Wanafunzi kubomoa sanamu ya Cecil Rhodes kutaondoa ubaguzi?  

Wanafunzi wakishangilia kuondolewa sanamu ya Cecil Rhodes iliyokuwepo katika lango kuu la kuingilia Chuo Kikuu  cha Cape TownNa Markus Mpangala

NIMEFUATILIA kwa muda mrefu maandamno na matamshi mbalimbali ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Cape Town cha Afrika Kusini dhidi ya utawala wa zamani wa Wazungu wachache nchini humo.

Maandamano hayo yaliambatana na matamshi makali ambapo wanafunzi walikubali kukacha masomo yao ili kushiriki mpango wa kuondolewa kwa sanamu ya Cecil Rhodes iliyokuwa kwenye lango kuu la kuingilia chuoni hapo, huku azima hiyo ikitimia Aprili 9 mwaka huu.

Wanafunzi hao walipinga kwa muda mrefu na kuchagizwa kwa maandamano yasiyo na kikomo hadi sanamu hiyo iondolewe.

Wanafunzi hao walikuwa na madai yao kwamba kuendelea kuwapo kwa sanamu hiyo ni kudumisha fikra za ukoloni, ubaguzi na utumwa uliowahi kufanyika barani Afrika.

Wanachuo wa Cape Town waliona ni ishara ya kudumisha utumwa kwa sanamu ya Cecil Rhodes kubaki kwenye  mazingira ya chuo chao. Ikumbukwe sanamu hiyo iliwekwa rasmi mwaka 1934 na utawala wa kibaguzi.

Kwa mtazamo wa wanafunzi wa chuo hicho, sanamu ya Cecil Rhodes haikustahili kuwapo kwa kuwa ni kiini cha madhira waliyowahi kukutana nayo mababu zao.

Aidha, Cecil Rhodes anakumbukwa kama mtawala wa Kikoloni aliyekuwa anawakilisha serikali ya kikoloni ya Uingereza.

Rhoeds alitawala mataifa ya South Rhodes (Zimbabwe) na North Rhodes (Zmabia), pamoja na mafungamano yake na utawala wa Afrika Kusini katika karne ya 19.

Si wanafunzi peke yao bali hata baadhi ya wapigania uhuru wa Afrika Kusini walikuwa wanapinga  uwepo wa sanamu hilo chunoni hapo.

Mikakati ya kutoka kizazi kimoja hadi kingine imefanikiwa kuondoa sanamu hiyo ambayo inachukuliwa kwa tafsiri mbaya na wanajamii wengi ya watu weusi nchini humo.

Watu weusi wanaamini kuwa walibaguliwa katika misingi ya rangi zao na hivyo kunyimwa fursa mbalimbali za elimu, uchumi, jamii na kadhalika.

Aidha, walioendesha mpamabano na maandamano makubwa hadi kuondolewa kwa sanamu hiyo ni wanafunzi weusi si wale wenye asili ya Kizungu.

Inafahamika kuwa Jiji la Cape Town lina wakazi wengi wenye asili ya Kizungu na ndiyo mzizi wa chama cha kisiasa cha Democratic Alliance.

Hata hivyo, wengi wanaamini sekta ya elimu iliwanyima nafasi wanafunzi wa Kiafrika kusonga mbele kulitumikia taifa lao, kwa hiyo wameamua kufuta kila alama ya Wazungu ambao walikuwa wakikandamiza watu weusi.

Kampeni kubwa ya ‘Cecil Must Fall’ ilianzishwa na wanafunzi wa chuo hicho kupitia mitandao mbalimbali ikiwamo Kamusi Elezo (Wikiepedia) ambao unatoa fursa kwa wasomaji kuweka taraifa zaidi za jambo linalozungumziwa.

Rhodes si wa kwanza kupingwa bali wapo Wazungu wengine ambao wanatajwa kujihusisha moja kwa moja na ubaguzi wa rangi, ukandamiza dhidi ya watu weusi, ukoloni na kubinywa kwa haki za binadamu ikiwamo kujipatia elimu.

Baadhi ya sanamu zilizopingwa na kusababisha maandamano ni ya Paul Kruger (rais wa zamani wa Afrika Kusini) iliyokuwapo jijini Pretoria.

Kufuatia wanafunzi wa Kiafrika kupinga sanamu za Kizungu, nao Wazungu wakaanza kupinga sanamu za viongozi wa zamani wa Kiafrika ambao walikuwa wakiendesha mapambano yaliyowakandamiza Wazungu.

Kruger alikuwa kiongozi mashuhuri wa Afrika katika karne ya 19 na alipingwa na wanafuzni wa Kizungu nchini Afrika Kusini kwa madai alikuwa akiwakilisha ubaguzi dhidi ya Wazungu.

Sanamu nyingine ni ya Jan Van Riebeeck iliyokuwapo Cape Town nayo ilisababisha ghasia na maandamano makubwa.

Van Riebeeck alikuwa mkoloni aliyewasili Afrika Kusini Aprili 5, 1652 akitokea nchini Uholanzi. Kiongozi wa chama cha siasa cha Economic Freedom Fighters, Julius Malema, alikuwa mstari wa mbele kuungana na wanafunzi kote nchini Afrika Kusini waliokuwa wakipinga kubakishwa kwa sanamu za viongozi wa Kizungu ambao wanadaiwa kuwakilisha ubaguzi.

Hata hivyo, Serikali iligoma kukubaliana na makundi yaliyokuwa yakipinga sanamu hizo, kabla ya kushindwa dhidi ya waandamanaji.

Sekta ya elimu imekuwa ikikumbwa na kumbukumbu mbaya ambazo zinawafanya vizazi vya watu weusi na Wazungu kupigania uponyaji wa mateso ya kisaikolojia yaliyosababishwa na watawala wa zamani.

Wanafunzi wenye asili ya Kizungu wanaowania watawala wakorofi wa Kiafrika waliopambana na kuwanyanyasa Wazungu ni wabaguzi, hali kadhalika wanafunzi wa Kiafrika wanaona sanamu za Kizungu ni kuendeleza ukoloni na kuabudu ubaguzi uliokuwa ukifanywa miaka ya nyuma.

Hata hivyo, swali ninalobaki nalo ni kwamba maandamano na mnyukano kama huo unawasaidia kukuza elimu au kujenga matabaka kulingana na jamii wanazotoka?

Je, kuondolewa kwa sanamu hizo kunawasaidia wanafunzi wa Kizungu na Kiafrika kusoma kwa uhuru au kinyume chake?

Mwisho wa matatizo hayo ni kwamba wanafunzi wa Kizungu na Kiafrika pamoja na jamii zao watajikuta wakiwa hawana njia nyingine zaidi ya kuweka mkazo kwenye mustakabali wao wa pamoja kama Taifa.

Mustakabali wa Afrika Kusini unawahusu jamii zote bila kujali wanakotoka iwe Waholanzi, Waingereza, Wahindi, Wayahudi na wengineo ambao ni raia halali wa nchi hiyo.

Elimu ni watu na watu ndiyo elimu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here