30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Wamisri kumaliza ubishi Yanga, Medeama

Pluijm akiwa na Obrey Chirwa.
Pluijm akiwa na Obrey Chirwa.

NA ADAM MKWEPU, DAR ES SALAAM

SHIRIKISHO la Soka barani Afrika (CAF), limepanga waamuzi kutoka nchini Misri kuchezesha mchezo wa Kundi A wa Kombe la Shirikisho Afrika kati ya Yanga na Medeama ya Ghana utakaochezwa Jumamosi katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas, alimtaja mwamuzi wa kati kuwa ni Ibrahim Nour El Din na wasaidizi, Ayman Degaish na Samir Ganal Saad huku Mohamed Maarouf Eid Mansour akiwa wa akiba.

Mechi kamishna wa mchezo huo ni Pasipononga Liwewe kutoka Zambia, Mfubusa Bernard wa Burundi amepangwa kuwa kiongozi wa waamuzi pamoja na Ian Peter Keith Mc Leod kutoka Afrika Kusini ambaye ni mratibu wa mechi.

Wakati huo huo, Kocha Mkuu wa timu ya Yanga, Hans van der Pluijm, ametamba kuwa sasa wachezaji wapo fiti kuivaa Medeama Jumamosi baada ya kufanya mazoezi ya nguvu tangu walipoingia kambini kwa maandalizi ya mchezo huo.

Mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, wamejichimbia kambini katika Hoteli ya Bahari Beach jijini Dar es Salaam, kujiwinda na mchezo huo baada ya kufungwa mara mbili na kupoteza pointi sita muhimu.

Yanga iliyopangwa Kundi A katika michuano hiyo, walianza vibaya kwa kipigo cha bao 1-0 ugenini dhidi ya Mo Bejaia ya Algeria kabla ya kufungwa bao 1-0 nyumbani dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) iliyoutema ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika na kuingia Kombe la Shirikisho.

Pluijm anayetamba kwa kuipa Yanga mataji mengi msimu uliopita, aliliambia MTANZANIA jana kuwa kikosi kimeimarika baada ya kuwapa wachezaji mbinu za kupiga mipira mirefu na mifupi, jinsi ya kulenga lango la wapinzani na kuimarisha sehemu ya kiungo.

“Tunakabiliwa na mchezo mgumu kwa kuwa na timu ngumu ya Medeama, tumejipanga kuondoka na pointi tatu baada ya kufanya maboresho kila idara iliyokuwa na tatizo, ingawa siwezi kutabiri kwani mchezo ni dakika 90,” alisema.

Hata hivyo, wachezaji wanne wa Yanga; Godfrey Mwashiuya, Haji Mwinyi, Deus Kaseke na Amissi Tambwe, bado wanasumbuliwa na majeruhi, huku Juma Mahadhi, Malimi Busungu, Donald Ngoma, Obrey Chirwa na Nadir Harub ‘Cannavaro’ wakiungana na wenzao kambini.

Kikosi cha Medeama kinatarajia kuwasili nchini kesho kwa ndege ya Shirika la Ndege la Kenya (KQ).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles