WANAHABARI WATAKIWA KUTOOGOPA VITISHO

0
1054

 

Na ANDREW MSECHU – DAR ES SALAAM


UMOJA wa Haki ya Kupata Taarifa (CoRI), umevitaka vyombo vya habari kuacha kufumbia macho ukandamizwaji unaofanywa na vyombo vya dola dhidi ya vyombo hivyo na wanahabari na kuwataka wadau wote kushiriki kwa ukamilifu katika uhuru wa kupata habari.

Wakizungumza na waandishi wa habari jijini jana, viongozi wa umoja huo unaoundwa na wanachama kutoka taasisi 11 za habari na  za haki za binadamu, wamevitaka vyombo vya habari kujitokeza na kutafuta msaada wa sheria  vinapokandamizwa kwa kuwa ndiyo njia pekee ya kuweza kuvisaidia.

Mwenyekiti wa umoja huo ambaye pia ni Katibu wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga, alisema matukio ya hivi karibuni ya kupigwa na polisi na kufunguliwa kesi kwa wanahabari Silas Mbise (Wapo Redio) na Sitta Tuma (Tanzania Daima) wakati wakiwa katika majukumu yao si jambo la kuvumiliwa katika ustawi wa haki ya kupata habari hivyo mkondo wa sheria unatakiwa uchukue nafasi yake.

“Ifahamike kwamba kila mtu ana haki ya kulindwa kwa mujibu wa sheria za nchi na vyombo vya utekelezaji vina jukumu na kulinda wanannchi na mali zao, ikijumuisha waandishi wahabari na watetezi wa haki za binadamu.

“Tunatambua kwamba Jeshi la Polisi nchini linaongozwa kwa sheria inayoliunda na kuliwekea majukumu kama ilivyoainishwa katika sehemu ya II kifungu cha 5(1),” alisema.

Alitaja matukio mengine ya unyanyasaji wa wanahabari kuwa ni kukamatwa kwa waandishi wa Raia Mwema, George Ramadhan na Christopher Gamaina mkoani Mwanza miezi miwili iliyopita kisha kufikishwa mahakamani, pia kwa mwandishi Emmanuel Kiniki anayekabiliwa na kesi mahakamani mkoani Iringa.

Mjumbe wa umoja huo ambaye ni Mkurugenzi wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu, Onesmo ole Ngurumwa alisema wataendelea kutumia njia za kudai haki kwa kutoa matamko, kwenda mahakamani na kufanya mazungumzo   itakapobidi.

Alisema pamoja na kuwapo   uonevu kutokana na   sheria mbovu, wataendelea kupigania sheria zinazoheshimu misingi ya sheria ya hali za binadamu na utawala bora, kwa kuhakikisha wanapigania kufutwa au kubadilishwa  sheria kandamizi.

“Vyombo vingi vya habari vimekuwa vikikaa kimya, vingine vikiendelea kusumbuliwa na hata kulipa faini zisizostahili kimya kimya.

“Tunavisihi vyombo vya habari na wanahabari wanaosumbuliwa wajitokeze  kupata msaada wa sheria,” alisema.

Mwakilishi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Wakili Godfrey Mpandilwa alisema hali si nzuri kwa wanahabari kwa kuwa hata baada ya   sheria mpya ya haki ya kupata habari iliyotegemewa kutoa fursa ya kusimamia haki ya upatikanaji wa habari bila vikwazo, bado haina nguvu za kutosha.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here