25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, December 19, 2024

Contact us: [email protected]

WAMEKUMBWA NA KASHFA YA UKWEPAJI KODI HISPANIA

NA BADI MCHOMOLO



HABARI kubwa ambazo zimekuwa zikitikisa vichwa mbalimbali vya habari nchini Hispania ni baadhi ya mastaa kutuhumiwa kukwepa kodi.

Tuhuma hizo zimeanza kuvumbuliwa ndani ya misimu miwili sasa tangu mwaka jana.
Awali tuhuma hizo zilikuwepo kwa miaka ya nyuma lakini hazikuwa na moto kama ilivyo msimu wa mwaka jana na mwaka huu kutokana na watuhumiwa wa kodi kuwa na majina makubwa.

SPOTIKI leo hii imekuanikia baadhi ya mastaa ambao wamekubwa na kashfa ya ukwepaji kodi katika soka la nchini Hispania.

Lionel Messi
Huyu ni staa wa klabu ya Barcelona na timu ya Taifa ya Argentina, amekuwa akikipiga katika kikosi cha Barcelona tangu mwaka 2004 hadi sasa.

Mwaka jana mchezaji huyo na baba yake ambaye anasimamia mapato yake, Jorge Messi, walikumbwa na kashfa ya ukwepaji kodi wa zaidi ya bilioni 10.

Inadaiwa kwamba Messi alikuwa na kosa la kutolipa kodi za haki ya matangazo ya picha yake, huku ikidaiwa kwamba fedha za mchezaji huyo zikifichwa nchini Uruguay ili kukwepa kodi.

Kutokana na kesi hiyo Messi na baba yake walitakiwa kwenda kuitumikia jela kwa miezi 21 pamoja na kulipa faini, lakini kuna uwezekano mkubwa wa wawili hao kulipa faini badala ya kutumikia jela kutokana na kubebwa na sheria.

Sheria za nchini Hispania kwa makosa kama hayo zinasema kwamba, mtuhumiwa kama hakuwa na kosa la jinai awali na kesi yake ni kwenda jela chini ya miaka miwili basi atatakiwa kulipa faini bila ya kwenda jela.

Hicho ndicho kinachoweza kumfanya Messi na baba yake kutotumikia kifungo, lakini watatakiwa kulipa faini, lakini wataalamu wa soka walisema kwamba kashfa hiyo imemfanya Messi kuwa na mawazo na kupoteza kiasi cha uwezo wake uwanjani.

Cristiano Ronaldo
Staa mwingine wa klabu ya Real Madrid na timu ya Taifa ya Ureno, yeye ni mchezaji ambaye anashambuliwa kwa sasa kwenye vyombo mbalimbali vya habari juu ya kukwepa kodi mara baada ya kujiunga na Real Madrid mwaka 2009 akitokea Manchester United.

Taarifa za Ronaldo kukwepa kodi zimegunduliwa mwaka huu baada ya wachunguzi wa mapato nchini Hispania kufuatilia ulipaji wake wa kodi.

Kashfa hiyo imempa wakati mgumu Ronaldo ambaye amekuwa na mchango mkubwa ndani ya klabu hiyo pamoja na timu yake ya Taifa.

Ronaldo anadaiwa kukwepa kodi ya Pauni milioni 13, ambazo ni zaidi ya bilioni 36 za Kitanzania, hata hivyo kesi ya mchezaji huyo inatarajiwa kusikilizwa Julai 31 mwaka huu.

Kesi hiyo inamfanya Ronaldo atangaze kuwa anataka kuondoka ndani ya klabu ya Real Madrid huku akidai kwamba klabu hiyo haitambui mchango wake.
Hata hivyo Madrid wamesema wapo tayari kutoa ushahidi wa kumtetea mchezaji wao juu ya tuhuma hizo ambazo zinaendelea.

Jose Mourinho
Huyu ni kocha wa klabu ya Manchester United, ambaye amekuwa miongoni mwa mastaa wanaotuhumiwa kukwepa kodi nchini Hispania.

Yeye ameshutumiwa na maofisa wanaoshughulikia masuala ya kodi nchini humo huku wakidai alikwepa kulipa mwaka 2011 na 2012 alipokuwa akikinoa kikosi cha Real Madrid.

Ripoti hiyo ilidai kuwa Mourinho anadaiwa kiasi cha pauni milioni 2.9 (euro mil.3.3) zaidi ya bilioni 8 za Kitanzania.
Tuhuma hizo zimekuja baada ya wiki moja kupita tangu Ronaldo kuhusishwa na kukwepa kodi nchini humo.

Hata hivyo Mourinho amesisitiza kuwa hana wasiwasi na taarifa hizo ambazo zinamchafulia jina lake, lakini yeye anakumbuka kwamba alilipa zaidi ya pauni milioni 26 kwa kipindi chote alichokaa nchini humo ambapo ni sawa na asilimia 41.

Di Maria
Ni nyota wa klabu ya PSG, inayoshiriki Ligi nchini Ufaransa, na yeye huenda akatumikia kifungo cha jela mwaka mmoja kutokana na tuhuma za ukwepaji kodi wakati anacheza soka katika klabu ya Real Madrid.

Mchezaji huyo anatuhumiwa kukwepa kodi ya Pauni milioni 1.14, ambazo ni zaidi ya bilioni 2 za Kitanzania, ambapo kodi hiyo alitakiwa kuilipa tangu mwaka 2010 hadi 2014 wakati anacheza soka nchini humo.

Tayari Di Maria amefikishwa mahakamani na kuhukumiwa kwenda jela mwaka mmoja au kulipa faini ya pauni milioni 1.76, ambazo ni zaidi ya bilioni 2 za Kitanzania. Mchezaji huyo amekili kufanya kosa hilo na anatarajia kulipa faini badala ya kwenda jela.

Neymar da Santos
Ni nyota wa Barcelona na timu ya Taifa ya Brazil, kwa upande wake amekumbwa na kashfa ya ukwepaji kodi wakati wa uhamisho wake akitokea klabu ya Santos na kujiunga na Barcelona pamoja na kusaini mkataba na kampuni ya Nike mwaka 2013.

Kodi nyingine anayodaiwa ni kutokana na kampuni zake ambazo ni Neymar Sport e Marketing, N & N Consultoria, N & N Administracao de Bens), hivyo anatuhumiwa kukwepa kodi ya dola milioni 63.5 ambazo ni zaidi ya bilioni 143 za Kitanzania.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles