Na Mwandishio Wetu, Mtanzania Digital
Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limethibitisha kuuawa kwa wanajeshi wake wawili nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kufuatia mashambulizi ya waasi wa M23 katika maeneo ya Sake na Goma.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Februari 2, 2025 na Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa JWTZ, Kanali Gaudentius Gervas Ilonda, lwanajeshi wengine wanne walijeruhiwa katika mashambulizi hayo yaliyotokea kati ya Januari 24 na 28, 2025, na kwa sasa wanapatiwa matibabu mjini Goma.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa taratibu za kusafirisha miili ya marehemu pamoja na majeruhi zinaendelea kupitia Sekretarieti ya SADC. Pia, ilisisitiza kuwa vikosi vya Tanzania vilivyopo nchini DRC vipo salama, imara, na vinaendelea kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa maelekezo ya uongozi wa SADC.
JWTZ imekuwa ikishiriki katika operesheni za ulinzi wa amani chini ya Umoja wa Mataifa na jumuiya za kikanda, ikihudumu katika nchi kama Lebanon, Sudan, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Liberia, Msumbiji, na DRC.