Manchester, England
SHABIKI yeyote aliyehusika katika tukio la kuishambulia nyumba ya Makamu Mwenyekiti wa Manchester United, Ed Woodward, atakiona cha moto.
Hiyo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na uongozi wa klabu hiyo juu ya tukio lililotokea juzi.
Kwa mujibu wa gazeti la Mirror juu ya kile kilichojiri, mashabiki wanaokadiriwa kufikia 30 walirusha moto kwenye nyumba ya bosi huyo.
Hatua yao hiyo iliyoonekana kuwa ni utovu wa nidhamu, ilikuja muda mfupi kabla ya Mashetani Wekundu kuwavaa mahasimu wao wa jijini Manchester, Manchester City.
Huo ulikuwa ni mtanange wa marudiano wa hatua ya nusu fainali ya Kombe la Ligi (Carabao Cup) baada ya Mashetani Wekundu kuchapwa mabao 3-1 katika ule wa kwanza uliochezwa mwanzoni mwa mwezi huu pale Old Trafford.
Katika taarifa ya Man United kulaani kitendo cha Ed Woodward kufanyiwa uhuni huo, uongozi wa Man United umesema shabiki atakayebainika kuhusika atachukuliwa hatua kali, ikiwamo kufungiwa maisha kuingia uwanjani.
“Klabu ya Manchester United imeweka wazi juu ya kilichotokea nje ya nyumba ya mmoja kati ya waajiriwa wetu.
“Tunafahamu kuwa ulimwengu wa soka utakuwa nyuma yetu kipindi hiki tunaposhirikiana na Polisi wa Manchester kuchunguza wahusika wa uhuni huo,” ilieleza taarifa hiyo.
Aidha, sehemu ya taarifa hiyo iliongeza kuwa Man United haimzuii shabiki kutoa maoni lakini kilichofanyika ni zaidi ya hapo.
“Mashabiki kutoa maoni yao ni jambo moja, uhalifu na nia ya kuhatarisha maisha ya mtu na mali ni jambo jingine. Hakuna kufumbia macho katika hili,” iliongeza.
Ni kwa muda mrefu sasa, kumekuwapo na uhusiano mbovu kati ya mashabiki wa Mashetani Wekundu na bosi wao huyo, Woodward, ambaye hakuwa nyumbani walipokwenda kufanya vurugu hizo.
Haijasahaulika kwamba kelele za kumbeza zilisikika wikiendi iliyopita, wakati kikosi hicho kikiibuka na ushindi wa mabao 6-0 dhidi ya Tranmere Rovers katika mchezo wa Kombe la FA.
Huku ‘chama’ lao likishika nafasi ya tano katika msimamo wa Ligi Kuu ya England, wengi wamekuwa wakimuona Woodward kuwa tatizo, hasa linapokuja suala la kusajili.
Kile kinachothibitisha mwenendo mbovu wa Man United iliyo chini ya kocha Ole Gunnar Solskjaer, timu hiyo ilikuwa imeshinda mechi tatu pekee kati ya nane zilizopita kabla ya kuivaa Man City usiku wa kuamkia leo.