30.6 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Wanafunzi wanadai elimu bure, Polisi wanaibuka na mabomu

south-a-students-protests-1

Na Balinagwe Mwambungu

JESHI la Polisi chini ya utawala wa Makaburu wa Afrika Kusini, inasemekana liliua zaidi ya watu 451, wakiwamo wanafunzi ambao walikuwa wanapinga mpango wa serikali wa kutaka watoto wa Kiafrika wafundishwe kwa lugha zao za Kibantu.

Wachunguzi wa mambo wanasema kuwa wakati ule chama cha African National Congress (ANC), kilikuwa kinapigania uhuru na jeshi lake—Umkhonto Wesizwe, lilikuwa linaendesha vita vya mstuni dhidi ya serikali ya chama cha kifashisti cha National Party.

Miaka 30 baadaye, wanafunzi wa nchi hiyo, wamerudi tena mitaani, lakini safari hii wakiidai serikali inayoongozwa na ANC, wapewe elimu bure hadi chuo kikuu. ANC ambacho waliowengi wanakiona ni chama cha ukombozi, kinalitumia Jeshi la Polisi, kama walivyofanya Makaburu, kupambana na wanafunzi wanaharaki wa Kiafrika.

Ukiitazama hali inayojitokeza Afrika Kusini, sio tofauti na hapa Tanzania. Chama cha Mapinduzi (CCM), ambacho kinadai ni mrithi wa chama cha ukombozi cha Tanganyika African National Union (TANU), kimegeuka kuwa chama kandamizi, serikali yake inalitumia Jeshi la Polisi kukandamiza vyama vya upinzani.

Haihitaji kwenda mbali kutoa mifano kwa sababu mara nyingi tumeshuhudia chama hicho kikibebwa na ‘State Aparratus’, hasa wakati wa uchaguzi. Tumeyaona yaliyotokea wakati wa kampeni na uchaguzi wa Oktoba, 2015, jinsi vyombo vya dola vilivyotumika na vinaendelea kutumika kukandamiza demokrasia—hasa kwa upande wa Zanzibar—Serkali inatumia nguvu nyingi kutaka kukifuta Chama cha Wananchi (CUF).

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kilipotangaza kwamba kitarudi kwa wapiga kura kuwashukuru kwa kukiamini na kukipa kura nyingi wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita, Serikali inayoongozwa na CCM, ikapiga marufuku mikutano ya hadhara kwa kisingizio kuwa wananchi watakuwa hawana muda wa kufanya kazi.

Lakini ni ukweli kwamba chama tawala kilipata mchecheto—hakikuwa na uwezo wa kujibu mapigo kwa sababu kilitumia fedha nyingi sana katika kampeni—ikiwa ni pamoja kuwanunua wasanii wengi ili kunogesha kampeni.

Wapinzani kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), wameungana kupinga marufuku ya kufanya siasa—wanasema kufanya siasa ndio kazi ya vyama vya siasa. Chadema wakasema watafanya maandamano nchi nzima kuendesha kupinga udikteta. Ukaibuka mvutano mkubwa wa kisiasa. Serikali ikaonesha nguvu zake kwa kumwaga polisi mitaani kwa kisingizio cha kufanya mazoezi.

Wananchi walishuhudia mambo ambayo hawajawahi kuyaona toka nchi yetu ipate uhuru—askari waliovalia silaha mbali mbali, wengine wakiwa wamepanda farasi na wengine wamebeba mbwa wa polisi—wakifanya mazoezi ya kijeshi.

Isingengekuwa busara ya viongozi wa Chadema kukubali ushauri wa viongozi wa dini wa kusitisha zoezi la maandamano—yaliyotokea SOWETO kati ya 1976/86, ingekuwa cha mtoto.

Askari walikuwa na kila aina ya silaha kama walivyokuwa askari wa utawala wa kibaguzi wa Afrika Kusini. Haingii akilini kwamba vijana wa Jeshi la Polisi, walikuwa wameandaliwa kuwavunja vunja raia, kuwajeruhi, kuwakata ngwara na kuwasweka rumande, kama kwamba walikuwa wahalifu.

Ninapo angalia harakati za wanafunzi wa Afrika Kusini, nawasikia wakiimba na kucheza ‘“toyi-toyi”—aina ya dansi ambayo ilitumika wakati wa kupinga uonevu wa serkali ya Makaburu. Nawakumbuka wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambao waliandamana huku wakiimba: Asingekuwa Nyerere wangesoma wapi—maana wakati wa Nyerere—elimu ya msingi na ya juu, ilikuwa bure. Vijana wale nao wakapigwa virungu na mabomu.

Wanafunzi wa Afrika Kusini wanadai kuwa gharama za elimu ya juu ni kubwa sana na ni ya kibaguzi—kwa sababu inawafungia nje vijana wengi wa Kiafrika. Waandamaji wanadai serikali itoe elimu bure, kwa kuwa itasaidia kupunguza tofauti iliyopo kati ya Wafrika na Wazungu.

Kama CCM na ANC, vimekuwa vikijinadi kama vyama vinavyowajali wananchi, na kila uchaguzi vina ahidi na kuchaguliwa kwa matumaini kwamba vitahakikisha kuwa serikali zao zitatoa huduma nzuri za afya na za bei nafuu, elimu bure, huduma za makaazi na ujenzi wa miundombinu—hasa barabara za kwenda vijijini.

Vija wa Afrika Kusini ambao wanaendesha vuguvugu chini ya Kauli Mbiu ‘FeesMustFall’—wanazidi kupata nguvu na wanaungwa mkono na wanafunzi wa vyuo vikuu, watu mashuhuri na baadhi ya mashirika makubwa nchini humo.

Hapa Tanzania vijana wametulia kidogo baada ya Serkali ya awamu ya tano kutangaza elimu bure katika shule za serkali, lakini je, inatekelezeka, au ni sehemu ya mchezo wa kisiasa? Watu wanafurahi uwingi wa watoto walioingia Darasa la Kwanza mwaka huu, hawaangalii kama watoto wanapata elimu bora!

Wakati wa uongozi wa Mwalimu Nyerere, chama tawala cha TANU, mwaka 1974 kilitangaza Azimio la Musoma—kwamba watoto wote wenye umri wa kwenda shule wawe shuleni ifikapo mwaka 1977/78, lakini hapakuwa na maandalizi ya kutosha kama vile ikama ya walimu, vyumba vya madarasa, vifaa vya kufundishia na miundo mbinu ya kuyafanya mazingira ya kusomea kuwa rafiki kwa wananfunzi.

Mwitikio ulikuwa mkubwa sana, watoto takriban 400,000 waliingia Darasa la Kwanza nchi nzima. Lakini jinsi miaka ilivyokuwa inaenda, dhana ya Elimu Bure ikaanza kufifia.

Mwisho wa siku, wazazi wakalazimika kuchanga hela kwa ajili ya daftari, unifomu,ujenzi wa nyumba za walimu na madarasa, kununua vifaa vya michezo, madawati na hela ya kumlipa mlinzi na hivi mwishoni—hela ya twisheni.

Kwa kuwa kampeni ya kuchagiza madawati imefanikiwa kwa kiasi kikubwa, lazima ziatakuwapo changamoto ambazo mwisho wa siku—dhana ya Elimu Bure itafifia na kutoweka.

Iliwezekana wakati wa Mwalimu Nyerere, wanafunzi wa vyuo vikuu walikuwa wanapewa ‘bursary’ kwa mkataba kwamba wakimaliza masomo, wataitumikia Serikali kwa muda wa miaka mitano (5) kwa kuwa walikuwa wanaajiriwa moja kwa moja. Huo haukuwa mkopo kama ilivyo hivi sasa.

Mpango huu wa sasa wa Elimu Bure kwa wanafunzi wa shule za msingi, haukuwa na maandalizi—makosa yale yale ya mwaka 1974/77. Ilitakiwa itafutwe gharama halisi ya kumsomesha mwanafunzi wa shule ya msingi kutoka Darasa la Kwanza hadi la Saba na bajeti ya kutosha iwepo.

Ipo haja ya Serikali na wataalamu, pamoja na wadau wa elimu, kukaa pamoja na kutafuta mwafaka wa ni elimu gani watoto wetu wapatiwe—elimu ambayo ni ya kutenda na kuonesha matokeo (result oriented).

Nchi zinazotoa elimu bure hadi vyuo vikuu ni Ujerumani na Sweden, zinauwezo wa kufanya hivyo kwa sababu ni nchi zenye viwanda vingi. Na zinawatoza kodi kubwa wananchi wake kati ya asilimia 40 na 45 ya kodi ya mapato. Je, Tanzania au Afrika Kusini, zinao ubavu wa kutoa elimu ya juu bure?

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles