26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Waliougua Dengue wafikia 1,200

WAANDISHI WETUDODOMA/DAR

WATU 1,237 wamethibitishwa kuwa na virusi vya ugonjwa wa dengue, ambao kati ya hao 1,150 wanatoka katika Jiji la Dar es Salaam, 86 Tanga huku mmoja akitoka Singida.

  Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Muhammad Kambi alisema jana kuwa  takwimu hizo ni kwa kipindi cha Januari hadi Mei.

 Alisema kwa Januari kulikuwa na wagonjwa 56, Februari wagonjwa 82, wakati Machi ilifikia wagongwa 159 na Aprili wagonjwa 940.

 Alisema mpaka sasa vifo vya watu wawili vimeshatokea lakini watu hao pia walikuwa na maradhi mengine.

 “Naomba wananchi mjitahidi kuchukua tahadhari za ugonjwa huu kwa sababu ni mbaya sana,” alisema Profesa Kambi.

 Alizungumzia jinsi ya kujikinga na ugonjwa huo kuwa ni watu kufikia madimbwi ya maji yaliyotuama, kunyunyuzia dawa ya kuua viluwiluwi vya mbu, kuondoa vitu vinavyoweza kuweka mazalia ya mbu, kufyeka vichaka vilivyo karibu na makazi ya watu.

 “Mbinu nyingine ya kuzuia mbu hao ni kuhakikisha maua yanayopandwa kwenye makopo hayaruhusu maji kutuama, kufunika mashimo ya maji taka kwa mfuniko imara na kusafisha kuta za paa la nyumba   kutoruhusu maji kutuama,” alisema.

 Alisema pia jamii inapaswa kuvaa nguo ndefu   kujikinga kuumwa na mbu, kutumia vyandarua vyenye viuatilifu, kutumia dawa za kufukuza mbu na kuweka nyavu kwenye madirisha na milango ya nyumba za kuishi.

 Alizitaja dalili za ugonjwa huo kuwa ni pamoja na homa ya ghafla, kuumwa kichwa hususani sehemu za macho na maumivu ya viungo kwa ujumla.

 “Dalili hizi huanza kujitokeza kuanzia siku tatu hadi 14 mtu anapoambukizwa ugonjwa huo na zinaweza kufanana na za malaria.

“Dalili nyingine ni mtu kutoka na damu sehemu za fizi, midomoni, puani, kwenye macho na kwenye njia ya haja kubwa na ndogo,” alisema.

 ILALA

Mganga Mkuu wa Manispaa ya Ilala, Dk. Emily Lihawa, alisema watu 548 wameugua dengue kuanzia Januari hadi sasa.

Alisema vifo vilivyotokea ni viwili katika Hospitali ya Regency na Aghakan.

Alisema kwa Ilala vipimo vya ugonjwa huo vinapatikana katika hospitali kadhaa za binafsi na ya Serikali ya Mnazi Mmoja kwa gharama ya Sh 15,000.

Dk. Lihawa alisema zimetengwa Sh milioni 52 kwa ajili ya kununua dawa za kuulia viluwiluwi vya mbu na tayari wameanza kupulizia maeneo yote yenye mazalia.

“Tatizo bado lipo na tunaendelea kupambana lakini cha msingi ni watu kuzingatia usafi wa mazingira,” alisema Dk. Lihawa.

Daktari ashauri namna ya kujikinga na Dengue

Katika hatua nyingine, Dakitari Bingwa wa Magonjwa yanayoambukiza kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dk. Joan Rugemalila, ameishauri jamii kujikinga na mbu hasa   kazini   kuepuka ugonjwa wa dengue.

Akizungumza na MTANZANIA   Dar es Salaam jana, Dk. Joan alisema mbu wanaoeneza   dengue hung’ata hata mchana hivyo jamii ichukue tahadhari.

Alisema ni vema kulala ndani ya chandarua hata kama ni mchana na kutumia dawa za kuzuia kuumwa na mbu.

“Ugonjwa huu upo na jamii inatakiwa kuchukua tahadhari kwa kuhakikisha wanajikinga na mbu kwa kulala ndani ya vyandarua na kupaka dawa za kuzuia mbu hata kama ni mchana,” alisema Dk. Joan.

Alisema ni muhimu kutunza mazingira kwa kuua mazalia ya mbu katika maeneo ya kuishi.

Aliwashauri wagonjwa wanaopata ugonjwa huo kuhakikisha wanakunywa maji mengi   na kupata muda wa kutosha wa kupumzika.

“Mtu akipatwa na ugonjwa dengue asitumie dawa za maumivu za ‘diclofenac’, aspirini na brufen kwa kuwa husababisha kuvuja damu,”  alisema Dk. Joan.

Akizungumzia dalili za ugonjwa huo, Dk.  Joan alisema tangu kuumwa na mbu hadi kuanza kuonekana dalili huchukua siku tatu hadi 14.

Alisema mgonjwa mwenye dengue hupata homa na maumivu ya kichwa.

Aliongeza kuwa dalili nyingine ni kuchoka kwa misuli ya mwili, maungio ya viungo, ngozi kupata vipele na kutapika.

“Kwa hapa nchini asilimia ndogo hupata maambukizi yanayosababisha kuvuja damu (hemorrhagic fever) ambao hupungukiwa maji na mshituko,” alisema Dk. Joan

Wakati huo huo, baadhi ya wazazi nchini wameomba elimu ya ugonjwa wa dengue itolewe kuanzia ngazi ya familia ili kujikinga na ugonjwa huo.

Wakizungumza na MTANZANIA kwa nyakati  tofauti, baadhi ya wazazi hao walisema  ugonjwa huo homa yake ni kali hivyo ni vema tahadhari ikachukuliwa mapema hasa kwa wanafunzi   shuleni.

  Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mwembe Madafu (CCM), Deus Nchimbi, alisema katika eneo lake wamekuwa wakijitahidi kutokomeza madampo ambayo mengi yamekuwa mazalia ya wadudu mbalimbali.

Alisema hali hiyo imekuwa ikisaidia kuwaepusha na magonjwa ya kuambukiza hasa wanafunzi wa shule zilizopo ndani ya kata hiyo, ikiwamo Shule ya Msingi Mzambarauni pamoja na kutunza mazingira.

“Naomba jamii ishiriki pamoja nasi katika shughuli mbalimbali za kufanya usafi  kupiga vita uchafu,” alisema Nchimbi.

*Habari imeandaliwa na Na Sarah Moses (Dodoma), Nora Damian na Tunu Nassor (Dar es Salaam).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles