33.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, March 22, 2023

Contact us: [email protected]

Wamarekani wajivunia Bush mkubwa

JOSEPH HIZA NA MITANDAO

KUNA masomo mengi ambayo Wamarekani na wanasiasa wa sasa duniani wanaweza kujifunza kutokana na maisha ya George H.W. Bush, Rais wa 41 wa Marekani aliyefariki dunia Ijumaa iliyopita akiwa na umri wa miaka 94.

George Herbert Walker Bush maarufu kama Bush Mkubwa aliyeingia madarakani mwaka 1989, alitumikia kipindi kimoja tu baada ya kushindwa wakati wa uchaguzi aliokuwa akitetea kiti chake mwaka 1992.

Akionesha ujasiri tangu akiwa kijana mdogo jeshini, Bush ameondokea kuwa kipenzi cha wengi hasa mara baada ya kustaafu kwa kuwa mfano wa maisha aishiyo ikionesha sifa zake, uaminifu wake,kujitoa, uvumilivu, unyenyekevu na kutokuwa na vinyongo.

Tofauti na ondoko la shujaa mwingine wa Marekani aliyefariki hivi karibuni John McCain, ambaye kabla hajafa alimpiga marufuku Rais Donald Trump kuhudhuria mazishi yake, kutokana na uhasama wao wa muda mrefu uliochochewa na bezo alilotoa Trump kuhusu ushujaa wa Seneta huyo mkongwe wa Arizona.

Mke wa Rais aliyemtangulia Trump, Michelle Obama hivi karibuni alitoa kitabu akisema hatomsamehe Trump kwa kitendo chake cha kuibua uzushi kuwa mumewe Barack Obama hakuwa mzaliwa wa Marekani.

Lakini Bush mkubwa kama kawaida yake ameweka kando tofauti ya familia yao ya Bush na Trump, iliyochochewa zaidi wakati mtoto wake Jeb alipokuwa akichuana na Trump kuwania tiketi ya kukiwakilisha chama cha Republican wakati wa uchaguzi wa 2016.

Bush ambaye familia yake imetoa marais wawili na kujenga ukaribu na waliokuwa mahasimu wao wa kisiasa wa chama cha Democratic, Rais wa 42, Bill Clinton na Obama, alimkaribisha Trump, ambaye kila uchwao anakumbwa na ‘majanga’ yanayoshusha umaarufu wake katika mazishi yake.

Bush mkubwa ana sifa zinaonekana kukosekana mno katika maisha ya Wamarekani na zimekuwa zikiadhibiwa katika siasa, kwamba wanasiasa wenye sifa hizo wamekuwa waathirika wa siasa za maji taka.

Sifa hizo, maamuzi, heshima yake kwa watu na kujiandaa kushika urais zinatajwa kuwa sababu za kuweza kufanikisha masuala magumu ya kimataifa lakini akilaumiwa kushindwa yale madogo hasa ya nyumbani, kitu kilichomgharimu.

Hebu fikiria maumivu aliyopata kwa kushindwa kuendelea na kipindi cha pili, lakini akaja ondoa kinyongo kwa kutengeneza urafiki mkubwa na hasimu wake kisiasa aliyemwangusha katika uchaguzi huo, Bill Clinton.

Baba huyo wa Rais wa 43 wa Taifa hilo, George Walker Bush alikuwa rubani wa jeshi la anga wakati ule wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

Alikuwa mbunge, balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, China na Mkurugenzi wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) na Makamu wa Rais wa mihula miwili chini ya Rais Ronald Reagan.

Maisha yake na kumbukumbu zilizopo yana kielelezo muhimu kuonesha uongozi wa kweli, ambao unahusisha mara nyingi si tu kufanya maamuzi magumu, bali pia ujasiri kwa kutofanya vitu rahisi.

Moja ya vitu ambavyo historia itamkumbuka mbali ya ushindi wake wa urais mwaka 1988 na ule wa Vita ya kwanza ya Ghuba, ambao Marekani na jeshi lake la ushirika ilifanikiwa hapo Februari 1991 kutimiza lengo lake la  kuing’oa Irak kutoka Kuwait.

Ukiondoa hayo pia atakumbukwa kwa juhudi zake za kuliunganisha Bara Ulaya kwa kuuangusha ukuta wa Berlinulioigawa Ujerumani na Ulaya katika kambi mbili; Magharibi na Masharikizikiongozwa na Marekani na Urusi,

Haina maana kuwa Bush alikuwa mtu mkamilifu. Wanawake wanane waliwahi kujitokeza kumtuhumu kwa udhalilishaji wa aina mbalimbali ikiwamo kuwatomasa.

Alikuwa kwa wakati fulani kuegemea uchama badala ya kuweka mbele utaifa wakati akiwa Mwenyekiti wa Kamati yaTaifaya Chama cha Republican kipindi kile cha kashfa ya Watergate.

Na kampeni zake za urais mwaka1988, timu yake ilitumia tangazo lisilosahaulika dhidi ya mgombea urais wa Chama cha Democratic, Michael Dukakis ambalo lilikumbushia mtazamo hasi kuhusu weusi na kuzua hofu kuhusu weupe.

Hata hivyo, Bush hakutengeneza maadui wa kudumu miongoni mwa wapinzani wake wa kisiasa.

Licha ya kwamba alikuwa mwanasiasa na aliyeweza kuendesha kampeni ngumu na chungu ili tu achaguliwe, alikuwa mtu aliyeamini katika siasa za kistaraabu na imani kuwa hakuna haja ya kuchukia watu wala mizozo ya muda mrefu

Kwa mfano, Bush alitengeneza urafiki na mtu aliyesababisha aishie muhula mmoja, Bill Clinton licha ya  kwa asilimiamaumivu kwa kushindwa kutetea urais.

Alishukuru wakati alipoondoka Ikulu akiandika barua nzuri ya kumtia moyo Clinton kuwa atakuwa ‘Rais wetu’.

Katika zama zao za baada ya urais, Bush na Clinton waliunda timu moja iliyosafiri duniani kwa ajili ya masuala mbalimbali yaliyolenga amani na ustawi wa dunia, ikiwamo uchangishaji fedha za kukabili majanga.

Bush alizaliwa Julai 12, 1924 huko  Milton, Massachusetts, ambapo baba yake alikuwa mwekezaji katika benki na baadaye akawa Seneta wa Marekani.

Bush alijiandikisha katika Jeshi la Anga la Marekani alipotimiza miaka 18 na kuweka rekodi ya kuwa rubani mdogo katika jeshi hilo.

Alijitolea kupigana katika Jeshi la Wanamaji Vita Vikuu vya Pili vya Dunia baada ya kushambuliwa kwa Pearl Harbor.

Ni baada ya kupata mafunzo ya kuendesha ndege za kivita kabla ya kupewa majukumu vitani katika Bahari ya Pacific, ambako alishiriki katika vita dhidi ya Wajapani wakati ule wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.

Akiwa miongoni mwa marubani wachanga kabisa kuwahi kutokea Marekani, aliendesha ndege za kuangusha mabomu zinazoruka angani kutokea meli kubwa za kivita.

Moja ya matukio yasiyosahaulika katika maisha yake jeshini humo ni pale ndege yake ilipotunguliwa Septemba 1944 alipokuwa akielekea kuangusha mabomu.

Moshi ulijaa ndani ya ndege, cheche za moto zilianza kuteketeza mbawa zote mbili. Anakumbuka akisema: “Mungu wangu! Ndege hii italipuka.”

Aliendelea kuendesha ndege hiyo huku akivurumisha mabomu katika maeneo kadhaa ya shabaha.

Aliwaamuru wenzake wawili aliokuwa nao watangulie kujiokoa kwa miavuli kutoka kwenye ndege hiyo, lakini hao wote wawili hawakuweza kunusurika.

Akiwa amesongwa na moshi, alifanikiwa kuvaa mwavuli na kuruka kabla ya kuangukia kwenye kisiwa kimoja baada ya kugonga kichwa chake na sehemu ya nyuma ya ndege kwa sababu ya upepo wakati akiruka.

Bahati nzuri mno kwake, aliweza kuokolewa na nyambizi ya Marekani.

Baada ya kuondoka kwenye kikosi cha wanamaji mwaka 1945 kwa heshima, Bush alimwoa msichana mwenye umri wa miaka 18, Barbara Pearce na baadaye kwenda kujiunga na Chuo Kikuu cha Yale.

Baada ya kuhitimu masomo yake, yeye na familia yake walihamia katika Jimbo la Texas.

Ndoa yao ilidumu miaka 72 baada ya mkewe kufariki dunia miezi saba iliyopita na walifanikiwa kuwapata watoto sita.

Mwana wao wa kwanza, ambaye baadaye alikuja kuwa Rais wa 43 wa Marekani, Rais George Walker Bush, alizaliwa mwaka mmoja baadaye.

Kabla ya kufikisha miaka 40, tayari alikuwa milionea lakini Bush na mkewe Barbara walisononeka sana baada ya binti yao wa pekee kugunduliwa kuwa na maradhi ya kansa ya kukosekana kwa damu mwilini, Laukaemia na kumuondoa duniani baada ya miezi michache.

Kwa msaada wa Rais Richard Nixon, Bush aliteuliwa katika Baraza la Wawakilishi la Marekani mwaka 1966 na mwaka 1971 Nixon alimteua kama balozi wa Marekani kwa Umoja wa Mataifa, kabla ya kumpeleka China na baadaye ukurugenzi CIA.

Baada ya kutumikia kama balozi na baadaye mkuu wa Shirika la Upelelezi wa Marekani (CIA) na Mbunge, alianza harakati za kisiasa kuelekea kileleni.

Akiibuka kwa kivuli cha Reagan, Bush alijaribu kugombea urais kupitia tiketi ya Chama cha Republican mwaka 1980.

Licha ya kushindwa katika kinyang’anyiro hicho, mwanasiasa mwenzake wa chama cha Republican Ronald Reagan alimchagua kuwa mgombea wake mwenza.

Uzoefu wake wa sera za kigeni wakati wa Vita Baridi dhidi ya Muungano wa Kisovieti wa Urusi (USSR) ulimsaidia kuteuliwa.

Baada ya miaka minane kama makamu wa rais wa Reagan, Bush alijaribu kwa mara nyingine tena kugombea urais mwaka1988 na kushinda uteuzi wa chama cha Republican. Kisha akaenda kushinda katika uchaguzi wa Rais wa Marekani – na kuwa Rais wa kwanza kipindi cha miaka 152 kushika wadhifa huo akitokea umakamu wa Rais.

Bush alimshinda mpinzani wake wa Chama cha Democratic, Gavana wa Jimbo la Massachusetts, Michael Dukakis kwa asilimia 54 ya kura zote zilizopigwa.

Hata hivyo katika uchaguzi huo wa1988, Bush alifanya makosa mawili makubwa; kumchagua mgombea mwenza asiyejulikana: Dan Quayle, aliyekuwa Seneta wa hadhi ya chini kutoka Indiana.

Quayle alijulikana zaidi kimataifa kutokana na makosa aliyoyafanya kwenye hotuba na mazungumzo yake.

Pili; aliahidi wakati wa MkutanoMkuu wa chama cha Republican ulioidhinisha mgombea wake wa urais kuwa hataongeza kodi, kitu ambacho alienda nacho kinyume na hivyo kumgharimu.

Alitoa ahadi hiyo wakati anamshambulia na mpinzani wake wa Democratic, Michael Dukakis kuhusu sera yakeya kifedha.

‘Isomeni midomo yangu,’ aliwaambia wajumbe waliokusanyika. ‘Hakuna kodi mpya.’

Wakati huu ulikuwa wa kipekee kwa sababu hapo ndipo Serikali ya Muungano ya Kisovieti iliporomoka na ‘Ukuta waChuma’ uliohesabiwa kutenganisha Ulaya Mashariki na Ulaya Magharibiukaangushwa.

Bush aliapishwa kuwa Rais wa Marekani Januari 20, 1989, ambapo anakumbukwa kwa hotuba yake, pamoja na mambomngine akisema; “Siku ya dikteta imefikia mwisho”.

Baadaye mwaka huo tawala za Kikomunisti katika nchi tofauti za Ulaya zikapinduliwa na harakati za kidemokrasia kuibuka na kuhitimisha Vita Baridi.

USSR nao uliokuwa umesalia, ikasambaratika miaka miwili baadaye na kulifanya Marekani kukosa mpinzani kama taifa kubwa lenye nguvu ya kijeshi, kiushawishi na kiuchumi duniani..

Lakini pia kutokana na uwezo wake wa kidiplomasia Bush aliweza kumshawishi kiongozi wa USSR, Mikhail Gorbachev katika makubaliano mbalimbali.

Hatua hiyo, ilikuwa muhimu sana katika kulishughulikia suala la kuungana kwa Ujerumani baada ya kufunguliwa kwa Ukuta wa Berlin.

Bush ambaye alikuwa miongoni mwa watu wa awali waliounga mkono Muungano wa Ujerumani, alifanikiwa kutuliza hofu za Gorbachev juu ya muungano huo.

Kwa sababu hiyo, makubaliano yakasainiwa mwaka 1990 kati ya pande mbili za Ujerumani na washindi wa Vita vya Pili vya Dunia ambao ni Uingereza, Ufaransa, Urusi na Marekani.

Makubaliano hayo yalisafisha njiana pande mbili za Ujerumani zikaweza kuungana, kurejeshwa kwa uhuru kamili waUjerumani, kubaki kama mwanachama wa NATO na kuondolewa kwa wanajeshi wa USSR upande wa mashariki.

Bush alitumia nguvu ya kijeshi na kuamuru uvamizi wa Panama na kumtia mbaroni kiongozi wake aliye daiwa kuhusikana dawa za kulevya, Manuel Noriega, Desemba 1989.

Mtihani mkubwa kwa Bush ulijitokeza wakati Irak ilipoishambulia Kuwait ghafla Agosti 1990.

Bush aliunda muungano wa ushirika wa kijeshi chini ya uongozi wake,  ambao haukuwahi kushuhudiwa kabla, ukijumuisha pia mataifa kadhaa ya Kiarabu.

Rais wa Irak, Saddam Hussein alipokataa kuondoa wanajeshi wake nchini humo, Vita vya Ghuba ikaibuka rasmiJanuari 1991.

Alipoamua kuchelewesha hatua ya kijeshi ili kupata baraka ya Umoja wa Mataifa (UN), Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Marehemu Margareth Thatcher alimshutumu vikali na kumwambia ‘huu si wakati wa kuyumbayumba’.

Vita viligeuka kuwa ushindi mkubwakwa Marekani na washirika wake, Marekani walipongezwa na taifa kwa jumla lilifurahia hadhi iliyotokea kwa jeshi baada ya mapigano hayo.

Licha ya ushindi aliopata, ambao uliimarisha umaarufu wake kisiasa hadi asilimia 90, kikosi cha jeshi lake hilo la ushirika hakikuweza kuingia Mjini Baghdad kwenyewe ambapo kilimwacha Saddam Hussein kuendelea madarakani.

Kumpindua Saddam Hussein na Serikali yake kulitekelezwa na George W Bush, mwanawe Bush huyu mkubwa mwongo mmoja baadaye.

Licha ya kupata umaarufu miongoni mwa raia baada ya kumalizika kwa Vita vya Ghuba, umaarufu huo ulipotea haraka baada ya kushindwa kushughulikia masuala mazito ya ndani ya nchi huku uchumi ukiwa unaporomoka.

Bush alishindwa na Bill Clinton katika uchaguzi wa Rais wa mwaka 1992,  kwa sababu alikubali kuongezwa kwa kodi ya petroli, kodi watu wa kipato cha juu pamoja na kupandishwa viwango vya ushuru kwenye vitu vya anasa licha ya ahadi yake ya wakati wa uchaguzi ya ‘kutoongeza kodi mpya.’

Clinton alimlaumu kwa kuanguka kwa uchumi wa nchi, kukua kwa pengo kati ya matajiri na maskini pamoja na deni la kitaifa.

Timu yake ya kampeni haikuwa na mipango mizuri na wakati huo huo alitoka ‘amejeruhiwa’ wakati wa chaguzi za mchujo kuwania kukiwakilisha chama akichuana vikali na Pat Buchanan.

Wakati wa uchaguzi Bush hakuwa na nguvu za kukabiliana na mpinzani wake, Bill Clinton, aliyekuwa mchanga na aliyependwa na watu wengi.

Bush baadaye alikiri kuwa bidii aliyokuwa nayo  Clinton, gavana wa umri mdogo kutoka Jimbo la Arkansas na ambaye alitoa matumaini ya ndoto mpya kuu ya Marekani, yeye Bush hangeweza.

Baada ya kushindwa na Clinton, Bush alijitoa kutoka katika siasa na kuhamia mjini Houston na mke wake Barbara, ambako aliishi hadi kifo chake.

Mara kwa mara alieleza wazi hatamani kurudi katika siasa wala kuandikwa kwenye vyombo vya habari.

Mwisho

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere: Miaka 19 baada ya kifo chake (6)

HII ni sehemu ya sita ya hotuba ya Profesa Mark Mwandosya kwa Chuo Kikuu cha Comoro wakati wa Maadhimisho ya Miaka 19 ya kifo cha Mwalimu Nyerere, Moroni nchini Comoro, Oktoba 26, 2018.

Katika sehemu ya tano, tuliona pamoja na mambo mengine harakati za Mwalimu katika ukombozi wa nchi za Afrika hususani za kusini mwa bara. Mwalimu alikaribisha vyama vya kitaifa vya kupigania uhuru katika mataifa hayo ya mstali wa mbele kuweka makao makuu nchini Tanzania. Sasa endelea…

Likiwa eneo la kimkakati na kuwa mstali wa mbele katika mapambano ya kupigania uhuru na dhidi ya ukandamizaji wakati wa miaka ile ya awali ya uhuru, Mbeya ilikuwa lango la kuingilia Tanzania lililotumiwa na wakimbizi na wapigania uhuru kutoka maeneo ya kusini mwa Afrika.

Katika kitabu chake cha A Long Road to Freedom, Nelson Mandela alikumbushia hisia za kimsisimko alizopata wakati akiwasili Mbeya mwaka 1962;

“…Kwa kweli nilishikwa na hisia kuwa niko katika nchi inayoongozwa na Waafrika. Kwa mara ya kwanza katika maisha yangu, nilikuwa mtu huru. Nilihisi mzigo wa ukandamizaji ukiondoshwa mabegaji mwangu. Kwa mara ya kwanza nilikuwa nikihukumiwa si kwa rangi ya ngozi yangu bali vipimo vya akili na tabia yangu”.

Mjini Dar es Salaam Mandela alikuwa mgeni wa TANU na Serikali, akifikia katika familia ya Asanterabi Zephania Nsilo Swai, Mhazina wa TANU na Waziri wa Biashara kipindi hicho.

Alipewa hati ya kusafiria ya Tanganyika, ambayo ilimwezesha kusafiri katika mataifa mengine ya Afrika kwa mafunzo ya kijeshi na uongozi.

Ikatokea, Mandela alisahau viatu vyake aina ya buti alivyokuja navyo kutoka Afrika Kusini katika familia ya Nsilo Swai wakati alipoondoka Dar es salaam kwenda kupata mafunzo ya uongozi na kijeshi ng’ambo.

Vicky Mawalla Nsilo Swai, mke wa marehemu Asanterabi Nsilo Swai alipata fursa ya kipekee ya kumkabidhi Rais Nelson Mandela pea hizo za viatu miaka 33 baadaye mjini Pretoria, Afrika Kusini.

Sam Nujoma wa SWAPO pia alipitia njia kama hizo akiingia Tanzania kupitia mkoani Mbeya na pia alipewa hati ya kusafiria ya Tanganyika.

Akiwa Mbeya alihifadhi baadhi ya wakimbizi huku wapigania uhuru wakienda kambi za mafunzo huko Chunya, kilomita 100 kaskazini magharibi.

Baadaye kambi zaidi za mafunzo mafunzo zilianzishwa katika maeneo ya Dakawa, Kongwa, Mgagao, Mazimbu na Nachingwea.

Ili kuhitimisha vyema kipande hiki kuhusu harakati za ukombozi wa Afrika ni vyema ninukuu Azimio la Mkutano wa Mataifa Huru Afrika CAIS/Plen./Rev./ambao ulianzisha Kamati ya Ukombozi ya OAU.

Mkutano wa kilele wa mataifa huru ya Afrika mjini Addis Ababa, Ethiopia, kuanzia Mei 22 hadi 25, 1963, ukiwa umezingatia masuala yote kuhusu kuuondoa ukoloni, kwa kauli moja uliona umuhimu mkubwa wa kuratibu na kuongeza juhudi za wapigania uhuru hao katika upatikanaji wa uhuru bila masharti katika maeneo yaliyokuwa yakikaliwa bado na wageni.

Azimio hilo pamoja na mambo mengine lilisema; Kwa kuzingatia kwamba ni wajibu wa mataifa yote huru ya Afrika kuunga mkono harakati za watu wa Afrika katika harakati zao za kudai uhuru;

Kwa kuangalia kwa masikitiko makubwa kwamba sehemu kubwa za meneo yaliyobakia yanayoendesha harakati hizo za kupigania uhuru wa Afrika yanatawaliwa na walowezi wa kigeni;

Kwa kuamini kuwa mataifa ya kikoloni hulazimisha uwekaji wa walowezi kudhibiti serikali na tawala za maeneo hayo, na hivyo kuanzisha maeneo ya kikoloni kati ardhi ya Africa;

Imekubaliwa kwa kauli moja kuziunga mkono na kuziratibu juhudi na harakati hizo eneo hilo, na kwa sababu hiyo imekubaliwa kuchukuliwa kwa hatua zifuatazo;

Kukaribisha makundi yote ya kitaifa ya ukombozi ili kuratibu juhudi zao kwa kuanzisha vuguvugu aina moja kwa kila eneo na ikibidi kuimarisha ufanisi wa harakati zao na matumizi mazuri ya misaada wanayopatiwa;

 Kuanzisha Kamati ya Uratibu yenye mataifa ya Algeria, Ethiopia, Guinea, Congo (Leopoldville), Nigeria, Senegal,  Tanganyika, Jamhuri ya Muungano wa Kiarabu na Uganda, makao makuu yakiwa Dar-es-Salaam, Tanganyika, ikihusika na jukumu la kuratibu msaada kutoka mataifa ya Afrika na kusimamia mfuko maalumu utakaoundwa kwa dhumuni hilo;

Uanzishaji wa mfuko maalumu utakaochangisha kwa hiari kutoka mataifa wanachama kwa mwaka uliopo, mwisho wa kuchangia ukiwa Julai 15, 1963; Kuiomba Kamati ya Uratibu kuwasilisha pendelezo la fedha miongoni mwa nchi wanachama na Baraza la Mawaziri ili kusambaza msaada wa kifedha na kiufundi kwa vuguvugu mbalimbali za ukombozi wa Afrika

Uanzishaji wa Kamati ya Ukombozi ya OAU, kuiwekea makao na kuisaidia kifedha, vifaa, kiufundi na maadili ulikuwa mchango mkubwa wa Nyerere na Tanzania kwa ukombozi wa Afrika.

Wakati Rais Nelson Mandela alipochukua kiti kinachomstahili kuiwakilisha Afrika Kusini katika mkutano wa kilele wa OAU nchini Tunisia mwaka 1994, tukio hilo liliashiria mwisho wa utawala wa kikoloni Afrika.

Majukumu ya Kamati ya Ukombozi ya OAU yakakoma na ilikuwa ‘Operesheni Imekamilika.’

Kamati ya Ukombozi ya OAU iliongozwa na makatibu watendaji watatu Watanzania: Sebastian Chale; mjomba wangu George Magombe; na Hashim Mbita.

Makatibu hao watendaji wanastahili sifa. Umoja na mshikamano wa Afrika utaendelea katika kizazi kijacho baada ya Nyerere kufuatia maono na msingi yeye na wenzake walioiweka.

Nyerere na Umoja wa Afrika

Ukombozi na umoja wa bara Aftika ulitawala katika fikra za Mwalimu na OAU kipindi chote cha urais wake na wakati wa uhai wa OAU.

Katika mkutano wa kwanza wa kilele wa mataifa huru ya Afrika, njia mbili za kuunganisha Afrika ziliwasilishwa mezani. Ya kwanza; ya kuanzisha mara moja muungano wa Afrika, likiwa wazo la Kwame Nkrumah wa Ghana.

Wazo la pili la kuunganisha Afrika hatua kwa hatua, lililoungwa mkono na Mwalimu Nyerere.

Mwishoni, wakuu wa nchi walichagua kubakia na mataifa yao na kuendeleza umoja hatua kwa hatua.

Itaendelea wiki ijayo

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,079FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles