Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Wanaharakati wa masuala ya kijinsia wamependekeza kuwe na ushiriki mpana katika mikakati ya maendeleo ya nchi ili makundi yote yaweze kufikiwa.
Mapendekezo hayo yametolewa Novemba 10,2023 wakati wa kuhitimisha Tamasha la 15 la Jinsia na maadhimisho ya miaka 30 ya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) yaliyofanyika katika viwanja vya mtandao huo Mabibo.
Akizungumza na waandishi wa habari Mkurugenzi wa TGNP, Lilian Liundi, amesema amesema ni muhimu kuwekeza vya kutosha katika uchambuzi wa matatizo na changamoto ili yakitokea kila mtu awe na uwezo wa kulielewa na kulitatua.
“Kama rasilimali zetu zingekuwa zinatengwa vizuri kunakuwa na uchambuzi wa kina wa makundi ya jamii na kujua kundi gani lina changamoto na rasilimali zielekezejwe hasa bajeti tungetatua matatizo mengi.
“Lakini kama hatuna uchambuzi wa kina wa kuelewa matatizo yako wapi tutakuwa tunatenga bajeti kwa jumla na matokeo yake matatizo yataendelea kuwepo,” amesema Liundi.
Ametolea mfano wa vilabu vya jinsia ambavyo vinawajengea uwezo wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kuwa na jicho la uchambuzi wa kina na kuweza kutengeneza suluhu wao wenyewe, kuelewa suala la ukatili wa kijinsia na namna ya kuuzuia.
“Tunachotaka ni kukomesha ukatili wa kijinsia na sio kusubiri utokee…madhara ya ubakaji ni ya muda mrefu sana,” amesema.
Ofisa Maendeleo wa Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa, Ellizabeth Shoo, amesema jitihada zinazofanywa na serikali na wadau mbalimbali wakiwemo TGNP zimesaidia kuongeza uelewa kwa jamii ndiyo maana matukio mengi ya ukatili wa kijinsia yamekuwa yakiripotiwa.
“Inawezekana kipindi cha nyuma matukio ya ukatili yalikuwa yakifanyika lakini kwa sababu wananchi hawakuwa na elimu kuhusu madhara hawakuyaripoti mengine yakawa yanaishia chini. Hatua kubwa imepigwa mpaka sasa tunaweza kusikia matukio yanapelekwa polisi, kwenye vyombo vya habari,” amesema Shoo.
Tamasha hilo lililokutanisha zaidi ya washiriki 2000 limeongozwa na mada kuu isemayo; ‘Miaka 30 ya TGNP na Tapo la Ukombozi wa Wanawake.