29.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 28, 2021

Waliotibiwa moyo nje ya nchi wakimbilia JKCI

 MWANDISHI WETU –DAR ES SALAAM

WAGONJWA saba waliowahi kwenda kufanyiwa upasuaji wa moyo nje ya nchi ambao hawajaweza kurudi huko kuhudhuria kliniki zao, ‘wamekimbilia’ katika banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), lililopo kwenye maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba).

Katika banda la JKCI wameweza kuonwa na wataalamu wabobezi wa magonjwa ya moyo na kisha kupatiwa utaratibu wa namna watakavyoweza kuanza kuhudhuria kliniki katika taasisi hiyo iliyopo Upanga, Jijini Dar es Salaam.

Sambamba na hilo, wananchi waliotembelea banda la JKCI lililopo katika ukumbi wa Karume wameweza kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo kwa kufanyiwa vipimo vya kisasa vya Electoral Cardiograph (ECG) na Echo Cardiograph (ECHO).

Kwa upande wake Fundi Sanifu wa Moyo (Cardiovasicular technologist), Abubakar Dalidali alisema mwitiko wa wananchi umekuwa mkubwa hivyo kuonesha kuwa wananchi wengi wanauhitaji wa kuchunguza afya zao mara kwa mara.

“Wananchi saba waliowahi kufanyiwa upasuaji nje ya nchi, hawajaweza kurudi walikofanyiwa upasuaji kuhudhuria kliniki, hivyo kufika katika banda la JKCI na kuchunguzwa tena mioyo yao inavyoendelea na kuweza kujua namna gani wataweza kuanza kuhudhuria kliniki kwenye taasisi yetu, tumewaelekeza,” alisema Dalidali.

Alisema kuwa kwenye banda la JKCI kuna vipimo mbalimbali vya uchunguzi wa afya ya moyo, kikiwemo kipimo cha Electoral Cardiograph (ECG) kinachochunguza mpitisho wa umeme unaopita kwenye moyo pamoja na kipimo cha Echo Cardiograph kinachochunguza utendaji mzima wa moyo.

“Kutegemeana na utaratibu wake ulivyopangwa mapigo ya moyo huwa kati ya wastani wa mapigo 60 hadi 100 kwa mtu mzima, hivyo ECG ni kipimo cha kwanza ambacho kinaweza kuonesha kama mapigo ya moyo yamezidi zaidi ya 100 na kuonesha kuwa kuna tatizo ama yamepungua chini ya 60 na kuwa tatizo pia.

“Tuliowafanyia uchunguzi wamegawanyika katika makundi mawili, wapo ambao majibu yao yameonekana hawana shida na wapo ambao yameonesha wanahitaji taratibu zaidi za kimatibabu, tumewapa rufaa kufika JKCI kwa ajili ya matibabu zaidi,” alisema Dalidali.

Mkazi wa Mbagala Jijini Dar es Salaam Fatuma Ally amesema kuwa katika maisha yake hakuwahi kuwaza kuwa ipo siku atachunguza moyo wake kama uko salama lakini baada ya kusikia kuwa wataalamu wa afya kutoka JKCI wapo katika maonesho ya Sabasaba akatumia fursa hiyo kutembelea banda hilo na kufanya vipimo vya kuchunguza moyo wake.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
158,609FollowersFollow
519,000SubscribersSubscribe

Latest Articles