30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Waliofukiwa ardhini siku 41 waanza kuona

Na Paul Kayanda, Kahama

HALI za wachimbaji wadogo waliookolewa baada ya kufukiwa na kifusi cha udongo kwa siku 41 katika machimbo ya Nyangarata, Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, zinaanza kuimarika huku baadhi yao wakianza kuona.

Kwa mujibu wa taarifa za kitabibu zilizotolewa na Hospitali ya Wilaya ya Kahama, wachimbaji hao wameanza kuona ingawa kwa uoni hafifu, lakini kadiri ya siku zinavyokwenda afya zao zitaanza kuimarika.

Akizungumza jana na MTANZANIA, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Kahama, Dk. Joseph Ngowi, alisema licha ya hali zao kuendelea vema, wachimbaji hao bado wako chini ya uangalizi maalumu wa madaktari.

“Kwa sasa wachimbaji hawa wanaanza kuonyesha kurejea katika afya zao kwa taratibu, lakini pia wameanza kuona kwa mbali (uoni hafifu), ila katika kipindi cha siku saba wanaweza kurejea katika hali yao ya kawaida.

“Maendeleo yao ni mazuri, bado tunaendelea nao na matibabu chini ya kitengo chetu cha lishe, wanaanza kurejewa na fahamu tofauti na walivyofikishwa hapa hospitali.

“Na hili la kushindwa kuona haraka linatokana na kukaa siku nyingi chini ya ardhi ambako kulikuwa na giza nene, na walipofikishwa hapa walikuwa hawaoni kabisa,” alisema Dk. Ngowi.

Wachimbaji hao waliotolewa kwenye mashimo ya mgodi huo Novemba 15, mwaka huu tangu walipofukiwa Oktoba 5, mwaka huu ni Chacha Wambura, Amos Muhangwa, Joseph Burulwa, Msafiri Gerald na Wonyiwa Moris, huku Mussa Spana, alifariki dunia siku chache baada ya kufukiwa na kifusi kwa kukosa chakula.

Mmoja wa wachimbaji hao, Wambura, juzi wakati akihojiwa na waandishi wa habari, alisema awali walifukiwa sita, lakini bahati mbaya mwenzao Spana alifariki dunia siku chache baadaye baada ya kukataa kula mizizi na wadudu.

Alisema hatua hiyo ilisababisha akumbwe na ugonjwa wa kuhara uliosababisha kifo chake.

“Tulikuwa tukitumia miti inayojengea kingo za mashimo kama chakula pamoja na wadudu wadogo wadogo ndani ya  mashimo hayo, hasa mende.

“Pia tulikuwa tukitumia kofia zetu ngumu (helmet) kukinga maji yaliyokuwa yakitiririka kutoka juu ya ardhi ingawa yalikuwa ni machafu. Mwenzetu Mussa alifariki dunia baada ya kukataa kutumia vitu hivyo,” alisema Wambura.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles