23.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Waliovamia ardhi ya Dk. Balali watakiwa kuondoka

Na MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

WATU waliovamia eneo la ardhi linalomilikiwa na mjane wa aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dk Daud Balali eneo la Maputo Kata ya Mbweni  jijini Dar es Salaam wametakiwa kuondoka mara moja katika eneo hilo.

Kwa mujibu wa barua iliyosainiwa na H.C. Mtutwa kwa niaba ya Kamishna wa Ardhi yenye Kumbukumbu No. LD/345555/9 ya Desemba 5 mwaka huu kwenda Kampuni ya Udalali ya SUMA JKT ambao ndiyo wamepewa kazi ya kuwaondoa wavamizi hao iliainisha hati mbalimbali za viwanja vilivyopo kwenye eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 12.

Awali SUMA JKT waliomba serikali kupitia Wizara ya Ardhi iwafahamishe mmiliki halali wa eneo hilo kabla hawajaanza kazi ya kuwaondoa kwa nguvu wavamizi hao.

Akizungumzia mgogoro huo, kaka wa mke wa marehemu Dk Balali, Olamu Muganda aliliambia MTANZANIA jana kuwa wanazo hati zote za viwanja vilivyopo kwenye eneo hilo na wamekuwa wakilipa kodi zote kila mwaka serikalini.

Katika maelezo yake, Muganda aliutupia lawama uongozi wa Serikali ya Mtaa wa Maputo Kata ya Mbweni kwamba wanapotosha na kuchochea wavamizi ili wasiondoke kwa maslahi yao binafsi.

“Kimsingi wavamizi hao hawana document (nyaraka) yoyote inayoonesha walipataje eneo hilo zaidi ya kutumia mapanga na silaha za jadi kujihami, wamekuwa wakimtisha mjane wa Dk Balali kila alipotaka kuendeleza eneo lake.

“Tumekwisha toa taarifa kwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama naamini analifanyia kazi”alisisitiza Muganda.

Diwani wa Kata ya Mbweni, Hashim Mbonde alisema anasikitishwa na kuwapo kwa wavamizi katika ardhi halali iliyonunuliwa na marehemu Dk Balali ambayo sasa inamilikiwa na mkewe, Anna Balali.

Mbonde alisema Dk Balali alinunua kihalali eneo hilo kutoka kwa Kitwana Halfan ambaye pia ni marehemu huku yeye (diwani) akiwa ni mmoja wa mashahidi.

Alisema baadaye Dk Balali alipima eneo hilo lakini cha kushangaza siku moja baada ya kifo chake watu zaidi ya 100 walivamia kwenye eneo hilo na kuanza kujimilikisha isivyo halali.

“Sheria zipo wazi za ugawaji viwanja na hata ununuzi hivyo naiomba Serikali kuwachukulia hatua watu wenye tabia ya kuvamia maeneo ya watu na kutengeneza migogoro isiyokuwa ya lazima hususani ukanda huu wa Dar es Salaam na Pwani kwa kusaidiwa na viongozi wa mitaa na vijiji wasiokuwa waaminifu.

Mwenyekiti wa Mtaa huo,Costantino Malifa juzi alikiri kwamba eneo hilo aliuziwa Dk Balali kwa ajili ya kujenga hoteli ya kitalii.

Hata hivyo katika mazungumzo na waandishi wa habari baadhi ya wakazi hao walikiri kuvamia, eneo hilo huku wakiomba huruma kwa Rais Dk. John Magufuli kuingilia kati na kuwamilikisha eneo hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles