31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

WANAKIJIJI WAUA MAJAMBAZI WATATU

black_bank_robber_mask__81906.1455327711.451.416

Na ABDALLAH AMIRI – IGUNGA

BAADHI ya wanakijiji wa Ncheli, Kata ya Sungwizi, wilayani Igunga, mkoani Tabora, wamewaua majambazi watatu kati ya watano akiwemo baba na mwanawe ambao walivamia nyumbani kwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Ncheli, Joseph Samwel (44) na kumvunja mkono.

Katika uvamizi huo uliotokea juzi usiku, majambazi hao walimjeruhi kwa mapanga na nondo Mwalimu Samwel na kumvunja mkono wa kushoto kisha kupora pikipiki, fedha taslimu na vifaa vya ndani.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Kamishna Msaidizi Hamisi Selemani Issa, alithibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kuwataja waliouawa kuwa ni Nkuba Mwadi (55), Bundala Nkuba (35), wote wakazi wa kijiji hicho huku jambazi mwingine anayekadiriwa kuwa na miaka 25 akishindwa kutambulika jina wala makazi yake.

Kamanda Issa alisema pikipiki iliyoibwa imehifadhiwa katika Kituo cha Polisi Igunga na kwamba hakuna mtu anayeshikiliwa kuhusiana na tukio hilo.

Akisimulia zaidi kuhusu mkasa huo, Diwani wa Viti Maalumu wa Kata ya Sungwizi, Anjel Milei, alisema majambazi hao walivamia nyumbani kwa Samweli saa tano usiku kwa kuvunja mlango wakitumia jiwe kubwa maarufu kama Fatuma.

Diwani Milei alisema baada ya majambazi hao kuingia ndani walianza kumshambulia Mwalimu huyo kwa silaha hizo zilizosababisha kuvunjika kwa mkono wake na baadaye alipoteza fahamu.

“Baada ya majambazi hao kuona Mwalimu ameanguka chini, walimwamuru mke wake awapatie funguo za pikipiki na kadi yake pamoja na fedha kiasi cha Sh 150,000 jambo ambalo alilitekeleza,” alisema Milei.

Milei alisema baada ya kupata vitu hivyo, majambazi hao bado walikusanya vitu vingine ikiwemo televisheni ambavyo thamani yake inakadiriwa kufikia Sh 3,680,000.

Alisema baada ya tukio hilo wanakijiji hao walijikusanya na kuwafuatilia majambazi hao ambao mmoja alikamatwa katika kijiji cha Kaumbu akiwa na pikipiki ya mwalimu huyo pamoja na baadhi ya vitu ikiwemo televisheni.

Alisema jambazi huyo alipohojiwa alianza kuwashambulia wanakijiji hao kwa nondo hali iliyozua hasira zilizosababisha auawe papo hapo baada ya kuwataja wenzake alioshirikiana nao.

Alisema baada ya hapo, wanakijiji hao waliwasaka majambazi wengine wawili na kuwaua ambao ni baba na mwanawe.

Akizungumza kwa shida wodini alikolazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Nkinga, Mwalimu Samwel aliiomba Serikali iwatengenezee mazingira bora ya kuishi walimu ili kulinda usalama wao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles