Wanafunzi 9,450 waliokosa nafasi sekondari Iringa, Dar wapangiwa shule

0
1028

BRIGHITER MASAKI Na FRANCIS GODWIN-DAR, IRINGA

WANAFUNZI 9,450 waliofaulu darasa la saba mwaka jana katika mikoa ya Dar es Salaam na Iringa na kushindwa kupangiwa shule kutokana na kutokamilika kwa miundombinu, hatimaye wamepangiwa shule na wametakiwa kuripoti kesho.

Wanafunzi hao ni 5,970 kwa Dar es Salaam na Iringa 3,480.

DAR ES SALAAM

Akizungumza na vyombo vya habari Dar es Salaam, Katibu  Tawala wa Mkoa, Abubakari Kunenge, alisema wanafunzi hao walishindwa kupangiwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo kutokamilika kwa miundombinu.

Alisema tayari wameshaifanyia kazi changamoto hiyo, hivyo jumla ya wanafunzi 74,940 watapata haki ya kuendelea na masomo ya sekondari.

Kunenge alisema wanafunzi wote waliofaulu wanatakiwa kuripoti shule walizopangiwa.

“Wanafunzi 63,937 walichaguliwa katika awamu ya kwanza kujiunga na shule za sekondari za Serikali, ambapo 5,970 walikosa nafasi.

“Wanafunzi wote wanatarajia kwenda kuripoti katika shule walizopangiwa kwa wakati na asiwepo atakayeacha kuripoti kwa namna yoyote ile.

“Wazazi wote wanatakiwa kuwaandaa watoto wao na kuwapeleka katika shule walizopangwa bila kukosa na haitakiwi kuwapo sababu yoyote ya kumfanya mtoto asiripoti alikopangwa kwa muda ulioainishwa,” alisema Kunenge.

IRINGA

Kwa upande wa Iringa, wanafunzi 3,480 wametakiwa  kuripoti shule kesho baada ya  nafasi kupatikana.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa, Lucas Kambelenje, alisema  ongezeko la ufaulu wa  wanafunzi mtihani wa darasa la saba limeibua changamoto  kubwa ya uhitaji wa vyumba  vya madarasa ili kuweza  kuchukua wote waliofaulu  kwenda sekondari.

Kambelenje alisema Mkoa wa Iringa ulikuwa na wanafunzi  25,325 waliosajiliwa kufanya mtihani wa taifa wa darasa la  saba mwaka jana, wakiwamo  wavulana 11,900 na wasichana  13,425 kwenye shule 493. Kati yao watahiniwa 24,998 wakiwamo wavulana 11,705 na wasichana 13,293 sawa na asilimia 98.7 walifanya mtihani  huo.

Alisema matokeo yalikuwa mazuri sana kwa watahiniwa 22,130 wakiwamo wavulana  10,324 na wasichana 11,806  sawa na asilimia 88.53.

Kambelenje alisema ufaulu huo ulikuwa wa kiwango kikubwa sawa na asilimia 5.3 ikilinganisha na matokeo ya  mwaka uliopita ambao ufaulu  ulikuwa ni asilimia 83.23.

“Mkoa wetu wa Iringa ulishika nafasi ya tatu kitaifa kati ya mikoa 26 ya Tanzania katika ufaulu wa wanafunzi wa darasa la saba.

“Ongezeko la ufaulu liliibua changamoto ya uhitaji  mkubwa wa vyumba vya madarasa katika shule za  sekondari,” alisema Kambelenje.

Alisema Halmashauri ya  Manispaa ya Iringa ilikuwa na  jumla ya watoto 893   waliofaulu na kushindwa kupangiwa katika shule yoyote  kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa.

Kambelenje alisema Halmashauri ya Iringa  wanafunzi 661 na Kilolo ni  wanafunzi 1,926 ambao  hawakuwa na uhakika wa  kuanza masomo ya sekondari  kwa wakati, huku Wilaya ya  Mufindi katika halmashauri  zake zote mbili watoto wote  walipata nafasi sekondari.

Alisema kutokana na  changamoto hiyo, ofisi ya mkuu wa mkoa wa Iringa na halmashauri ziliweka mkakati wa kukabiliana na hali hiyo ili   kuhakikisha wanafunzi wote   wanajiunga na kidato cha kwanza kwa wakati.

Alitaja mikakati hiyo kuwa ni  kukamilisha na kupata vibali  vya uanzishwaji wa shule za  sekondari mpya na hadi sasa ujenzi wa shule za sekondari  tatu umepata vibali ambazo ni  Mivinjeni iliyopo Manispaa ya  Iringa  na shule mbili za Makifu na Izazi zilizopo Halmashauri ya  Iringa.

Kambelenje alitaja mkakati mwingine kuwa ni ule wa upatikanaji wa nafasi wazi  katika shule za sekondari kwa  kutumia vyumba vilivyokuwa  vikitumiwa kwa shughuli  nyingine na pia kuweza  kuomba kibali cha kutumia  utaratibu wa wanafunzi  kusoma kwa awamu mbili kwa  siku (double shift).

Wanafunzi 701,038 sawa na asilimia 92.27 waliofaulu mtihani wa darasa la saba mwaka jana walipangiwa shule, huku wengine 58,699 wakikosa nafasi kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa katika mikoa mbalimbali nchini.

Alipokuwa akitangaza matokeo ya darasa la saba Desemba mwaka jana, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Selemani Jafo, aliagiza mikoa yote iliyokuwa na upungufu wa vyumba vya madarasa kuhakikisha wanatatua changamoto hiyo mapema ili wanafunzi hao waweze kuripoti kwa wakati.

Jafo alisema kuwa waliokosa nafasi walikuwa wanatoka katika mikoa 13, Dar es Salaam ikiwa miongoni mwa mikoa hiyo huku Kigoma  ikiongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi waliokosa nafasi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here