RAMADHAN HASSAN-DODOMA
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amesema watu waliojenga kwenye maeneo hatarishi ikiwamo mabondeni na kwenye hifadhi za barabara, wataendelea kutozwa kodi mbalimbali ikiwamo za majengo ingawa makazi yao hayatarasimishwa.
Lukuvi alisema hayo jana bungeni jijini hapa alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Zainab Amiri (CUF).
Katika swali lake, mbunge huyo alisema kuna baadhi ya watu wanajenga mabondeni, wengine jirani na hifadhi ya barabara na reli, lakini Serikali hukusanya kodi za maeneo na majengo katika maeneo hayo.
“Je, Serikali inaeleza nini kuhusu kadhia hii?Ili mwananchi ajenge mahali husika lazima apate kibali. Je, nini adhabu ambayo wanapewa wanaotoa vibali kwenye maeneo hatarishi?” alihoji.
Akijibu swali hilo, Lukuvi alisema utoaji wa leseni za makazi hautafanyika kwa watu waliojenga maeneo hatarishi.
“Ni kweli kuna watu wanajenga kwenye hifadhi za barabara na hifadhi za miundombinu mingine na mabondeni, wamefanya hivyo kinyume na sheria,” alisema.
Aidha alisema wapo ambao wamejenga kwenye maeneo hayo, hivyo sheria itachukua mkondo wake.
“Ni kweli kodi inakusanywa kwa sababu bado wanatumia rasilimali zilizopo, lazima wachangie, lakini ujenzi katika maeneo hayo hairuhusiwi,” alisema.
Alisema kodi za majengo zitatozwa na kodi wanazotozwa raia wengine zitatozwa, lakini haitahalalisha wao kuwa wamekaa kwenye maeneo hayo kihalali.
“Lolote likitokea linaweza kama wapangaji na halmashauri husika wakiamua kuchukua hatua. Vibali vya ujenzi vinatolewa na timu ya wataalamu ya ujenzi na havichukui zaidi ya siku tatu na vinatolewa kwa kasi,” alisema.
Katika swali la msingi, mbunge huyo alihoji mkakati wa Serikali wa kuwapatia wananchi wa Tanzania elimu stahiki ili waepukane na ujenzi ambao hauzingatii mipango miji.
Akijibu swali hilo, Lukuvi alisema Serikali imekuwa ikitekeleza mikakati mbalimbali ya kuwaelimisha wananchi kuhusu ujenzi unaozingatia mipango miji ili kuepuka madhara mbalimbali ikiwemo kubomolewa nyumba zao bila kulipwa fidia.
Alitaja mikakati hiyo kuwa ni pamoja na kutoa elimu kwa njia ya vyombo vya habari kama vile redio, runinga, magazeti, vipeperushi, machapisho mbalimbali, mitandao ya kijamii pamoja na tovuti ya wizara.
“Serikali inaendelea kusisitiza kuwa wananchi wazingatie sheria na taratibu za uendelezaji miji ili kujiepusha na ujenzi holela,” alisisitiza.
Aidha aliwataka wananchi waepuke kujenga mijini bila kuwa na vibali vya ujenzi ili kuepuka kubomolewa nyumba zao bila kulipwa fidia.