23 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 18, 2024

Contact us: [email protected]

WAMILIKI MITANDAO YA JAMII WAONYWA

Na MWANDISHI WETU
-DAR ES SALAAM
KAMATI ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imewataka wamiliki wa mitandao ya jamii kufuata maadili kwa kufanya uchujaji wa habari hasa katika kujadili faragha za watu.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Valerie Msoka, alikuwa akizungumza Dar es Salaam jana kwenye mkutano na wamiliki wa mitandao ya jamii.
Alisema baadhi ya habari zinazowekwa kwenye mitandao ya jamii hazina tija kwa jamii na wakati mwingine zimekuwa zikiingilia faragha za watu.
Mkutano huo ulikuwa na lengo la kuzungumzia namna bora ya upashanaji wa habari na utangazaji wa matukio yanayotokea kwenye jamii kupitia mitandao ya jamii.
“Wengine wamekuwa vyanzo vya habari kwa kujirekodi na kusambaza taarifa. Wengine wanasambaza picha za ajali ambazo zinamuonyesha mtu utupu ama akiwa na damu jambo linaloleta hofu kwa jamii.
“Kuanzia sasa tunapiga marufuku watu wanaorekodi matukio ya ajali na kuyasambaza kwenye mitandao, tunataka mitandao ifanye kazi kwa kufuata maadili ya nchi,” alisema Msoka.
Alisema kwa sasa teknolojia ya habari kwa njia ya mitandao imetoa fursa kwa mtu yeyote kuwa chanzo cha habari na kusababisha baadhi ya watu kuitumia vibaya mitandao.
Aliwataka wamiliki wa mitandao hiyo kuhakikisha inakuwa na vyanzo bora na vya uhakika kabla ya kusambaza habari na matukio mbalimbali.
Kuhusu matumizi ya lugha, alisema baadhi ya mitandao imekuwa ikitumia lugha chafu zisizo na staha kwa jamii na kusisitiza kuwa ni lazima izingatie matumizi sahihi ya Kiswahili.
Naye Mmiliki wa Mtandao wa Jamii Media, Maxence Melo, aliishauri mamlaka hiyo kuendeleza kampeni ya kukabiliana na matumizi mabaya ya mitandao maarufu kama ‘Futa-Delete-Kabisa’ ili kutokomeza usambazaji wa matukio yasiyofaa kwa jamii.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles