23.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, July 24, 2024

Contact us: [email protected]

Wanafunzi Mkwapa wanavyosoma kwa hofu chini ya mikorosho

wanafunzi wakisoma chini ya mikoroshoNA FLORENCE SANAWA, MASASI

PAMOJA na utekelezaji wa sera ya elimu bure kuendelea kufanyiwa kazi mijini na vijijini bado hali ya miundombinu ya shule ni mbaya hatua inaonyesha wazi kufeli kwa zoezi la madawati hasa kwa shule za vijijini.

Wakati agizo hilo la madawati likiendelea kutekelezwa baadhi ya wanajamii wanashangaa na kuhoji uhalali wa madawati kutengenezwa na kufikishwa katika shule zao ambazo kwa sehemu kubwa hazina vyumba vya madarasa wala vyoo huku wanafunzi wakisoma kwa hofu chini ya miti.

Uwepo wa agizo hilo umezua maswali mengi hasa vijijini ambapo zipo shule ambazo zina ofisi za walimu na darasa moja hali ambayo inasababisha watoto kusomea chini ya miti huku wakiongezeka kwa idadi kubwa baada ya utekelezaji wa sera ya elimu bure.

Changamoto hizo ambazo kwa sehemu kubwa zipo vijijini hali inayonilazimu kufunga safari ambayo inanifikisha katika Shule ya Msingi Mkwapa, wwilayani Masasi mkoani Mtwara.

Shule hiyo ambayo ina madarasa manne huku ikiwa na darasa la awali hadi la saba inazua sintofahamu ya ujio wa madawati  ambayo baadhi ya madarasa yanafanyia vipindi vyake chini ya miti ya mikorosho.

Mazingira hayo yamelalamikiwa na wanafunzi kwakuwa huwalazimu kuwa likizo hasa nyakati za mvua ambapo hushindwa kusomea chini ya miti na kuwafanya kukimbia hovyo hivyo kuvuruga ratiba ya masomo shuleni hapo.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Baruani Makota, anasema hadi sasa wanafunzi 60 hawana mahali pa kusomea hasa darasa la awali, la tano na la tatu na kwamba wote husomea chini ya miti.

Anasema shule hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo uhaba wa madarasa na walimu  hali ambayo inawafanya wawe na ‘shift’ ambayo si ya kawaida ili kuhakikisha wanafunzi hao wanapata elimu.

Anasema  hadi sasa shule hiyo ina madarasa manne hali inayosababisha wanafunzi wa awali kusomea chini ya mti. Anasema shule ina wanafunzi 380 na ina walimu sita tu.

Hata hivyo anaongeza kuwa shule hiyo imekuwa na vyoo vya muda ambavyo ni matundu manne kwa wanafunzi wakati walimu hawana vyoo hali inayosababsiha wanafunzi wote 380 na walimu sita kujisaidia pamoja na hivyo kuhatarisha afya za watumiaji wa vyoo hivyo.

“Tunaiomba serikali iitizame kwa jicho lingine shule hii hasa wakati huu wa masika, mara kwa mara huwa tunakimbia na mazingira haya yanasababosha wanafunzi kutokuwa na uelewa wa kutosha.

“Watoto wa awali wanahitaji mazingira bora ya kusomea lakini hawana darasa hili jambo ni hatari sana kwani miti inaweza kudondoka ama wadudu wanaweza kuwadhuru pia,” anasema Makota.

Anasema mwalimu mmoja anafundhisha masomo 10 na kuhoji ni miujiza gani mwalimu afanye ili mtoto awe bora kuliko mwingine.

Mmoja wa walimu wa shule hiyo, Zenna Lionjo, anasema kitendo cha wanafunzi kusomea chini ya miti kimekuwa kikishusha uelewa wa mtoto kutokana na ufundishaji kuwa magumu hasa unapohitaji kumsaidia mtoto mmoja mmoja.

Anasema ufundishaji chini ya mti unasababisha mwalimu kushindwa kutoa ufafanuzi wa kutosha kwa maandishi kutokana na ufinyu wa ubao hivyo kumfanya mtoto awe na uelewa mdogo zaidi na kushindwa kupambanua kwa kirefu baadhi ya masomo hasa Hisabati.

Lionjo anasema serikali inatakiwa angalie shule za vijijini ambazo ziko pembezoni ikiwemo kupeleka vitendea kazi kwa walimu na wanafunzi ili kuweza kuboresha elimu ambayo kwa vijijini imekuwa ikisuasua.

Anasema uhaba wa walimu na madarasa umekuwa ukilazimisha wanafunzi kusoma kwa shida hali inayowafanya walimu na wazazi kushindwa kumudu kutatua changamoto hizo.

“Tunatumia ubao mdogo sana kutoa maelekezo kwa wanafunzi tena tukiwa tumeuning’iniza kwa kamba, hawawezi kumudu kuelewa kutokana na mazingira wanayosomea.

“Unajua hata ukiangalia hapa nilipo nafundisha somo la hisabati ubao wenyewe ndio huu hakuna vifaa vya kujifunzia, walimu nao ni changamoto kubwa tupo sita tu ambapo watano ni wa kiume na wa kike niko peke yangu,” anasema Lionjo.

Adamu Amasha ni mwanafuzi katika shule hiyo, anasema kukaa chini mara zote kumesababisha kushindwa kuumba herufi kutokana na mazingira wanayosomea.

“Tunasoma kwa shida sana hata kuandika tumekuwa tukiandika kwa tabu na miandiko yetu imekuwa haileleweki,” anasema Amasha.

Mwanafunzi mwingine Tabitha Filikisi, anasema shule hiyo ina changamoto ya miundombinu ambayo si rafiki kwa wanafunzi.

“Unajua mazingira ya shule yakiwa mabaya hata mwanafunzi wa kike hawezi kusoma kwa raha…hebu angalia chini palivyolowa (anamwonyesha mwandishi).

“Jana usiku mvua ilinyesha lakini asubuhi tumekuja kukaa palepale palipoloa hivi tutakuwa tunaelewa kweli? anahoji Filikisi.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Bernad Nduta, anasema wilaya hiyo imejipanga kutatua tatizo la madawati na miundombinu ya shule za msingi na sekondari.

Anasema hadi sasa wameshakarabati madawati 1,000 ambayo yameshaanza kutumika huku wakiendelea na utegenezaji wa madawati mapya.

“Hadi sasa tunasimamia kwa suala la madawati lakini tukimaliza tutaingia kutatua changamoto nyingine za elimu. Hatutaweza kuzimaliza kwa wakati mmoja lakini tunaamini kwa kasi hii tunaweza kuzipunguza,” anasema Nduta.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles