Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
WALIOKUWA wafanyakazi wa kampuni ya Tancoard ambayo kwa sasa inaitwa Sisalana Cordage Factory wameiomba Serikali kuingilia kati suala la notisi ya kuhama ili wasihamishwe kwenye nyumba za kampuni hadi watakapolipwa stahiki zao.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Mei 11, na waandishi wa habari kwa niaba ya wafanyakazi wenzake Moses Shekalaghe amesema walio kuwa wafanyakazi wa kampuni hiyo wanaishi kambi ya mikoroshini, kata ya Ngomeni Wilaya ya Muheza mkoani Tanga hawajalipwa mishahara na malimbikizo yao tangu mwaka 2018.
“Kampuni hiyo ilikuwa na zaidi ya wafanyakazi 120 ambao wanadai haki zao za kazini ikiwemo mishahara na malimbikizo mengine, na kuna wafanyakazi 100 wamesimashiwa kazi mpaka sasa bila malipo,”amesema Shekalaghe.
Amesema Januari 26, mwaka huu walipewa notisi ya kuhama katika nyumba za kampuni kinyume cha sheria pamoja na makubaliano waliyoingia wakati wanaanza kazi katika kampuni hizo.
Aidha Shekalaghe amesema wanaiomba kampuni hiyo ifuate haki na taratibu na sheria ilivyoanishwa katika katiba ya nchi sheria ya ajira na mahusiano kazini, pamoja na mikataba ya kimataifa ya haki za Wafanyakazi.
Mtanzania Digital ilimtafuta kwa njia ya simu Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Sisalana Cordage Factory, Elizabeth Kalambo ambapo amesema kampuni hizo mbili ni tofauti na Sisalana haihusiki inayohusika ni Katani Limited na Tancoard.
Amesema ni kweli walipewa notisi na walitoa tangazo waachie nyumba hizo na sasa wamepewa notisi ya pili kisheria hawatakiwi kuwepo pale ni ubinadamu tuu.
“Kesi yao ipo Mahakamani na hairuhusiwi kuzungumzia kisheria vitu vikifika mahakamani tunachia Mahakama,” amesema Kalambo.