Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital
WAANDISHI wa habari wa mchezo wa gofu, wamempongeza Ofisa Habari wa Klabu ya Gofu ya Lugalo, Meja Seleman Semunyu kwa utendaji kazi wake katika kutoa taarifa za mchezo huo uliomfanya apandishwe cheo kutoka Kapteni na kuwa Meja.
Pongezi hizo zimetolewa jana usiku wakati wa hafla ya utoaji zawadi kwa washindi wa shindano la Johnnie Walker Waitara Trophy, iliyofanyika kwenye viwanja vya Gofu ya Lugalo, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kwa niaba ya waandishi wenzake, Rahel Pallangyo, amesema wameamua kumpongeza Meja Semunyu kwa sababu amekuwa akitimiza majukumu yake inavyotakiwa hali iliyomfanya apandishwe cheo kutokana na mchango wake katika klabu hiyo.
“Sisi kama Wanahabari tunampongeza Meja Semunyu kwa kupandishwa cheo, pia amekuwa akifanya kazi yake vizuri na sisi. Muda wowote tukiwa tunahitaji taarifa kuhusu Klabu ya Gofu Lugalo amekuwa akitupa ushirikiano mkubwa.
“Tumeona tutumie hafla hii na sisi kumpongeza na tumemuandalia zawadi ya keki,” ameeleza Rahel.
Kwa upande wake Meja Semunyu amewashukuru waandishi wa habari, huku akiahidi kuendelea kushirikiana nao katika kukuza mchezo wa gofu.