23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

… wanalazimishwa kula rushwa?

toa-rushwa

NA RACHEL MRISHO

MIONGONI mwa sababu zinazochangia watu kujihusisha na vitendo vya rushwa ni kulipwa ujira mdogo ama kutolipwa.

Kama ambavyo rushwa inaelezwa kuwa ni adui wa haki, nami nitasimamia msimamo huo huo kuwa si sahihi kutumia kigezo cha aina yoyote kutenda kosa la ama kutoa au kupokea rushwa.

Nashawishika kuandika makala haya kutokana na malalamiko yaliyotolewa hivi karibuni na askari wetu wapya walioajiriwa Juni, 2016 ambao kwa kipindi cha miezi minne hawajalipwa mishahara yao.

Taarifa ya malalamiko hayo ilithibitishwa na  Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Christina Mwangosi.

Pamoja na majibu yake ya kushughulikia  mishahara ya askari hao ikiwamo kuingiza majina yao kwenye mfumo wa malipo ili hatua za ulipwaji zianze.

Binafsi majibu hayo nayatilia shaka kwa sababu askari hao walipotoka mafunzoni walipewa  likizo ya mwezi mmoja kwa ajili ya kusubiri kuingizwa katika mfumo wa malipo, nini kimekwamisha hadi sasa kutolipwa stahiki yao?

Askari ni miongoni mwa watumishi muhimu wanaotegemewa na Serikali pamoja na raia katika kulinda amani ya taifa, raia na mali zao.

Mbali ya dhima hiyo askari ni watu wenye mahitaji zikiwamo huduma zote muhimu za kijamii kama makundi mengine yalivyo.

Kutokana na malalamiko haya kuna haja ya kujiuliza hivi katika mazingira  ya kawaida mtumishi ambaye hajalipwa mshahara hata wa miezi miwili anaishije?

Je, askari ambao wamepitisha miezi minne bila kulipwa mishahara yao wanajikwamuaje kiuchumi, wanahudumiaje familia zao na wanalipaje kodi za nyumba maana askari wengi wanaishi uraiani.

Kwa hao waliomaliza mafunzo na kubahatika kupata ajira hapana shaka kuwa miongoni mwao huenda bado wapo mikononi mwa wazazi au walezi ambao wanasubiri kula matunda ya vijana wao ama kuhama na kuanza kujitegemea.

Yapo maswali mengi ya kujiuliza kuhusu changamoto wanazopitia askari hao, lakini katika kuliangalia suala zima ni muhimu kwa Serikali kuangazia kwa jicho pevu malalamiko ya askari hao.

Kama nilivyoanza makala haya nimegusia suala la rushwa. Askari hao ni binadamu wanapita katika kipindi kigumu cha kukosa fedha za kujikimu, hivi itakuwaje pale rushwa ya fedha ama kitu chochote kitakapopita machoni mwao? Nauliza tu!

Itakumbukwa kuwa zipo tuhuma dhidi ya askari wetu wakiwamo wa kikosi cha usalama barabara kuhusishwa na vitendo vya rushwa, miongoni mwa askari waliopata kutuhumiwa walikuwa waajiriwa kwa maana kwamba walikuwa wanapokea mishahara yao kama kawaida.

Hoja yangu ni kuwa hao walikuwa wanapokea mishahara lakini bado walishawishika kupokea rushwa, Je, inakuwaje kwa hawa walioajiriwa lakini hapokei mishahara? Nauliza tu!

Kwa muktadha huo naona lipo tatizo kubwa linalobeba dhana pana ya malalamiko ya askari hao.

Hadi wanalalamika inamaana maji yamewafika shingoni, kama hatua za makusudi hazitachukuliwa kitakachotokea ni nini? Nauliza tu!.

Sawa wamepewa matumaini kuwa wasubiri taratibu zote zitakapokamilika watalipwa mishahara yao, kwa maana nyingine waendelee kusubiri siku, wiki na miezi mingine isiyofahamika huku wakiendelea kuishi katika mazingira magumu kama wanavyodai. Matumaini hayo yana sura tata.

Tukiiangazia kauli ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani  ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira, nayo inazidisha kuondoa matumaini ya kutatuliwa haraka jambo hilo.

Meja Jenerali Rwegasira, alisema baada ya askari hao kumaliza mafunzo majina yao yalipelekwa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa ajili ya kuingizwa kwenye mfumo wa malipo.

Nanukuu; “Walivyotoka mafunzoni tuliwapokea na kupeleka majina yao Utumishi kama bado hawajaanza kulipwa nakuomba waulizeni Utumishi ndiyo wenye majibu sahihi”.

Naishauri Serikali suala hili la mishahara ya askari lichukuliwe kwa uzito mkubwa, haipendezi walinzi wetu wa amani na mali za raia waishi maisha ya kupiga ‘vibomu’ mitaani.

Wasisukumwe kutamani rushwa, itapendeza zaidi kama askari wetu hasa wanaotoka mafunzoni watazingatia maadili na kupambana na rushwa kikamilifu. Pia kuwapo na taarifa za namna suala hilo linavyoshughulikiwa.

Changamoto wanazozipitia zisiwashawishi kuingia kwenye mdudu hatari rushwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles