NA HARRIETH MANDARI
-GEITA
WANAFUNZI watatu wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Makurugusi iliyopo Chato mkoani Geita, wamepoteza maisha kwa kuzama katika Ziwa Victoria baada ya mtumbwi waliokuwa wamepanda kupinduka.
Walikuwa ziwani wakifanya mradi (project) ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuhitimu kidato cha nne.
Mradi wao ulikuwa unahusu ongezeko la watu na athari za mazingira katika eneo la mwalo wa Matofali Kibunda, Kata ya Makurugusi, ambao waliuanza Mei mosi na walikuwa wawasilishe ripoti yao kesho.
Akitoa ufafanuzi juu ya tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoani Geita, Mponjoli Mwabulambo, aliwataja waliopoteza maisha kuwa ni Atha Gabriel (19), Manyencha Faustin (18) na Masalu Hamis (22).
Kamanda Mwabulambo alisema wanafunzi watano wakiwa kwenye mafunzo yao ya mradi, walitamani kutembelea mandhari ya ziwa hilo, wakaamua kukodi mtumbwi ili kufanya utalii wa ndani.
Alisema walipanda mtumbwi ambao dereva alikuwa Daud Thomas na wakati wakiwa umbali wa mita 120 kutoka ufukweni, mmoja wao, aliyejulikana kama Samson Kano alivua nguo na kutumbukia majini kwa nia ya kuogelea.
Kamanda Mwabulambo alisema kuwa mwanafunzi huyo alipotaka kurudi katika mtumbwi, alivuta ukingo wa mtumbwi huo na ndipo ulipoegemea upande huo na kupinduka.
“Mtumbwi ulipopinduka wanafunzi wote walizama na kati yao watatu walizama kabisa, huku wengine wawili wakifanikiwa kuogelea na kutoka,” alisema.
Kamanda Mponjoli aliwataja waliookolewa kuwa ni Abiana Fitina (19) ambaye pia alikunywa maji mengi na hali yake sio nzuri na mwingine ni Yohana Yamonda (19).
Alisema harakati za kuwaokoa zilifanyika chini ya uongozi wa Mkuu wa Wilaya ya Chato, Mtemi Msafiri, Mkuu wa Polisi wa Wilaya na wananchi ambazo zilichukua siku nzima ya juzi hadi miili kupatikana saa 11 jioni.
Kamanda Mwabulambo aliwaonya wananchi watumiao vyombo vya majini kuhakikisha wanafuata taratibu na kanuni za usafiri huo.
“Pamoja na kwamba tukio hilo ni la ajali, lakini ni vyema pia waendesha mitumbwi wanapokuwa na abiria kama hao wanafunzi, wawe wanawapatia elimu au maelekezo ya kanuni na taratibu za kufuata wakati wakianza safari ili kuepukana na ajali kama hiyo kutokea tena,” alisema Kamanda Mwabulambo.