24.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Wanafunzi wasio na ulemavu wanavyowasaidia wenzao kujikinga na corona

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko iliyopo Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imetengeneza urafiki baina ya wanafunzi wasio na ulemavu na wale wenye ulemavu ili waweze kuwasaidia wenzao kuchukua tahadhari dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Corona (UVICO).

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko, Charity Chikoleka, akiwaelekeza wanafunzi kunawa mikono kwa maji tiririka kabla ya kuingia darasani ili kujikinga na Corona.

Mtanzania Digital imetembelea shuleni hapo na kushuhudia tahadhari zote zikiwa zimechukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwekwa ndoo za maji tiririka katika kila darasa na vitakasa mikono ili kuwakinga wanafunzi.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko, Charity Chikoleka mwenye taaluma ya kufundisha watoto wenye ulemavu, amesema wamechukua tahadhari kwa kuweka vitakasa mikono na maji tiririka pamoja na sabuni ambapo kabla ya kuingia darasani ni lazima wanafunzi wote wanawe mikono.

“Wanafunzi ambao hawana ulemavu wanawasaidia wanafunzi wenzao katika kunawa mikono na maji tiririka na tuna mlezi ambaye anasaidia kusimamia zoezi zima la kunawa mikono. Kila siku tunaendelea kuwaelimisha kwa sababu kwa watoto wenye ulemavu suala la kujifunza ni endelevu na haitokei kwamba wakapokea tu kwa mara moja elimu inatolewa kila siku,” amesema Mwalimu Chikoleka.

Naye Mwalimu Edith Dosha kutoka kitengo cha viziwi wasioona, amesema wanahakikisha walimu wanavaa barakoa kwa sababu wanafunzi wengi ni wale walio na umri chini ya miaka mitano na wengine wana matatizo ya kiafya hivyo hawaruhusiwi kuvaa barakoa.

“Watoto katika kitengo hiki huwa wanakaa hosteli zilizopo hapa shuleni na changamoto tuliyonayo ni uhaba wa walimu kwa sababu watoto ni wengi na wanataka usaidizi muda wote lakini tahadhari zote tunachukua,” amesema Mwalimu Dosha.

Mmoja wa wanafunzi wa darasa la sita Rahim Jumanne, amesema wameelimishwa na walimu juu ya kuwasaidia wenzao wenye ulemavu na amekuwa akifanya hivyo kila siku.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles