Wanafunzi wa kike kupimwa ujauzito shule zikifunguliwa

0
663

NA ALLAN VICENT

UONGOZI wa Mkoa wa Tabora umesema utahakikisha wanafunzi wote wa kike wanapimwa ujauzito kabla ya kuanza kuingia darasani punde tu shule zikifunguliwa.

Agizo hilo limetolewa juzi na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri alipozungumza na walimu wakuu, maofisa elimu, wakufunzi wa vyuo na walimu wa shule za msingi na sekondari mkoani hapa.

Alisema baadhi ya wazazi na walezi wameacha watoto wao kuzurura ovyo mitaani badala ya kuwasaidia watulie nyumbani kujisomea, hali ambayo baadhi yao hujiingiza katika vitendo vya ngono na michezo mingine isiyofaa.

Mwanri alisisitiza janga la ugonjwa wa corona likipita, Serikali itafungua shule na vyuo ili kuruhusu wanafunzi kuendelea na masomo yao, hivyo akabainisha kuwa kabla ya kuanza masomo, wasichana wote watapimwa kama wana mimba, hivyo akawataka kujitunza vizuri kipindi hiki.

“Shule zitakapofunguliwa kazi ya kwanza tutakayofanya ni kuwapima watoto wa kike wa shule zote, yeyote atakayekutwa na ujauzito atachukuliwa hatua yeye na mzazi au mlezi wake,” alisema Mwanri. 

Alimwagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk. Honoratha Rutatinisibwa na waganga wakuu wa wilaya kujipanga vizuri kutekeleza kazi hiyo ya upimaji mimba.

Aliwataka wenyeviti  wa vitongoji na maofisa watendaji wa vijiji na kata kuelimisha wazazi na walezi kukaa vizuri na watoto wao katika kipindi hiki cha mapumziko ili kujiepusha na maambukizi ya virusi vya corona, ikiwemo kupata mimba.

Mratibu wa wajasiriamali wa mkoa huo, Asha  Mwazembe aliwataka wazazi na walezi wa watoto wote katika mkoa huo kuwachunga watoto wao katika kipindi hiki cha mapumziko ya dharura kabla shule hazijafunguliwa.

Alisema baadhi ya wanafunzi wameachwa huru kiasi hata kusoma hawasomi, badala yake wamekuwa wakizurura mitaani.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here