Claudia Uwera wa Ucoco Brand, ni mbunifu wa mavazi nchinI Burundi, ni miongoni mwa wabunifu wa nje ya Tanzania ambao wamekua wakishiriki Swahili Fashion Week, kila wakati mpaka sasa ameonyesha kazi zake kwa muda wa misimu mitatu.

Anasema Swahili Fashion Week, ni jukwaa ambalo limewapatia fursa wabunifu na wanamitindo wa Afrika, kuonyesha ulimwengu kwamba Bara la Afrika kuna watu wana vipaji vikubwa katika tasnia ya mitindo.

Anaeleza kwa upande wake anaona uongozi wa Swahili Fashion Week, wanafanya kazi yao kwa ufasaha hivyo wabunifu kutoka sehemu mbalimbali wajitokeze kuonyesha kazi zao katika msimu huu wa 15.

Chua Fashion ni mbunifu wa mavazi hapa nchin ambaye anapatika katika Jiji la Arusha ameshiriki tamasha hilo kwa miaka mitano tangu kuanzishwa.

Anasema Swahili Fashion Week, imefungua milango kwa upande wake na kumfanya ajulikane yeye kama mbunifu wa mavazi na kazi zake, kupata wanunuzi wa moja kwa moja kutoka nchi za nje ikiwemo Marekani na Ujerumani ambao mpaka sasa anafanya nao kazi kwa ukaribu.

Anasema kuelekea kutimiza miaka 15 ya tamasha hilo, anaona vizuri uongozi ukaweka utaratibu wa kutoa pesa kwa washindi wa tuzo na kuboresha ada iwe kiwango cha kimataifa kwa sababu tamasha limekuwa kubwa.

“Kwa upande wa tozo ya kushiriki ziboreshwe ziwe za kiwango cha kimataifa, washindi wa tuzo walipwe pia wapatiwe fursa ya kutoa semina kwenye vyuo vya ufundi mfano Veta ili kuwa jengea vijana uwezo na changamoto wanapo ingia katika tasnia ya ubunifu,” anasema Chua Fashion.

Aliongeza kuwa Swahili Fashion Week ni jukwaa sahihi kwa mbunifu anayetaka kujikita katika tasnia hasa kwa wale wanao jitambua na kufahamu wanataka nini.

T-ngazy ni mbunifu wa mavazi hapa nchini ambaye anapatikana katika visiwa vya Zanzibar japo kuwa amekuwa akiishi nje ya nchi ameshiriki mara tatu tamasha la Swahili Fashion Week.

Anasema wakati alipoamua kufanya Swahili Fashion Week, alikuwa tayari jina lake la T-Ngazy, linajulikana kwa sababu alishafanya matamasha ya nje ya Tanzania, lakini aliona akishiriki jukwaa la nyumbani itapendeza na moja ya faida aliyoipata nikusaidia kuuza kazi zake kirahisi.

Anasema Swahili Fashion Week, imekua kwa kiwango cha juu na uongozi unatakiwa kutengenezea njia madhubuti kwa wabunifu kuweza kuuza kazi zao kupitia mitandao ya kijamii.
Anafafanua kuwa mfano kupitia ‘website’ yao au hata kwa mnada kwa sababu wabunifu wanatumia fedha nyingi kujiandaa na kazi zao (collection), jambo la kusikitisha wakishamaliza maonyesho zile nguo ndio zinakaa.
“Itapendeza wachukuwe jukumu la kuwatafutia masoko ya zile kazi, ili wabunifu wapate kurejesha fedha zao,” anasema.

Ally Chama ‘Chamack

Ally Chama ‘Chamack’, ni mwanamitindo aliyepata mafanikio makubwa kupitia tamasha hilo, alianza kupanda jukwaa hili mwaka 2015, alipohitimu kidato cha nne kwa wakati huo hadi mwaka jana 2021 takribani miaka 6 mfululizo ameweza kupanda katika jukwaa hilo.

Chamack anasema tamasha la Swahili Fashion Week, ni jukwaa zuri ambalo linainua vijana wengi katika tasnia ya mitindo na wanamitindo mbalimbali wanapata nafasi za kuoyesha vipaji vyao.

“Maisha yangu ya sasa kwa asilimia kubwa yanatokana na tamasha la Swahili Fashion Week, nina miliki biashara, nimefanya matangazo ya bidhaa mbalimbali za makampuni na hata kutumiwa na wabunifu wa mavazi kuonyesha mavazi, pia nimekua kioo kwa wanamitindo chipukizi,”anaeleza Chamack

Aidha anasema anatamani Swahili Fashion Week, iwe inafanyika mikoa mingine nje ya Dar es Salaam, hata kupeleka mbuga za wanyama, Bagamoyo na Zanzibar ili liwe tofauti na yaliyopita.

Kuhusu usaili anasema unafanyika kwa haki kwa wenye vigezo, hivyo kwa mwanamitindo chipukizi akikosa nafasi ajue kuna baadhi ya vigezo hajakidhi japo wanamitindo wa mikoani wanasahaulika.

” Ifike wakati usahili usifanyikie Dar es Salaam, pekee bali hata mikoani kuna wanamitindo wazuri na wenye vigezo vya kupanda katika jukwaa la Swahili Fashion Week,” anasema Chamack.

Kwa upande wake Anitha Mlay, anasema alianza kushiriki tamasha hilo kuanzia mwaka 2018 na kubahatika kupata tuzo ya mwamamitindo bora wa kike 2021.

Anasema kama mwanamitindo, Swahili Fashion Week imempatia kujiamini na ujasiri wa kushiriki Miss Landscape Tanzania 2019 na alipofika shindano la dunia akawa mshindi wa pili wa Miss Landscape International.

Pia kwa kuonekana kwenye jukwaa hilo ameweza kupata kazi nyingine za mitindo na kuona kuwa tamasha hilo linazidi kukuwa likikuwa na wandaaji waendelee hivyo hivyo na mapungufu ni machache kwa mfano mwaka jana wanamitindo hawakupata picha nzuri, hivyo mwaka huu watilie mkazo suala la taa za jukwaa.

Anasema amepata fursa ya kufahamiana na kuvaa nguo za wabunifu wengi wakongwe kwenye tasnia na wote anapenda kufanya shoo zao, ila alikosa nguo za Martin Kadinda.

“Martin kwanza nguo zake nyingi ni za kiume anatengeneza nguo chache za kike mpaka mwanamitindo wa kike kufanya shoo yake ujue amekuchagua mwenyewe (Hand-picked) kwa dhumuni la kupendezesha na ukichaguliwa na Martini Kadinda kufanya shoo yake uko vizuri,” anasema Anitha Mlay.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles