25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Wanafunzi wamng’oa meno mwalimu mkuu kwa ulawiti  

wanafunzi-wamngoa-meno-mwalimu-mkuu-kwa-ulawitiNa Walter Mguluchuma, Katavi

WANAFUNZI wa kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Usevya, Halmashauri ya Mpimbwe, mkoani hapa, wanadaiwa kumshambulia kwa kumcharaza viboko na kumng’oa meno mwalimu mkuu msaidizi kwa madai ya kulawiti wanafunzi.

Tukio hilo lilitokea Agosti 12, mwaka huu ambapo walimu wawili walijeruhiwa vibaya akiwamo Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule hiyo, Makonda Ng’oka ambaye ameng’olewa meno yake matano.

Inadaiwa chanzo cha tukio hilo ni wanafunzi wa kidato cha sita shuleni hapo kutomtaka mwalimu Ng’oka kuendelea kuwafundisha kwa madai kuwa ana tabia ya kuwadhalilisha wanafunzi wa kiume.

Akisimulia mkasa huo, mwalimu huyo alisema siku ya tukio alikuwa nyumbani na familia yake pamoja na mgeni aliyemtembelea ambaye ni mwalimu mwenzake aitwaye Gabriel Kambona.

Alisema ghafla waliingia wanafunzi hao wakiwa na silaha kama fimbo na marungu na kuanza kuishambulia familia yake na mgeni huyo.

“Muda huo mimi nilikuwa bafuni, ghafla nikasikia mayowe ya kuomba msaada, nilipotoka nikawakuta ni wanafunzi wanawashambulia watu na silaha, waliponiona wakanigeukia mimi na kunipiga hadi nikapoteza fahamu.

“Nilipozinduka nikajikuta nipo Zahanati ya Usevya, ndipo nikagundua nimepoteza meno yangu matano huku nikiwa nimejeruhiwa kichwani,” alisema mwalimu Ng’oka.

Aidha, mwalimu huyo alisema uhasama baina yake na wanafunzi hao umedumu kwa muda mrefu, lakini anashangaa uongozi wa Halmashauri ya Mpimbwe na Wilaya ya Mlele umeshindwa kumpangia kituo kingine cha kazi.

“Isitoshe uongozi wa halmashauri na wilaya haujawachukulia hatua yoyote wanafunzi hao, licha ya kupeleka majina yao kwani nawafahamu wote waliohusika, na ukweli ni kwamba siko tayari kukanyaga tena shule ile labda nipangiwe shule nyingine nje ya Katavi,” alisema.

Hata hivyo, wanafunzi hao walidai kuwa mwalimu huyo amekuwa akiwalawiti baadhi yao ikiwa ni adhabu mbadala wanapobainika kufanya makosa shuleni hapo.

Inadaiwa mwalimu huyo alishawahi kufikishwa mahakamani baada ya wanafunzi wa kiume wanaosoma shuleni hapo kumshitaki na kutishia kuandamana kupinga vitendo vyake vya kulawiti wanafunzi, lakini mahakama ilimwachia huru baada ya kukosekana kwa ushahidi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Walimu (CWT), Mkoa wa Katavi, Gregory Mshota, alikiri kufahamu tukio hilo.

Alisema CWT inawasiliana na uongozi wa halmashauri ya wilaya kuhakikisha mwalimu huyo anakuwa salama.

“Kwa sasa jambo hili halihitaji mjadala zaidi, kinachotakiwa ni mwalimu huyo kupangiwa kituo kingine cha kazi ili kunusuru uhai wake, na uamuzi huu ulipaswa ufanyike mapema,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles