WANAFUNZI WAJAWAZITO KURUDI SHULE PASUA KICHWA

0
716

SAID ABDALLAH (OUT) NA TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM

ALIYEWAHI  kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mwantumu Mahiza, amewataka wanafunzi wanaobeba ujauzito kabla ya masomo yao kujiendeleza kupitia mfumo usio rasmi.

Ameshauri wanafunzi hao baada ya kujifungua wajiunge na Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Walioikosa (MEMKWA) kwa shule za msingi  na Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES).

Mwantumu alisema wanafunzi hao wanaweza kujiunga pia na Mpango wa Elimu ya Mafunzo ya Ufundi Stadi  na Mpango wa Uwiano Kati ya Elimu ya Watu Wazima na Jamii (MUKEJA).

Naibu waziri huyo wa zamani ametoa kauli hiyo siku chache baada ya Rais Dk. John Magufuli kusema kuwa ndani ya utawala wake hakuna mwanafunzi atakayepata mimba na baadaye kuruhusiwa kurudi shuleni.

Rais Magufuli alizijia juu taasisi zinazotetea utaratibu wa wanafunzi kurudi shule baada ya kujifungua, huku akizitaka kufungua shule zao za wazazi na si kuilazimisha Serikali.

Mwantumu alitoa kauli hiyo alipokuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari waliotaka kujua msimamo wake kuhusu wanafunzi wanaobeba ujauzito kutokuruhusiwa kurejea masomoni.

Katika maelelezo yake, Mwantumu alisema kwa mujibu wa utafiti uliofanywa kipindi cha Serikali ya awamu ya nne, utoro uliosababishwa na ujauzito ni asilimia 0.5.

“Niwaombe wanafunzi waliozaa kujiendeleza kupitia mipango ya elimu isiyo rasmi kama mpango wa MEMKWA, MMES na MUKEJA,” alisema Mwantumu.

Alisema katika mipango hiyo, wanafunzi wanaruhusiwa kuingia darasani wakiwa na watoto wao na darasa linaendelea.

Mwantumu pia aliwaonya wanawake wanaojiingiza katika mapenzi na watoto wadogo ambao wako sawa na watoto wao.

“Naikumbuka vizuri kauli ya Rais wa awamu ya nne, Dk. Jakaya Kikwete.

“Aliwataka wanafunzi wa kike kuacha viherehere, kwa kuwa alitambua kuwa wengine wanabeba mimba kwa kujilengesha,” alisema Mwantumu.

Hivi karibuni, Taasisi ya HakiElimu, iliitaka Serikali kuharakisha kupitisha miongozo itakayowawezesha watoto wa kike wakijifungua kurejea shule.

Vilevile, taasisi kadhaa zilimtaka Rais Magufuli kutafakari upya katazo lake hilo, zikisema suala la ujauzito kwa wanafunzi linachangiwa na mambo mengi, ukiwamo umasikini na miundombinu ya baadhi ya shule nchini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here