25.2 C
Dar es Salaam
Monday, August 15, 2022

Wanafunzi 230 wakatisha masomo kwa ujauzito

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Meck Sadiki.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Meck Sadiki.

Na Upendo Mosha, Moshi

WANAFUNZI 230 wa shule za msingi na sekondari mkoani Kilimanjaro wamekatisha masomo,baada ya kubainika ni  wajauzito tangu Januari hadi Agosti, mwaka huu.

Kutokana na hali hiyo, Serikali mkoani humo imeliagiza jeshi la polisi  kuacha kufanyakazi kwa mazoea na kuhakikisha linawakamata watuhumiwa wote  waliohusika kuwapa ujauzito wanafunzi hao na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria.

Kauli hiyo, imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Meck Sadiki, wakati wa sherehe za kuwapongeza na kuwakabidhi zawadi maofisa 34 wa jeshi la polisi waliohitimu kozi za uongozi jana.

Alisema wanafunzi wa kike 238 katika kipindi hicho, wameshindwa kuendelea na masomo kutokana na kupata ujauzito wakiwa shuleni jambo ambalo ni hatari na tishio katika utoaji wa elimu bora kwa mtoto wa kike.

Alisema jeshi la polisi halipaswi kufumbia macho suala hilo, bali lihakikishe watuhumiwa wote wanakamatwa.

“Januari hadi Mei, mwaka huu tulikuwa na wanafunzi wajawazito 77, lakini ripoti ya Agosti walipopimwa, tumekuta wameongezeka mpaka 238, jamani Taifa linapoteza wasomi.

“Wilaya inayoongoza ni Rombo,wanafunzi 60, sasa sijui mpaka  Desemba watakuwa wangapi maana ni kama wanashindana,Mei walikuwa na 24.Wilaya ya Same wapo zaidi ya 50, polisi hebu amkeni jambo hili si la kufurahia hata kidogo,”alisema Sadik.

Aliwataka wananchi kuacha mila potofu za kusuluhishana kimila pale inapobainika mtoto kafanyiwa unyama wa kupewa mimba,kubakwa au  kulatiwa, kwani kufanya hivyo kunaongeza matatizo.

“Kuna mila ya kupeana jani linaloitwa ‘mashale’ na kusuluhishana.. mila hii inawakandamiza watoto wa kike wanaopewa mimba”,alisema

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Willbroad Mutafungwa alisema wameanza kuchukua kwa kuwakamata baadhi ya watuhumiwa.

Alisema makosa ya kubaka na  kulawiti katika  mkoa huo, yameongezeka kwa kasi na kwamba kuanzia Machi hadi Agosti, mwaka huu  watoto 151 walibakwa na wengine 12 kulawitiwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,784FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles