23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Wamwomba Lukuvi kuingilia mgogoro wao wa ardhi

Tunu Nassor -Dar es salaam

BAADHI ya wakazi wa Mtaa wa Amani katika Kata ya Kipunguni, Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam wamemwomba Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kuingilia kati mgogoro wa ardhi unaoihusu mipaka katika eneo hilo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika kikao chao na wapima ardhi wa Manispaa ya Ilala walioagizwa kuhakiki mipaka, wakazi hao wamesema mlalamikiwa Wilson Gabusha alipima eneo lake bila kushirikisha majirani jambo lililosababisha kuingilia mipaka ya majirani zake na kuyapima.

Mmoja wa wakazi hao, Aluwiya Shomary (Bi Shikoo) alisema eneo hilo linatambulika kwa mipaka ya asili ambayo mtuhumiwa aliikiuka.

Alisema wakati mtuhumiwa anapima eneo lake hakumshirikisha bali alikuja na wapimaji wake na kupima hadi katika eneo lake.

“Mipaka yetu ya asili inajulikana yeye alikuwa anaishia kwenye mikorosho yake lakini cha ajabu baada ya kupima inaonekana na maeneo yetu yapo ndani ya eneo lake,”alisema Aluwiya.

Naye Tulo Shemakange alisema kutokushirikishwa kwa wananchi katika eneo hilo kumesababisha maeneo mengi yanayozunguka eneo la mlalamikiwa kudaiwa kuwa mali yake.

“Tulifikisha kilio chetu kwa Waziri alipofanya mkutano wa hadhara pale Gongolamboto naye akatukabidhi kwa manispaa ya Ilala, lakini kinachofanyika hapa ni kuhalalisha mipaka ya mtuhumiwa hivyo tumamwomba waziri Lukuvi aje kututatulia suala hili,”alisema Shemakange.

Alisema eneo la Gabusha lilikuwa ekari nane pekee lakini sasa katika ramani yake inaonesha maeneo mengi ya wananchi yapo katika himaya yake.

Aliongeza kuwa wananchi wamekuwa hawana imani na mtaalamu wa upimaji aliyetumwa na Manispaa ya Ilala, Ramadhan Chamwiti kwa kuwa anachokwenda kukifanya ni kuhalalisha mipaka iliyomo katika ramani.
Alisema baada ya mwaka 2011 kulipima eneo hilo alijenga ukuta ambao wala haukufuata vipimo ambavyo vipo kwenye ramani jambo
ambalo hata wataalamu wa upimaji walilithibitisha hilo.  

Kwa upande wake, Gabusha alisema taratibu zote zilifuatwa wakati wa upimaji na bahati mbaya sheria inayotaka majirani kujaza fomu haikuwapo kipindi hicho.

“Nilifuata ngazi zote kuanzia serikali ya mtaa mpaka nikapata ruhusa ya kupima lakini sheria ya majirani haikuwapo kipindi hicho,” alisema Gabusha.

Naye Diwani wa Kata ya Kipunguni, Mohamed Msofe alisema kwa kuwa wananchi hawaridhishwi na mtaalamu huyo ni vyema kesi hiyo kurudishwa kwa Lukuvi ili aweze kutoa maamuzi.

Alisema shauri hilo limekuwa zito kutokana na pande zote mbili kutoridhiana, hivyo ni vyema kutumia busara kwa kuahirisha uwekaji wa mawe mpaka hapo waziri atakapotoa ufafanuzi.

“Ili kulinda amani katika eneo hili nikiwa kama mtawala naona pande zote mbili hazijaridhia kuendelea na shughuli hii ya uwekaji mawe ‘Beacon’ hivyo ni vema jambo hili lirejeshwe kwa waziri kwa hatua zaidi,”alisema Msofe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles