26.2 C
Dar es Salaam
Saturday, August 13, 2022

Wamefuata nyayo za Wenger

arsene-wenger-609836LONDON, England

MOJA kati ya makocha wenye heshima kubwa na waliojenga heshima yao kupitia mchezo wa soka nchini England, ni kocha Mfaransa, Arsene Wenger, kocha wa kikosi cha washika bunduki wa London Kaskazini, Arsenal.

Kocha huyo aliyeanza kukiongoza kikosi hicho msimu wa 1996, akitokea klabu ya Nagoya Grampus Eight iliyokuwa ikishiriki Ligi Kuu ya Japan, kutokana na kazi nzuri aliyofanya kocha huyo amedumu katika kikosi hicho mpaka hivi sasa.

Kati ya rekodi anayoshikilia ni ya kutopoteza mchezo msimu wa 2002-2003, akiwa na kikosi kilichokuwa na nyota wenye uwezo mkubwa kama Tony Adams, Patrick Vieira, Thiery Henry na Martin Keown.

Kutokana na kuvutiwa na ujuzi walioupata kutoka kwa Mfaransa huyo, wachezaji hawa wameamua kufuata nyayo zake.

 

THIERY HENRY

Nyota huyu Mfaransa alicheza kwa mafanikio katika kikosi cha Arsenal, akicheza jumla ya michezo 254 na kupachika mabao 174, hivyo kuweka rekodi ya mchezaji aliyepachika mabao katika historia ya klabu hiyo.

Staa huyo ambaye pia aliwahi kucheza kwa mafanikio katika klabu ya FC Barcelona pamoja na klabu ya Juventus, amekichezea kikosi cha timu ya Taifa ya Ufaransa jumla ya michezo 123 na kuzifumania nyavu mara 51.

Mchezaji huyo alistaafu kusakata soka akiwa na klabu ya New York Red Bulls msimu wa 2014.

Hivi sasa nyota huyo ni kocha msaidizi wa kikosi cha timu ya Taifa ya Ubelgiji, akiwa msaidizi wa Kocha Mark Wilmots.

REMI GARDE

Moja kati ya makocha wenye majina makubwa hivi sasa ni Remi Garde, ambaye hivi sasa ni kocha mkuu wa klabu ya Olympic Lyon inayoshiriki Ligi Kuu ya Ufaransa.

Mfaransa huyo alipitia katika mikono ya Wenger, katika msimu wa 1996 na kuondoka mwaka 1999 akiwa moja kati ya wachezaji waliofanya vizuri katika kikosi cha Wenger.

Kocha huyo hivi sasa anakifundisha kikosi cha Aston Villa, akichukua nafasi ya Tim Sherwood aliyejiunga na Totenham Hotspurs.

TONY ADAMS

Ni nembo ya miamba hiyo ya London Kaskazini, akicheza kwa kujituma na kuacha alama katika kikosi cha Mfaransa huyo mwenye rekodi ya kutopoteza mchezo msimu wa 2003-2004.

Amekuwa akitabiriwa kuwa siku moja atapewa mikoba ya kukiongoza kikosi hicho cha washika bunduki wa London, amecheza michezo 504 na kuzifumania nyavu mara 32.

Mchezaji huyo alianza kazi ya ukocha katika kikosi kinachoshiriki Ligi Daraja la Pili cha Wycombe Wanderers nchini England, pia amezifundisha klabu kama Portsmouth na Gabala.

PAUL MERSON

Ni mchezaji ambaye alikuwa kipenzi cha kocha huyo Mfaransa, ambaye alimalizia soka lake katika kikosi cha Middlesbrough.

Alicheza kwa mafanikio katika kikosi hicho cha London Kaskazini, akicheza michezo 289 na kufunga mabao 78 ambaye alifuata njia za kocha wake kwa kuanza kuwanoa vijana wa Walsall.

DAVID PLATT

Ni kiungo raia wa England, ambaye alikuwa na uwezo na alitoa mchango mkubwa akiwa na kikosi cha kwanza cha miamba hiyo ya London Kaskazini, kwa kucheza michezo 88 na kufunga mabao 13.

Mara baada ya kustaafu, kazi yake ya kwanza ilikua ya ukocha akiwa na kikosi cha Sampdoria, lakini baadaye akajiunga na Nottingham Forest.

Pia kocha huyo aliwahi kufanya kazi na kocha Mtaliano, Roberto Mancini, alipokuwa na kikosi cha Manchester City kabla hajatimuliwa.

STEVE BOULD

Alikuwa mmoja kati ya mabeki hodari katika kikosi cha washika mtutu, alitengeneza kombinesheni nzuri na nahodha, Tony Adams.

Amekitumikia kikosi cha washika bunduki wa London kwa miaka 11, katika dimba la Highbury kati ya mwaka 1988 mpaka 1999, huku akicheza michezo 372.

Hivi sasa ni miongoni mwa makocha wanaokinoa kikosi cha vijana chini ya umri wa miaka 18.

DENNIS BERGKAMP

Ni jina ambalo likitajwa mashabiki wa Arsenal husimama kutoa heshima kwa gwiji huyo ambaye alifanya vizuri akiwa na kikosi cha miamba hiyo ya London.

Mara baada ya kustaafu soka, nyota huyo alirejea katika kikosi chake cha zamani cha Ajax kwenda kumsaidia kocha Frank de Boer kwa zaidi ya miaka minne.

Amecheza michezo 423 na kupachika mabao 120, katika kikosi cha Arsenal ambapo ametumia miaka 11 katika dimba la Highbury.

STEFAN MALZ 

Unamkumbuka nyota huyu? Ni moja kati ya wanaume wa shoka kutoka nchini Ujerumani ambaye kwa misimu miwili aliyocheza katika kikosi cha Gunners alicheza kwa mafanikio.

Aliondoka katika kikosi cha Arsenal msimu wa 2001, akiwa amecheza michezo 6 na kufunga bao 1 mara baada ya kushindwa kupata nafasi ya kikosi cha kwanza cha miamba hiyo.

Mchezaji huyo alianza kazi ya ukocha katika kikosi cha Niederkirchen, kinachoshiriki Ligi Daraja la Pili nchini Ujerumani.

NICOLAS ANELKA

Ni mchezaji wa Ufaransa aliyeitikisa dunia kwa kiwango chake maridadi, aliyecheza katika kikosi cha Arsenal kuanzia msimu wa 1997 mpaka 1999 alipotimkia Real Madrid.

Nyota huyo aliyekipiga katika klabu mbalimbali kama vile Liverpool, Manchester City, Chelsea, Bolton na West Bromwich Albion, alikuwa mmoja kati ya wachezaji wenye uwezo mkubwa.

Mfaransa huyo alienda kumalizia soka lake katika kikosi cha Shanghai Shenhua, mwaka 2012.

Hivi sasa nyota huyo anaifundisha klabu ya Mumbai City, inayoshiriki Ligi Kuu ya India.

OLEG LUZHNY

Alikua ni nyota wa kimataifa wa Ukraine, mmoja kati ya wachezaji wa kutumainiwa na kocha Wenger, katika msimu wa 2001/2 walipochukua kombe la Ligi Kuu ya England.

Mara baada ya mafanikio hayo, mchezaji huyo alienda kujiunga na Wolverhampton na alienda kumalizia soka lake katika klabu ya FK Venta, akiwa kama kocha mchezaji mwaka 2005.

Alianza kazi ya ukocha katika klabu ya Dinamo Kiev mwaka 2007, ambapo alishinda michezo yote ya nyumbani aliyokiongoza kikosi cha Kiev.

Alishindwa kufurukuta katika mashindano ya Europa mara baada ya kupangwa kundi moja na Manchester United, As Roma na Sporting Lisbon.

SILVINHO

Alikuwa beki wa kushoto wa  kutumainiwa wa timu ya taifa ya Brazil na washika mitutu wa London, Arsenal.

Aliondoka katika kikosi cha Wenger msimu wa 2009 -10 na kujiunga na matajiri wa jiji la Manchester, Manchester City, nyota huyo pia amepita katika kikosi cha FC Barcelona.

Alianza kazi ya ukocha chini ya Kocha Mtaliano, Roberto Mancini, katika kikosi cha Manchester City kama kocha msaidizi, baada ya hapo alijiunga na klabu ya Cruzeiro inayoshiriki Ligi Kuu ya Brazil kama kocha msaidizi pia.

Mchezaji huyo pia amepitia katika klabu nyingine kama Sport Recife, Nautico, Corinthians na Inter Milan inayoshiriki Ligi Kuu ya Italia.

LEE CANOVILLE

Anakumbukwa na mashabiki wa klabu ya Arsenal, kwa kuifungia bao la ushindi katika  mchezo wa kombe la ligi dhidi ya Ipswich Town walipoibuka na ushindi wa mabao 2-1 msimu wa mwaka 2000.

Mchezo huo ni wa kukumbukwa na mashabiki wa Arsenal, waliokuwa wakihitaji matokeo ya ushindi ili kuibuka mabingwa.

Mara baada ya kuachana na miamba hiyo ya London Kaskazini, nyota huyo alicheza klabu nane kabla ya kustaafu na kuanza kazi ya ukocha.

Lee alianza kazi ya ukocha akiwa na mchezaji mwenzake wa zamani wa klabu ya Arsenal, Jason Lee, kukifundisha kikosi cha Boston United, alishindwa kuendelea na kazi hiyo mwaka 2012 mara baada ya kuwa mgonjwa.

IGORS STEPANOVS

Nyota huyo alishinda mataji mawili ya Ligi Kuu ya England pamoja na kombe la FA, katika kipindi alichokaa na kikosi cha Arsenal dimba la Highbury alisumbuliwa na majeruha ya mara kwa mara ambayo yalishusha kiwango chake.

Mchezaji  huyo alidumu katika kikosi cha Arsenal kwa misimu minne, kabla ya kuachwa na washika mitutu wa London Kaskazini.

Alianza kazi ya ukocha katika klabu ya FK Jurmala, kama kocha mkuu kabla ya kupata kazi ya ukocha katika nchi ya Latvia akifundisha kikosi cha vijana chini ya umri wa miaka 17.

GIOVANNI VAN BRONCKHORST

Ni mmoja kati ya wachezaji wa daraja la juu, akiwa mchezaji ametwaa mataji mbalimbali akiwa na  klabu tofauti tofauti Barcelona, Rangers, Arsenal na Feyenoord.

Nyota huyo raia wa Uholanzi, alikuwa katika kikosi kilichoshindwa kutwaa Kombe la Dunia mwaka 2010  nchini Afrika Kusini, akiwa amecheza michezo 100 katika kikosi cha timu ya Taifa hilo.

Mara baada ya kustaafu kucheza soka, alichaguliwa na kuwa kocha wa kikosi cha vijana chini ya umri wa miaka 21 cha klabu ya Feyernood cha nchini Uholanzi.

Hivi sasa ni kocha mkuu wa klabu hiyo, inayoshiriki Ligi Kuu ya Uholanzi ya Eredivisie.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,625FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles