21.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 4, 2022

WAMILIKI MABASI WACHEKELEA WAZO SAFARI ZA USIKU KUANZA

Na LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM          |

SIKU chache baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, kumwagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro, kufika ofisini kwake kueleza sababu za mabasi kutosafiri usiku, Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa) kimefurahia hatua hiyo.

Lugola alitaka IGP Sirro na makamishna wake kumweleza kama polisi wamesalimu amri kwa majambazi na kuamua kusitisha safari za mabasi usiku pamoja na kufunga biashara mbalimbali saa 12 jioni.

Kutokana na hali hiyo, Katibu wa Taboa, Ernea Mrutu, alisema amelipokea agizo hilo kwa mikono miwili kwa sababu kilikuwa kilio chao cha muda mrefu, lakini bado yako mambo ambayo ni lazima wajadiliane kabla ya utekelezaji wake.

Alisema ili kufanikisha utaratibu wa mabasi kusafiri usiku, wanaweza kuanza kwa baadhi tu ya njia hasa ambazo magari yake hayakamilishi safari na kulazimika kulala njiani.

“Binafsi naamimi tuanze kwa baadhi ya njia kwa miezi miwili kama majaribio, tutaona kama inawezekana.

“Hata nyuma tulitaka lianze kwa baadhi ya barabara kwa sababu mabasi ya safari ndefu yamefungwa GPS, hatukutaka lianze ‘general’.

“Kwa mfano tunaweza kuanza na magari yanayotoka Mwanza, Musoma na Bukoba ambayo yanalazimika kulala Morogoro,” alisema Mrutu.

Aliongeza kuwa wakati wa kuanza utaratibu huo, lazima kuwe na masharti yatakayowabana madereva na wamiliki wa mabasi, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kila basi linakuwa na madereva wawili.

Mrutu aliongeza kuwa basi lolote litakalokutwa limechezewa mfumo wa kielektroniki wa kudhibiti mwendo, mmiliki na dereva wachukuliwe hatua.

“Naamini yako mambo ya kushirikiana ambayo tutayazungumza na waziri kwa sababu ameonyesha nia ya kutaka kukutana nasi, hata sisi hatutaki ajali zikatishe maisha ya Watanzania,” alisema Mrutu.

Aidha Mrutu alisema wakati wa utekelezaji wa mpango huo, ni lazima Jeshi la Polisi liwe tayari kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha usalama muda wote wa safari.

“Lakini ni lazima tufanye utafiti kufahamu kilichotuzuia awali kufanya safari hizi usiku na nini tumerekebisha ili tuanze kufanya hivyo sasa,” alisema Mrutu.

Mkurugenzi wa Udhibiti Usafiri wa Barabara wa Mamlaka ya Uthibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini, Johansen Kahatano, alisema suala hilo linawezekana, lakini linahitaji ushirikishwaji mkubwa wa Jeshi la Polisi ili kuimarisha usalama.

Kahatano alisma kuhusu udhibiti wa ajali, wamedhibiti kiasi cha kutosha ambapo karibu mabasi 1,600 nchini kote yamefungwa mfumo wa kudhibiti mwendo wa GPS, hivyo yanaweza kuonekana muda wote wa safari.

“Kimsingi linawezekana, kwa sababu ni suala la kujitayarisha tu, kwa ushirikiano kati ya Sumatra, polisi na wamiliki wa mabasi wenyewe,” alisema Kahatano.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania, Mchungaji Silver Kiondo, alisema wengi hawafungi biashara mapema kwa kuhofia usalama ila hulazimika kufanya hivyo kutokana na mazingira ya kufanyia biashara.

Alisema wafanyabiashara wanaoweza kufunga mapema kwa kuhofia usalama ni wale wanaofanya biashara meneo ya mipakani.

“Biashara nyingi zinafungwa mapema kutokana na ‘nature’ (asili) ya biashara yenyewe. Kuna biashara zinafungwa saa 12:00 jioni, lakini nyingi zinafungwa saa 2:00 usiku, inategemeana ni biashara gani.

“Ninachoweza kusema ni kwamba biashara nyingi zinafungwa kutokana na mazingira, kama hakuna umeme ni lazima biashara itafungwa. Umeme ni adui mkubwa wa biashara.

“Kwa mfano mtu anayefanya biashara ya kuuza vifaa vya elektroniki na anataka ‘ku-display’ picha kwenye vifaa hivyo na hakuna umeme, ni lazima atafunga biashara saa 12:00,” alisema Mchungaji Kiondo

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,654FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles