23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Waliotafuna fedha ushirika wakabidhiwa Takukuru

RAMADHAN HASSAN-DODOMA

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imekabidhiwa orodha ya majina ya vyama vya ushirika ambavyo vinadaiwa kutafuna mabilioni ya fedha, huku Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo akiwataka wahusika kuanza kuzirejesha kuanzia jana na wakishindwa mali zao zitataifishwa.

Akizungumza jana Dodoma wakati akitoa taarifa ya ukaguzi wa vyama vya ushirika uliofanywa na Shirika la Ukaguzi wa Vyama vya Ushirika (Coasco), Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, alisema taarifa hiyo  imeonyesha kuna ubadhirifu mkubwa wa fedha katika vyama hivyo.

 “Namkabidhi taarifa Kamishna ili akashughulike nao, sisi tunachotaka ni hela zirudi,” alisema Hasunga.

Alisema kuwa katika mwaka wa fedha wa 2018/19 Serikali ilitoa maagizo kwa Coasco kukagua vyama vyote vya ushirika na hadi kufikia Juni 30, mwaka huu vyama 11,410 vilivyosajiliwa vilikaguliwa ambapo vyama sinzia ni 2,844 na vyama ambavyo havipatikani 2,103.

“Kutokana na maagizo hayo, hadi kufikia  Juni 30, 2019 Coasco ilikagua vyama vya ushirika vipatavyo 4,413 sawa na asilimia 102.63 ya lengo la Serikali la kukagua vyama 4,300.

“Katika vyama hivyo 4,413 vilivyokaguliwa, vyama 303 sawa na asilimia 6.87 vilipata hati inayoridhisha, vyama 2,378 asilimia 53.89 vilipata hati yenye shaka, vyama 879 sawa na asilimia 19.92 vilipata hati isiyoridhisha na vyama 853 asilimia 19.32 vilipata hati mbaya,” alisema Hasunga.

Alisema vyama vikuu vilivyokaguliwa vilikuwa 38, ambapo kati ya hivyo vyama vya mazao ni 2,710, vyama vya akiba na mikopo 1,448, vyama vingine 217 hivyo kuwa jumla ya vyama 4,413.

Hasunga alisema kati ya vyama vikuu 38, vyama vinne vilipata hati safi, vyama 22 vilipata hati yenye shaka, tisa vilipata hati isiyoridhisha na vitatu hati mbaya.

Vyama hivyo vikuu vitatu vilivyopata hati inayohusisha hoja zenye viashiria vya ubadhirifu wenye jumla zaidi ya Sh milioni 856.

Hasunga alisema Chama Kilele (Shirikisho-TFC) kimepata hati isiyoridhisha ambayo inajumuisha fedha benki zisizofanyiwa malinganisho na pia kutoonyeshwa katika taarifa za fedha kiasi cha Sh bilioni 1.5.

Alisema kati ya Saccos 1,448, Saccos 261 zilipata hati safi, 887 yenye shaka, 218 isiyoridhisha na 82 hati mbaya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles