33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Waliopata chanjo ya corona nchini wanasemaje?

Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital

Chanjo ya corona aina ya Johnson and Johns (J&J) imeanza kutolewa nchini, ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amekuwa mtu wa kwanza kuchanja chanjo hiyo (Julai 28, 2021).

J&J imekuja ikiwa ni baada ya kuwapo kwa mlolongo mrefu wa panda shuka juu ya uamuzi wa kutumia chanjo hapa nchini.

Awali, Tanzania haikuwa imeonesha msimamo wake juu ya utayari wa kutumia chanjo ya Corona lakini sasa hilo limepita na imeanza kutolewa.

Mtanzania Digital imepata nafasi ya kusikia shuhuda za waliopata fursa ya kuchanjwa na wengi wamepongeza ujio wa chanjo hiyo na kusema ‘kinga ni bora kuliko tiba’.

Wakati wa uzinduzi wa chanjo hiyo, Rais Samia alianza kwa kutoa nasaha kwa Watanzania ambao wanaelezwa kuleta mzaha.

“Wale wote ambao kwa hiyari yao wako tayari kuchanja tutahakikisha chanjo zinapatikana. Kwenye mwili wangu nadhani nina chanjo kama sita hivi ya leo itakuwa ya saba.

“Niseme ndugu zangu, mimi ni mama wa watoto wanne wanaonitegemea, ni bibi wa wajukuu kadhaa wanaonipenda sana na mimi nawapenda sana. Mbali ya yote, ni mke na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amir Jeshi Mkuu wa majeshi ya nchi hii.

“Nisingejitoa mwenyewe, nikajipeleka kwenye kifo, nikajipeleka kwenye hatari nikijua kwamba nina majukumu yananitegemea.

“Kwa wale ambao koo zao hazijaguswa, hawajapata madhara ya maradhi haya, wanaweza kusema wanavyotaka, lakini nenda leo Moshi, nenda Arusha, nenda Kagera hata Dar es Salaam uonane na zile koo ambazo zimeguswa…,” alisema Rais Samia.

Viongozi wa Vyama Vya Siasa

Profesa Ibrahim Lipumba ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), ni miongoni mwa Watanzania waliobahatika kupata chanjo ya Corona.

“Nimekuja hapa. Wala haichukui muda ni kama dakika 15 hivi. Unadungwa kisindano kidogo wala hakiumi na najisikia imara kwani baada ya kupata chanjo unashauriwa kupumzika kwa takribani dakika 15.

“Na iwapo kutakuwa na tatizo lolote basi uweze kumjulisha daktari, lakini kwa ujumla hakutegemei kuwa na tatizo lolote.

“Hivyo, natoa wito kwa Serikali kuweza kuweka mpango mzuri wa Watanzania wote ambao wako tayari ili waweze kupewa chanjo hii.

“Pia, Serikali iendelee kutoa elimu kuhusu hizi chanjo kwa sababu watu wengi wana wasiwasi kuhusu hizi chanjo. Zimefanyiwa utafiti na ziko salama, watu wengi wameshapata hizi chanjo kwa sababu kwa maradhi haya,” amesema Prof. Lipumba.

Kwa upande wake, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapunduzi (CCM), Shaka Hamdu Shaka, amesema Chama kiliahidi kuwakinga Watanzania na maradhi, hususan ya mlipuko kama ilivyo Corona.

Viongozi wa Dini

Mufti wa Tanzania, Shiekh Aboubakar Zubeir, amesema: “Kutakuwa hapana budi kuchanja kwa wakati ujao. Mfano kwa Waislam sasa hivi tunalazimika kuchanja sababu hakuna njia ya kwenda Hija kama hujachanja. Na juzi wamefungua Umra kule Saudi Arabia,” amesema Muft Zubeir.

Naye Askofu Mkuu wa Kanisa la KKKT, Dk. Fredrick Shoo, amesema zinatakiwa zipatikane chanjo za kutosha ili kila Mtanzania aweze kupata.

“Kubwa ni kuondoa hofu na tusikubali mambo ya upotoshaji kwamba chanjo hizo siyo salama,” amesema Dk. Shoo.

Wanamichezo

Aidha, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Wallance Karia, amesema wanamichezo ni watu wanaokuwa kwenye mikusanyiko na mara kwa mara wanasafiri, hivyo chanjo hiyo ni muhimu.

“Hivi ninavyozungumza vijana wetu na timu yetu ya Taifa chini ya miaka 23 wako nchini Ethiopia, hivyo tunasafiri na kuna nchi tayari zina taratibu hizo.

“Lakini pia, kutukinga sisi na maradhi haya ni la muhimu sana wanamichezo kuhakikisha kuwa tunapata chanjo hiyo, unapopata fursa uitumie,” amesema Karia.

Wananchi wanasemaje?

Nao wananchi wa kawaida, akiwamo John Shemoka, mkazi wa Dar es Salaam, amesema ni wakati wa Watanzania kuondokana na dhana kwamba Wazungu wanataka kuua watu weusi na badala yake wajitokeze kuchanja chanjo.

“Watu tusijisahau na kukubali kudanganywa kwamba Wazungu wanataka kutuua. Hapana, jambo la msingi tujitokeze kuchanjwa chanjo ili maisha yaendelee. “Kwani kama wangekuwa na nia ya kutuua basi wangekuwa wameshatuua muda mrefu kupitia kwenye misaada mbalimbali ambayo wanatuletea,” amesema Shemoka.

Akichangia mjadala huu, Gertrude Urassa, mkazi wa Sinza jijini Dar es Salaam, amesema hakuna haja ya kuingiza siasa katika suala hilo la chanjo.

“Tujitokeze tu kupata chanjo kwani ugonjwa upo na unaua ila kama mtu hataki basi asubiri mtu mwingine wa kuja kumfungua macho. Ni chanjo hiyo hiyo tunayosikia wenzetu wamechanjwa lakini sisi bado tuna mashaka, hivyo tuepuke huu uzushi wa mitandaoni,” amesema Gertrude.

WAPO WALIOKO NJIAPANDA NA CHANJO HIYO

Johari Joseph mkazi wa Dar es Salaam amesema yeye binafsi anapinga mpango huu kwa kile alichosema kwamba chanjo hiyo ndio ambayo aliwahi kusikia ikikataliwa kwenye mataifa kama Marekani kutokana na kwamba inasababisha madhara alafu ndio hiyohiyo ambayo tumeletewa kutoka huko Marekani.

“Alafu tumeletewa sisi hapana, wanatuthibitishia kwamba iko salama na tunaambiwa tuchanje hapana, mimi binafsi siko tayari kuchanja hiyo chanjo ndugu yangu, kwanza Serikali imesema kuchanja ni hiari ya mtu.

“Lakini pia sina magonjwa ambayo ni hatarishi, pia kinga yangu ni imara hapa nina takribani miaka saba sijawahi kuumwa zaidi ya kichwa tu ambacho huwa namuona Daktari ananipa dawa napona.

“Kwa kipindi hiki tunatumia sana tiba za asili kama tulivyoshauriwa na wataalamu ikiwamo limao na mengine kama hayo,” amesema Johari.

Upande wake, Laizer Baraka, anasema kuwa chanjo hiyo bado ni mtego kwa watanzania waliowengi kwani kama rais wan chi amekuwa mtu wa kwanza kucho0ma basi maana naye anataka Watanzania wamfuate licha licha ya ukweli kuwa sehemu nyingine ilishakataliwa.

“Kosa lingekuwa kama ametulazimisha ila kwa kuwa yeye amechanja basi acha ibaki hivyo, lakini hatujui kuna nini kwenye hii chanjo, kwani kumbuka hii ilishakataliwa sehemu nyingi.

“Hatuwezi tukasema moja kwa moja kwamba hawa wnaaotuletea hii chanjo wana nia gani na sisi. Kama wao walivyosema kwamba ni hiari lakini Rais wa nchi akakubali kuchanja hadharani sasa huwezi jua baadae hizo Ofisi zilizo chini yake zitakuwa na utaratibu gani.

“Mfano utakuja utaumwa hapa utaenda kwa Daktari utaambiwa kama hujachanjwa Mgonjwa wako hapokelewi, kama kuna dhamira mbaya tayari, hata usema kwamba hutachanjwa bado hili linaenda kuwa lazima kwani itafika sehemu huduma itakuwa changamoto, ila kwangu binafsi siwezi kuchanja,” amesema Baraka.

USHAURI WA MTAALAMU

Katika hatua nyingine, mtaalamu wa afya, Dk. Elisha Osati, amezungumzia ujio wa chanjo hiyo akisema hatua ya rais kuchanja ni ishara ya chanjo hiyo kutokuwa na makandokando.

“Mpaka mkuu wa nchi ametoa kofia zake mbalimbali na kukubali kuchanja, basi hakuna haja ya Watanzania kuendelea kuwa na wasiwasi. Wajitokeze kupata chanjo.

“Kwani malengo ya chanjo ni kuzuia ugonjwa usiwe mkali zaidi hata kama mtu atapata hapo baadaye. Hata Uingereza na Marekani, wengi wa wagonjwa waliongezeka ni wale ambao hawajachanjwa au hawajamaliza chanjo zao,” amesema Dk. Osati.

Mwisho

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles