Wanafunzi wengine 11,378 wapewa mikopo elimu ya juu

0
831

Na MWANDISHI WETU- DAR ES SALAAM

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetoa orodha ya awamu ya pili ya waombaji wa mikopo kwa mwaka wa masomo 2019/2020 yenye jumla ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza 11,378 waliopewa mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 35.06.

Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru, ilieleza kuwa idadi hiyo ya awamu ya pili inafanya jumla ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliopata mikopo kufika 42,053 ambao wamepata mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 148.56.

Katika orodha ya awamu ya kwanza iliyotangazwa wiki iliyopita, wanafunzi wa mwaka wa kwanza 30,675 walipata mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 113.5.

Badru alisema katika mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali imetenga Sh bilioni 450 kwa jumla ya wanafunzi 128,285.

Alisema kati yao, wanafunzi zaidi ya 45,000 watakuwa wa mwaka wa kwanza na wengine 83,285 ni wanafunzi wenye mikopo wanaoendelea na masomo.

Badru alisema mwaka 2018/2019, Sh bilioni 427.5 zilitengwa na kuwanufaisha jumla ya wanafunzi 123,285 wakiwemo wanafunzi 41,285 wa mwaka wa kwanza.

 “Tumeboresha sana mifumo yetu, na sasa mwanafunzi anaweza kufungua akaunti yake aliyoombea mkopo maarufu kama SIPA – Student’s Individual Permanent Account – na kupata taarifa zake zikiwemo za kiwango cha mkopo alichopata,” alisema Badru.

Pamoja na SIPA, Badru alisema majina yote ya waombaji waliofanikiwa kupangiwa mikopo katika awamu hii ya pili yanapatikana katika mtandao wa HESLB wa uombaji mkopo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here