BRIGHITER MASAKI Na FRANCIS GODWIN-DAR, IRINGA
WANAFUNZI 9,450 waliofaulu darasa la saba mwaka jana katika mikoa ya Dar es Salaam na Iringa na kushindwa kupangiwa shule kutokana na kutokamilika kwa miundombinu, hatimaye wamepangiwa shule na wametakiwa kuripoti kesho.
Wanafunzi hao ni 5,970 kwa Dar es Salaam na Iringa 3,480.
DAR ES SALAAM
Akizungumza na vyombo vya habari Dar es Salaam, Katibu Tawala wa Mkoa, Abubakari Kunenge, alisema wanafunzi hao walishindwa kupangiwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo kutokamilika kwa miundombinu.
Alisema tayari wameshaifanyia kazi changamoto hiyo, hivyo jumla ya wanafunzi 74,940 watapata haki ya kuendelea na masomo ya sekondari.
Kunenge alisema wanafunzi wote waliofaulu wanatakiwa kuripoti shule walizopangiwa.
“Wanafunzi 63,937 walichaguliwa katika awamu ya kwanza kujiunga na shule za sekondari za Serikali, ambapo 5,970 walikosa nafasi.
“Wanafunzi wote wanatarajia kwenda kuripoti katika shule walizopangiwa kwa wakati na asiwepo atakayeacha kuripoti kwa namna yoyote ile.
“Wazazi wote wanatakiwa kuwaandaa watoto wao na kuwapeleka katika shule walizopangwa bila kukosa na haitakiwi kuwapo sababu yoyote ya kumfanya mtoto asiripoti alikopangwa kwa muda ulioainishwa,” alisema Kunenge.
IRINGA
Kwa upande wa Iringa, wanafunzi 3,480 wametakiwa kuripoti shule kesho baada ya nafasi kupatikana.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa, Lucas Kambelenje, alisema ongezeko la ufaulu wa wanafunzi mtihani wa darasa la saba limeibua changamoto kubwa ya uhitaji wa vyumba vya madarasa ili kuweza kuchukua wote waliofaulu kwenda sekondari.
Kambelenje alisema Mkoa wa Iringa ulikuwa na wanafunzi 25,325 waliosajiliwa kufanya mtihani wa taifa wa darasa la saba mwaka jana, wakiwamo wavulana 11,900 na wasichana 13,425 kwenye shule 493. Kati yao watahiniwa 24,998 wakiwamo wavulana 11,705 na wasichana 13,293 sawa na asilimia 98.7 walifanya mtihani huo.
Alisema matokeo yalikuwa mazuri sana kwa watahiniwa 22,130 wakiwamo wavulana 10,324 na wasichana 11,806 sawa na asilimia 88.53.
Kambelenje alisema ufaulu huo ulikuwa wa kiwango kikubwa sawa na asilimia 5.3 ikilinganisha na matokeo ya mwaka uliopita ambao ufaulu ulikuwa ni asilimia 83.23.
“Mkoa wetu wa Iringa ulishika nafasi ya tatu kitaifa kati ya mikoa 26 ya Tanzania katika ufaulu wa wanafunzi wa darasa la saba.
“Ongezeko la ufaulu liliibua changamoto ya uhitaji mkubwa wa vyumba vya madarasa katika shule za sekondari,” alisema Kambelenje.
Alisema Halmashauri ya Manispaa ya Iringa ilikuwa na jumla ya watoto 893 waliofaulu na kushindwa kupangiwa katika shule yoyote kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa.
Kambelenje alisema Halmashauri ya Iringa wanafunzi 661 na Kilolo ni wanafunzi 1,926 ambao hawakuwa na uhakika wa kuanza masomo ya sekondari kwa wakati, huku Wilaya ya Mufindi katika halmashauri zake zote mbili watoto wote walipata nafasi sekondari.
Alisema kutokana na changamoto hiyo, ofisi ya mkuu wa mkoa wa Iringa na halmashauri ziliweka mkakati wa kukabiliana na hali hiyo ili kuhakikisha wanafunzi wote wanajiunga na kidato cha kwanza kwa wakati.
Alitaja mikakati hiyo kuwa ni kukamilisha na kupata vibali vya uanzishwaji wa shule za sekondari mpya na hadi sasa ujenzi wa shule za sekondari tatu umepata vibali ambazo ni Mivinjeni iliyopo Manispaa ya Iringa na shule mbili za Makifu na Izazi zilizopo Halmashauri ya Iringa.
Kambelenje alitaja mkakati mwingine kuwa ni ule wa upatikanaji wa nafasi wazi katika shule za sekondari kwa kutumia vyumba vilivyokuwa vikitumiwa kwa shughuli nyingine na pia kuweza kuomba kibali cha kutumia utaratibu wa wanafunzi kusoma kwa awamu mbili kwa siku (double shift).
Wanafunzi 701,038 sawa na asilimia 92.27 waliofaulu mtihani wa darasa la saba mwaka jana walipangiwa shule, huku wengine 58,699 wakikosa nafasi kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa katika mikoa mbalimbali nchini.
Alipokuwa akitangaza matokeo ya darasa la saba Desemba mwaka jana, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Selemani Jafo, aliagiza mikoa yote iliyokuwa na upungufu wa vyumba vya madarasa kuhakikisha wanatatua changamoto hiyo mapema ili wanafunzi hao waweze kuripoti kwa wakati.
Jafo alisema kuwa waliokosa nafasi walikuwa wanatoka katika mikoa 13, Dar es Salaam ikiwa miongoni mwa mikoa hiyo huku Kigoma ikiongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi waliokosa nafasi.