25.5 C
Dar es Salaam
Thursday, February 13, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Wanaharakati watoa ushauri kuhusu mpango wa kuwafikishia umeme waafrika milioni 300

Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital

WANAHARAKATI wa Mabadiliko ya Tabianchi na Mazingira nchini wamewashauri viongozi wakuu wa Afrika kuzingatia teknolojia ya nishati jadidifu na endelevu katika utekelezaji wa mpango wa kuwafikishia umeme waafrika milioni 300 ikifapo mwaka 2030.

Kauli ya wanaharakati hao imekuja siku chache baada ya kumalizikia Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Afrika kuhusu nishati(misheni 300) ulifanyika Januari 27-28, 2025 jijini Dar es Salaam.

Wakizungumza na waandishi wa habari leo Januari 20,2025 Dar es Salaam, wanaharakati hao wametoa wito kwa Serikali za nchi za Afrika kulingana na fedha zilizotengwa kuhakikisha wanatoa kipaombele katika nishati jadidifu kama vile uzalishaji wa umeme wa maji,jua, upepo na joto ardhi.

Mratibu wa taasisi ya GreenFaith Tanzania, Baraka Lenga, amesema endapo Serikali itajikita katika kuwekeza katika nishati hizo jadidifu, itapunguza kwa kiasi kikubwa uchafuzi wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi.

“Umeme ni nyenzo kubwa sana ya maisha ya binadamu, kwa hiyo basi tulikuwa na mapendekezo yetu ya kuiambia Serikali kwamba wawekeze katika kwenye nishati safi ambayo ni nishati ya jua, nishati ya upepo, nishati joto ardhi na nishati ya maji,” ameeleza Lenga.

Naye Ofisa Mwandamizi wa Mabadiliko ya Tabianchi na Nishati Jadidifu wa taasisi hiyo, Baraka Machumu amefafanua kuwa kutokana na takwimu zilizotolewa katika mkutano huo, matumizi ya nishati jadidifu yataleta uendelevu na kufikia watu wengi zaidi.

“Mipango ni mizuri lakini tunapokuwa na mipango mizuri tuone mahitaji ya watu ni kitu gani. Ili kuhakikisha tunaepuka athari za mazingira na mabadiliko ya tabianchi na kupunguza utegemezi na kuleta haki sawa kwa jamii wananchi tunahitaji nishati mbadala,” anasema.

Mkurugenzi wa Green Conservers, Ziada Kassim amesema mwanamke ni mtu anayetakiwa kuzingatiwa zaidi katika suala la nishati kwa sababu ndiyo waathirika wakubwa nishati chafu.

Kwa upande wake Steven Selestin ambaye ni mkulima kutoka Tekelelo, Morogoro amesema umeme unamhusu kila mtu kuanzia anayeishi mjini hadi kijiji, kama wakulima wana uhitaji mkubwa wa nishati hiyo, hivyo anaiomba Serikali kuhakikisha wanatumia njia mbadala kuwafikishia.

Katika mkutano huo wa Wakuu wa Nchi za Afrika, umefanikiwa kupata ahadi za ufadhili wa Dola za Marekani Bilioni 40 kutoka Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa ajili ya kuwezesha usambazaji wa umeme barani Afrika. Aidha, jumla ya nchi za Afrika 12 zimeingia kwenye Mipango Mahsusi wa Kitaifa kuhusu Nishati.

Aidha Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ambaye alikuwa mwenyeji wa mkutano, wakati wa mkutano huo alisema Mpango Mahsusi wa Kitaifa kuhusu Nishati(National Enerrgy Compact) uliozinduliwa unalenga kuiwezesha Tanzania kuunganisha umeme kwa kaya milioni 8.3 zaidi ifikapo mwaka 2030.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
594,000SubscribersSubscribe

Latest Articles