25.5 C
Dar es Salaam
Monday, November 29, 2021

Walinzi walioiba mabilioni NBC wapandishwa kortini

Christina Gauluhanga – Dar es Salaam

WATU saba wakiwamo wafanyakazi watatu wa Kampuni ya Ulinzi ya G4s Secure Solution Tanzania Limited na wafanyabiashara wanne, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, wakikabiliwa na mashtaka manne likiwamo la utakatishaji fedha wa Sh bilioni 2.2.

Washtakiwa hao ni walinzi Christopher Rugemalila (34) mkazi wa Chanika, Ramadhani Athumani (40) mkazi wa Kijichi Njia ya Ng’ombe na Ibrahim Maunga (49) ambaye ni mfanyabiashara mkazi wa Kiluvya.

Wengine ni Salim Mtandika (45) mlinzi, mkazi wa Mbagala Kizuiani, Dismas Mgongolwa (45), mkazi wa Kibamba, Godfrey Saimon (33), mkazi wa Manzese na Ladslaus Macha (44), mkazi wa Ukonga Kipunguni.

Washtakiwa hao wamefikishwa mahakamani hapo na kusomewa mashtaka yao na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mkunde Mshanga mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Augustina Mbando.

Akisoma hati ya mashtaka, Wakili Mshanga alidai katika shtaka la kwanza washtakiwa wote wanadaiwa kuwa kati ya Februari Mosi na 7, mwaka huu ndani ya Jiji la Dar es Salaam kwa pamoja waliungana na kuunda genge la uhalifu kisha kuiba Sh bilioni 2.2.

Mshanga alidai katika shtaka la pili, kati ya Februari Mosi na 7, mwaka huu eneo la Chang’ombe lililopo Temeke jijini Dar es Salaam, washtakiwa hao kwa pamoja waliweza kuiba kiasi cha Sh bilioni 1.2, Dola za Marekani 402,000 sawa na Sh milioni 924.6 pamoja na Euro 22,700 sawa na zaidi ya Sh milioni 59 ambapo jumla ya fedha zote ni Sh bilioni 2.2 mali ya Kampuni ya G4s Secure Solution Tanzania Limited.

Shtaka la tatu linalowakabili Christopher, Ramadhan na Ibrahim, inadaiwa kuwa Februari 7, mwaka huu, maeneo ya Chang’ombe Temeke jijini Dar es Salaam washtakiwa hao kwa pamoja wakiwa wafanyakazi wa Kampuni ya G4s Secure Solution Tanzania Limited, walifanikiwa kuiba fedha za Tanzania kiasi cha Sh bilioni 1.2 na dola za Marekani 402,000 mali ya mwajiri wao.

Katika shtaka la mwisho, Mshanga alidai kati ya Februari 7 na 23, mwaka huu, washtakiwa wote kwa pamoja walijipatia kiasi cha Sh bilioni 2.2 kutoka Kampuni ya G4s Secure Solution Tanzania Limited huku wakijua fedha hizo zinatokana na mazalia ya uhalifu na kosa la wizi.

Baada ya kuwasomea mashitaka hayo, washtakiwa hao hawakuruhusiwa kujibu chochote, ambapo upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Washtakiwa hao wamepelekwa rumande kwa sababu kesi hiyo haina dhamana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu  haina uwezo wa kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.

Awali ilidaiwa kuwa Februari, 25 mwaka huu, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam lilitangaza kuwashikilia watu wanne, wakiwamo  wafanyakazi hao wa Kampuni ya G4s kwa tuhuma za wizi wa fedha walizokuwa wakizipeleka makao makuu ya Benki ya NBC kutoka katika matawi ya benki hiyo.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,301FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles