29.8 C
Dar es Salaam
Sunday, September 15, 2024

Contact us: [email protected]

‘Akilimali avuliwe uanachama Yanga’

Mzee Ibrahim Akilimali
Mzee Ibrahim Akilimali

ADAM MKWEPU NA DOREEN PANGANI (TUDARCO), DAR ES SALAAM

MKUTANO wa dharura wa wanachama wa klabu ya Yanga, umeuomba uongozi wa klabu hiyo kuitisha kikao ili kumvua uanachama Katibu Mkuu wa Baraza la Wazee, Ibrahim Akilimali, kwa kitendo chake cha kutaka kuivuruga Yanga na uongozi wake.

Wanachama hao ambao walikutana jana asubuhi katika Makao Makuu ya klabu hiyo, waliliomba Baraza la Wadhamini kumvua madaraka kiongozi huyo kwa kitendo chake hicho kabla ya kuitishwa Mkutano Mkuu wa dharura wa wanachama wa klabu hiyo.

Uamuzi huo umekuja siku chache baada ya Mwenyekiti wa klabu hiyo kutishia kujiuzulu wadhifa wake katika klabu hiyo, huku Akilimali akituhumiwa kumtusi na kumkebehi Mwenyekiti huyo ambaye aliomba kukodisha klabu hiyo kwa miaka 10.

Akizungumza katika Mkutano huo Mwenyekiti wa matawi ya klabu hiyo jijini Dar es Salaam, Robert Kasela, alisema kwamba kabla ya kuvuliwa uanachama, Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Baraka Deusdedit, aitishe mkutano wa Baraza la Wadhamini wa klabu hiyo, ili kumvua madaraka kiongozi huyo kutokana na kitendo chake cha usaliti dhidi ya Mwenyekiti wao.

“Kitendo kilichofanywa na Akilimali kinalaaniwa na wanachama wa Yanga, tumetoa ombi la kutaka kufukuzwa uanachama kutokana na tabia hiyo ambayo ni ya kisaliti na inaonekana haina lengo zuri katika klabu.

“Tuendelee kuupa sapoti uongozi uliopo madarakani unaoongozwa na Mwenyekiti wetu, pia kwa sasa hoja zozote kutoka kwa wazee zipitishwe kwenye matawi yanayotambulika ya Yanga ili kujadiliwa kwanza.

Kwa upande wake Akilimali alikana tuhuma za kumtusi Mwenyekiti wake kwa kusema amekurupuka kwani neno hilo ni la kawaida na wala hakuwa na dhamira mbaya.

“Mie naomba tuwe na umoja kama awali, tatizo letu na Mwenyekiti ni kushindwa kutuita wazee kwenye mpango wake wa kuichukua timu kama alivyokua anafanya awali ambapo alikua akiwashirikisha katika kila jambo.

“Sina chuki na Mwenyekiti kwani niliwahi kushiriki kumweka madarakani hadi pale umma wa Watanzania waliposema tumevunja Katiba ya klabu.

“Ninachotaka alitambue Baraza la Wazee na sisi tukae naye tuzungumze mustakabali wa klabu yetu,” alisema Akilimali.

Alieleza bado anampenda kiongozi huyo na hayupo tayari aondoke, pia akaongeza kwamba wanahitaji aendelee na mfumo wa zamani wa kuthamini wazee.

Migogoro Yanga

Yanga imekua katika migogoro mbalimbali inayosababishwa na wanachama wake.

Migogoro katika klabu hiyo kongwe nchini imeanza siku nyingi lakini baadhi ya migogoro ya kukumbukwa ni ule wa mwaka 1972, uliosababisha baadhi ya wanachama kijitenga na kuzaliwa Pan African.

Mgogoro wa miaka ya tisini wa Katibu  George Mpondela (marehemu), aliyependekeza Yanga kuwa kampuni lakini alipingwa vikali na Mzee Akilimali.

Mgogoro mwingine ni ule wa Uongozi wa Yanga chini ya Rais Francis Kifukwe na mmoja wa wazee wa klabu hiyo, Yusuph Mzimba mwaka 2006, uliokuja kupatanishwa na Mwenyekiti wa sasa.

Mgogoro wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Yanga, Imani Madega na Mwenyekiti wa sasa, pia ule ilimwondoa Mwenyekiti Lloyd Nchunga, uliohusisha Jengo la Mafia na huu wa sasa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles