29.4 C
Dar es Salaam
Sunday, October 13, 2024

Contact us: [email protected]

WAMEPANIA

Sosthenes Nyoni -Dar es salaam

WAWAKILISHI wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika, timu za Simba, Yanga na KMKM, leo zitashuka dimbani kuzindua kampeni zao za michuano hiyo.

Simba na Yanga zinaiwakilisha nchi katika michuano hiyo mikubwa zaidi katika ngazi ya klabu, zikitokea Tanzania Bara, huku KMKM ikitokea visiwani Zanzibar.

Ilivyo Simba 

Wekundu hao wenyewe watakuwa ugenini jijini Beira,nchini Msumbuji kuumana na wenyeji wao UD Songo . 

Inashiriki michuano hiyo ikiwa inajiamini kiasi cha kutosha, hali hiyo inatokana na kufanya vizuri katika michuano iliyopita ilipofika hatua ya robo fainali, kabla ya kuondolewa na TP Mazembe.

Hata hivyo, kikosi cha safari hii kitakuwa  na baadhi ya sura mpya, baada ya usajili wa wachezaji kadhaa wapya.

Usajili huo mpya umelenga kuziba nafasi za wale walioitumikia timu hiyo msimu uliopita na sasa wameachana nayo kutokana na sababu tofauti ikiwemo mikataba kuisha.

Wachezaji wapya Simba walioko kwenye usajili wa Shirikisho la Soka Afrika(Caf), ni Deo Kanda kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo(DRC), Francia Kahata(Gor Mahia, Kenya), Tairone da Silva, Gerson Veira(Brazil), Sharaf Shiboub(Sudan) Beno Kakolanya, Gadiel Michael na  Ibrahim Ajib(Yanga).

Wachezaji hao ndio mbadala wa viungo Haruna Niyonzima na James Kotei, kipa Deogratius Munish ‘Dida’ na mshambuliaji Emmenuel Okwi.

Uongozi wa Simba haukuona umuhimu wa kurefusha mikataba ya Niyonzima, Dida na Kotei kutokana na kutovutiwa na viwango vyao, lakini kwa Okwi aliamua mwenyewe kutafuta changamoto mpya.

Uongozi wa Simba umeweka wazi nia yake ya kuhakikisha unapata mafanikio zaidi ya msimu uliopita katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kikosi cha wachezaji 19 wa Simba kilichoondoka jijini Dar es Salaam jana tayari kimetua Beira kikisubiri kuwavaa wenyeji wao.

Wachezaji walioifuata UD Songo, Kakolanya, Michael, Kapombe, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Shiboub na Kahata.

Wengine ni Meddie Kagere, John Bocco
,Clatous Chama, Ally Salim, Mohamed Hussein, Silva, Mzamiru Yassin, Veira, Kanda, Rashid Juma na Hassan Dilunga.

Nyota muhimu ambao hawajaambatana na kikosi hicho ni kipa wa kwanza Aishi Manula anayesumbuliwa na majeraha aliyoyapata wakati akiitumikia timu ya taifa(Taifa Stars) katika fainali za mataifa ya Afrika(Afcon), iliyofanyika nchini Misri kuanzia Juni 21 hadi Julai 19. Nafasi ya Manula  katika mchezo huo inatarajiwa kuzibwa na Kakolanya.

Mwingine ni Ajib ambaye pia ana majeraha aliyoyapata wakati akiichezea timu ya taifa(Taifa Stars) katika michezo ya kufuzu fainali za mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaochezaji ligi za ndani(Chan).

Katika kujiandaa na michuano hiyo, Simba ilipiga kambi ya  wiki tatu nchini Afrika Kusini na kucheza michezo minne ya kirafiki ya kujipima ubavu, ikianza kuumana na timu ya chuo kikuu  ya ORBIT TVET na kushinda mabao 4-0, ikailaza timu ya daraja la pili ya Platinum Stars mabao 4-0, ikalazimisha sare ya bao 1-1 na Township Rollers kabla ya kuhitimisha na sare nyingine ya bao 1-1 na Orlando Pirets.

Baada ya kumaliza ziara yake Afrika Kusini, ilirejea nyumbani na kucheza mchezo mmoja wa kimataifa wa kirafiki siku ya kilele cha tamasha la klabu hiyo maarufu Simba Day kilichofanyika Jumanne ya wiki hii, ikiivaa Power Dynamos ya Ligi Kuu Zambia na kushinda mabao 3-1, Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mbelgiji Patrick Ausseems amesema wana kila sababu ya kufanya vizuri katika michuano hiyo  kutokana na ubora wa kikosi chake.

Mchezo wa marudiano kati ya Simba na UD Songo utapigwa kati ya Agosti 23 na 25, mwaka huu, Dar es Salaam.

Ilivyo Yanga

Inarejea katika michuano ya kimataifa, baada ya kukosekana kwa miaka miwili.

Miamba hiyo ya Jangwani  yenyewe itapepetana na Townshipo Rollers, Uwanja wa Taifa.

Ili kuhakikisha inafanya vizuri, Yanga imefanya usajili wa zaidi ya wachezaji 10 wapya kuunganisha nguvu na wale walioitumikia msimu uliopita na kuziba nafasi za wale walioondoka.

Kwa upande wa wachezaji wa kigeni imewasajili Juma Balinya kutoka (Polisi, Uganda), Maybin  Kalengo(Zesco, Zambia), Patrick Sibomana(ARP, Rwanda),Issa Bigirimara(Mukura Sports, Rwanda), Sidney Urikhob(Namibia), Mustafa Selemani(Burundi), Farouk Shikalo(Bandari, Kenya)na David Molinga kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo(DRC).

Molinga na Balinya wamesajiliwa ili kuziba pengo la aliyekuwa mshambuliaji nyota wa timu hiyo raia wa DRC, Eritier Makambo aliyejiunga na klabu ya Horoya ya Guinea.

Kwa upande wa wachezaji wazawa waliosajiliwa katika kikosi hicho ni Mapinduzi Balama kutoka Alliance ya Mwanza, Ally Mtoni(Lipuli), Ally Ally(KMC), Muharami Issa Said(Malindi), Abdulaziz Makame kutoka Mafunzo ya Zanzibar.

Kujiweka fiti kwa ajili ya michuano hiyo, Yanga ilipiga kambi  mkoani Morogoro na kucheza michezo kadhaa ya kujipima makali kabla ya kurejea Dar es Salaam na kisha kwenda Zanzibar.

Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera amesema wachezaji wake sasa wameanza kuelewana katika kiwango ambayo yeye anakitaka, baada ya kutomfurahisha katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Kariobangi Sharsk ya Kenya.

 Mchezo huo uliochezwa Agosti 4 Uwanja wa Taifa, ikiwa ni siku ya kilele cha tamasha la klabu hiyo maarufu Wiki ya Mwananchi ulimalizika kwa sare ya bao 1-1.  

Baada ya sare ya Kariobangi, Yanga ilienda kambini Zanzibar kuivutia kasi Township.

Ikiwa huko, ilicheza michezo miwili ya kirafiki dhidi ya Mlandege na kushinda mabao 4-1 kabla ya sare ya bao 1-1 na Malinzi.

Ilivyo KMKM

Timu hii inayomilikiwa na Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo Zanzibar kitashuka dimbani Uwanja wa Amaan kukabiliana na D’Agosto ya Angola.

Kocha wa timu hiyo, Ame Msimu amesema wamefanya maandalizi ya kutosha ikiwemo kushiriki michuano ya Kagame nchini Rwanda,hivyo ana matumaini watafanya vizuri na kuandika historia mpya kwa klabu za Zanzibar.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles