25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

WANAFUNZI 2,300 WASHINDA RUFAA BODI YA MIKOPO

Na KULWA MZEE- DAR ES SALAAM


WANAFUNZI 2,348 kati ya wanafunzi 20,020, waliokata rufaa katika Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), wameshinda rufaa zao.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo, katika kipindi cha kati ya  Novemba mosi, 2016 na Januari 31, 2017, jumla ya rufaa 20,020 ziliwasilishwa kwa njia ya mtandao.

Kati ya rufaa hizo, fomu za rufaa zilizowasilishwa zikiwa na nyaraka ni 17,020 zilipokelewa kutoka vyuoni zikiwa na viambatanisho muhimu. 

“Mapitio ya rufaa zilizowasilishwa yalifanywa kwa fomu zote zilizopokelewa na matokeo ya rufaa zilizoshinda kwa makundi ni walemavu 61, yatima familia zenye kipato duni 1,169 na waliosomeshwa na wahisani ni 491

“Kwa hiyo, Bodi ya Mikopo tayari imetuma vyuoni majina ya wanafunzi walioshinda rufaa zao na inaendelea kukamilisha malipo ya mikopo yao.

“Pamoja na hayo, bodi inawataarifu waombaji na umma kwa ujumla, kuwa mchakato huo umefungwa rasmi hadi hapo utakapotangazwa tena katika mwaka ujao wa masomo,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Taratibu za upangaji na utoaji wa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, zinatoa fursa kwa waombaji ambao ama hawakupata mikopo au wamepata kiwango cha mikopo wanachoona hakikidhi mahitaji, kukata rufaa.

Kwa mujibu wa taratibu zilizopo, waombaji hupewa siku 90 kuanzia mwanzo wa mwaka wa masomo kuwasilisha rufaa zao. 

Rufaa hizo huwasilishwa kwa njia ya mtandao na vielelezo/viambatanisho huwasilishwa kupitia madawati maalum ya mikopo vyuoni. 

Rufaa hizo zilitokana na taarifa ya Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru, kusema wanafunzi 25,717 wa mwaka wa kwanza pekee, ndiyo watakaopata mikopo kwa mwaka wa masomo 2016/17 kati ya wanafunzi 58,000 ambao majina yao yaliwasilishwa kwake na Tume ya Vyuo Vikuu Nchini (TCU).

Mbali na hilo, alisema bodi hiyo pia ina hakiki majina ya wanafunzi 93, 295 waliokuwa wananufaika na mikopo hiyo ili kujiridhisha kama kweli walistahili kulingana na vipaumbele vya Serikali na watakaobainika kukosa sifa, wataondolewe kwenye mfumo na kutakiwa kurudisha fedha.

Kwa mujibu wa Badru, bodi ya mikopo baada ya kupitia taarifa za waombaji, iligundua kuna wanafunzi ambao historia zao zinaonyesha walisoma shule za gharama na wanapata mikopo, hivyo ni wakati wa kuachana na kundi hilo kama litakuwa halina vigezo husika.

Alisema uhakiki huo utaangalia vipaumbele vya Taifa, familia maskini, yatima, waliosomeshwa na taasisi na walemavu, hivyo wahusika wakiwa si katika makundi hayo wanaweza kufutiwa mikopo.

Kuhusu wanafunzi watakaonufaika na mikopo, alisema bajeti ya Serikali kwa mwaka 2016/17 ni Sh bilioni 483 itakayohusu wanafunzi 25,717 wa mwaka wa kwanza na wanaondelea ni 93, 295 ambao watakuwa katika uhakiki.

Alisema hadi sasa wanafunzi wa mwaka kwanza ambao wamepatiwa mikopo ni 20, 391 na orodha za majina hayo zimetumwa katika vyuo mbalimbali walivyopangiwa na TCU.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles