26.1 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Wanafunzi elimu ya juu kilio mikopo

Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako.

Na JONAS MUSHI, DAR ES SALAAM

WAKATI Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ikitangaza nafasi 5,398 za wanafunzi waliokosa mikopo kukata rufaa, wanafunzi wa vyuo vikuu wamelalamikia  wenzao wapatao 600 wamenyang’anywa mkopo.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Waziri wa Mikopo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Abdul Nondo, alisema awali wanafunzi 3,666 walikuwa wamepata mkopo lakini baada ya upangaji mpya wamepungua hadi kufikia 3,072.

Awali, Bodi ya Mikopo ilipanga kutoa fedha za kujikimu kulingana na asilimia aliyopata mwanafunzi na kusababisha baadhi ya wanafunzi kupata fedha kidogo za kujikimu.

Baada ya malalamiko ya wanafunzi, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, aliitaka bodi kuondoa utaratibu huo na kuwalipa fedha za kujikimu kwa usawa kwa wanufaika wote.

Lakini jana, Nondo alisema   wanafunzi waliondolewa kwenye mkopo wameathirika kwa kiasi kikubwa ikizingatiwa   wengi wao walikwisha kulipia kiasi cha ada na hawana uwezo wa kumalizia ada iliyobaki.

“Ukosefu wa mikopo utarudisha wanafunzi wengi nyumbani na hawa ambao walishalipia kiasi cha ada iliyobaki baada ya awali kuona kuwa wamepata mkopo   hivi sasa hawana fedha za kumalizia ada yao,” alisema.

Nondo alisema zaidi ya asilimia 90 ya wanafunzi waliopata mikopo hawajapangiwa fedha za kujikimu wakati wa kwenda kufanya mafunzo kwa vitendo.

Alisema wizara yake imekusudia kupeleka mapendekezo katika Wizara ya Elimu Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi ikiwamo kuongeza bajeti ya mikopo ya wanafunzi ili wengi waweze kuipata.

Mapendekezo mengine ni mkopo wa awamu ya pili utolewe haraka, kuwarejeshea mikopo waliokuwa wamepata awali na kuzingatia wanafunzi waliosoma diploma na  waliorudia elimu ya sekondari.

Rais wa Serikali ya wanafunzi wa Taasisi ya Usimamizi wa Fedha (IFM), Kilonzo Mringo, alithibitisha idadi ya wanafunzi watakaopewa mkopo imepungua.

Ameitaka  Serikali kutoa mikopo kwa wahitaji wote badala ya kuangalia bajeti.

“Wanafunzi wanapata shida, mwanzo waliambiwa wamepata mikopo na sasa  wanaambiwa hawana tena mkopo unaweza kuona wakati mgumu walionao,” alisema Mringo.

MTANZANIA ilimtafuta Mkurugenzi wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Abdul-Razaq Badru,   kutoa ufafanuzi wa mabadiliko hayo.

Alisema maboresho yaliyofanywa yamewanufaisha wenye uhitaji zaidi.

“Naomba nitumie mfano huu; una gari limejaa abiria wengi hadi limeshindwa kutembea katika kupunguza watu.

“Lazima tuangalie mwenye matatizo zaidi na wazee, watoto na wagonjwa ndiyo wataanza kupewa nafasi na wengine inabidi washuke.

“Tuliporekebisha zile kasoro za awali na kuamua wanafunzi wote wapewe fedha za kujikimu zinazolingana wale waliokuwa na fedha kidogo wameongezewa.

“Hivyo lazima idadi itapungua na katika kupunguza tumeangalia wale ambao hawana uhitaji sana tukawaondoa,” alisema.

Alisisitiza kwamba lengo la serikali ni kutoa mikopo kwa wanafunzi 25,717 tu ambao wana uhitaji zaidi kuliko wengine kwa kuangalia vigezo vilivyowekwa.

Awali Badru alisema  Bodi  imefungua dirisha la rufaa kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliokosa mikopo katika awamu ya kwanza.

Hiyo itakuwa ni awamu ya pili ambako mwanafunzi yeyote ambaye hakuridhika na utolewaji wa mikopo anapewa fursa ya kukata rufaa wakiwamo waliodahiliwa na TCU katika awamu ya nne.

Alisema dirisha hilo litafunguliwa kwa siku 90 kuanzia Novemba 2 mwaka huu.

Alisema rufaa hizo zitajaza nafasi 5,598 ili kufikia lengo la kutoa mikopo kwa wanafunzi 25,717 wa mwaka wa kwanza  kwa mwaka huu baada ya kutoa kwa wanafunzi 20,391 katika awamu ya kwanza.

“Baada ya kukamilisha upangaji na utoaji mikopo kwa awamu ya kwanza yenye wanafunzi 20, 391 wa mwaka wa kwanza, bodi inaandaa awamu ya pili ya ya upangaji mikopo  kukamilisha lengo la kutoa mikopo kwa wanafunzi 25,717 wa mwaka wa kwanza kwa mwaka huu 2016/17,” alisema Badru.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles