Elizabeth Kilindi, Njombe
WAKATI wazazi wengi wakitamani watoto wao wafanye vema darasani, hali ni tofauti katika Wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe.
Katika wilaya hiyo, shule za msingi Igodivaha na Kinenulo wazazi wamekuwa wakiwashawishi watoto wao kufanya vibaya katika mitihani yao ya mwisho na hivyo kuongeza idadi ya wanafunzi waliofeli.
Baadhi ya wazazi wilayani humo wamekuwa na tabia ya kuwafundisha watoto wao kuandika madudu katika mitihani yao ya darasa la saba ili wafeli wasiendelee na masomo ya sekondari na badala yake wasaidie shughuli za nyumbani ikiwamo kilimo.
Jambo hilo limekuwa likifanywa zaidi na wazazi ambao wamekuwa wakidai hawana fedha za kuwaendeleza watoto wao kusoma sekondari.
Shule hizo zilizopo katika Kata ya Imalinyi, zimekuwa zikishika nafasi ya mwisho miaka mitatu mfululizo katika matokeo ya darasa la saba.
Sababu kubwa ikiwa ni wazazi kuwashawishi wanafunzi kufanya vibaya katika mtihani wa darasa la saba.
Changamoto hiyo imekuwa ikijadiliwa katika vikao mbalimbali vya masuala ya elimu wilayani na mkoani bila ya kuleta matokeo chanya.
Wakizungumzia suala hilo, wanafunzi hao wanasema baadhi ya wazazi huwalazimisha kukataa shule au kuwashauri wakosee majibu ya mitihani ya darasa la saba ili wawapunguzie gharama za kusomesha.
“Kuna mwenzetu mmoja alikuwa na akili sana, matokeo yalivyotoka hakufaulu kujiunga na kidato cha kwanza, tulipomuuliza akasema baba yake atampa ng’ombe,” anasema Mary Msigwa, moja wa wanafunzi hao.
Nao walimu wa shule hizo wanakiri kitendo cha wazazi kuwashawishi watoto wao kuweka majibu ya uongo kwenye mitihani ya kuhitimu darasa la saba ili wasifaulu kwenda sekondari.
Abobakar Shemdoe, ni Mwalimu wa Taaluma katika Shule ya Msingi Igodivaha, anasema suala la taaluma shuleni kwao ni changamoto kubwa kwa sababu wazazi hawana mwamko wa elimu, ndio maana wanafikia hatua ya kuwashawishi wanafunzi kufanya vibaya.
Shemdoe anasema wazazi wanaogopa kusomesha kutoakana na ukubwa wa familia.
“Si unajua huku vijijini unakuta mzazi ana watoto wengi hivyo, wanawashawishi wafanye vibaya ili asimpeleke sekondari,’’ anasema.
Anasema matokeo yanayopatikana shuleni hapo yanawavunja moyo kwani huwa wanatumia muda, nguvu kubwa katika kufundisha wanafunzi hao lakini pindi tu mtihani wa mwisho unapofika wanafanya vibaya.
Anasema licha ya kuwapa mbinu za ufaulu, pia hufanya mitihani ya majaribio mara kwa mara, ikiwamo mitihani ya ujirani mwema na huwa wanafanya vizuri, lakini unapokuja mtihani wa taifa wanafeli.
“Tumekuwa tukifanya majaribio mbalimbali lakini bado wazazi wanatukwamisha, wamekuwa wakirudisha taaluma nyuma kwa ngazi ya wilaya, mkoa hadi taifa,” anasema.
“Hapa tunayo mifano ya wanafunzi ambao walifanya vizuri katika mitihani mbalimbali ya majaribio lakini cha kustajabisha unakuta wale waliokuwa wanafanya vizuri wamefeli,” anasema Shemdoe na kuongeza:
“Pia katika kuwatisha watoto, tulikuwa na kesi ya mtoto ambaye baba yake alimtisha kuwa akifaulu atajinyonga, baadaye tulimuita mwanafunzi na kumuonya akaelewa, na baada ya kufanya mtihani alifaulu na wala baba yake hakujinyonga hadi leo hii yupo. Kwa hiyo alikuwa anataka kumtisha tu,” anasema.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Igodivaha, Shedrack Mbwanji, anasema licha ya changamoto hiyo pia suala la upungufu wa walimu linachangia.
Anasema shule yake inakuwa walimu wanne wanaofundisha kuanzia darasa la kwanza hadi la saba.
“Pamoja na kufanya vibaya kwa wanafunzi, bado tunachangamoto nyingine ya walimu ambapo tuna walimu wanne na hivyo wanachoka na kukosa umakini wakati wa ufundishaji,’’ anasema Mbwaji.
“Katika kukabiliana na changamoto hiyo, tumekuwa tukiitisha vikao na viongozi wa kata pamoja na wazazi ili kuwaelimisha juu ya umuhimu wa elimu, lakini hakuna mabadiliko yoyote. Matokea ya mwaka 2018 ndio yalizidi kuwa mabaya,” anasema Mbwaji.
Anasema wanafunzi wakiwa katika mitihani ya kujipima (Mock) wanafanya vizuri cha kushangaza katika mtihani wa mwisho wanafanya vibaya.
“Baada ya kuona mwanafunzi anafanya vizuri katika mitihani ya kujipima, ilitulazimu kuwaita wazazi na wanafunzi waliofanya vibaya ili kujieleza, moja ya sababu ikawa ni kushawishiwa na wazazi,” anasema Mwalimu Mbwaji.
Rahel Mbilinyi ni Mkuu wa Shule ya Msingi Kinenulo, anasema baadhi ya wazazi katika maeneo hayo wamekuwa chanzo cha kukwamisha ndoto za watoto wao.
“Wazazi ndio wanaokwamisha elimu ya watoto wao, unakuta katika mitihani mbalimbali ya kujipima mtoto anafaulu vizuri lakini pindi anapofanya mtihani wa darasa la saba anafeli. Hii ni changamoto,” anasema Mwalimu Mbilinyi.
Anasema changamoto hiyo imekuwa ikififisha juhudi za walimu katika ufundishaji.
“Tegemeo la mwalimu yeyote ni kuhakikisha anamfundisha mtoto hadi anaelewa na siku ya mtihani afanye vizuri, sasa unakuta una uhakika wa kufaulisha halafu mwanafunzi anafeli,” anasema.
Anaongeza: “Maeneo haya hawataki kabisa kuchangia chochote katika suala la elimu, mwamko wao katika elimu ni mdogo na utaratibu wetu huku mtoto akifaulu anakwenda kusoma bweni, jambo hilo ndio hawalitaki kabisa wazazi.”
Wakizungumzia suala hilo, wazazi wanakiri, wakisema wapo baadhi ya wazazi ambao wameipa kisogo elimu na hivyo kuwashawishi watoto wao kufanya vibaya.
Agnes Kilamya anasema wazazi ndio chanzo, wanawashawishi watoto kufanya vibaya ili wawasaidie kufanya shughuli za kilimo.
“Sisi huku vijijini tunategemea kilimo, lakini isiwe chanzo cha kukatisha ndoto za watoto wetu. Unakuta mzazi bila ya aibu anamwambia mtoto wake mimi sina uwezo fanya vibaya unisaidie kulima,” anasema Agnes na kuongeza:
“Watoto wengine ni yatima, wanaishi na bibi hivyo uwezo wao kifedha ni mdogo, sasa anamwambia mtoto ukifaulu nani atakusomesha, basi mwanafunzi anaamua kufanya vibaya,” anasema Agnes.
Naye Daudi Mbwiro, anasema sababu kubwa ya wazazi kuwashawishi watoto wao kufanya vibaya ni kukosa fedha za kusomeshea.
Silvesta Msigara anasema gharama ya kupeleka mtoto sekondari ni kubwa, walimu nao wanawafuatilia sana wakishindwa kulipa wanawanyanyasa.
“Michango bado ipo inaendelea, mtoto anarudishwa nyumbani kwa sababu ya michango wakati mimi hela ya kula yenyewe shida,” anasema Msigara.
Kwa upande wake Mratibu wa Elimu, Kata ya Imalinyi, Euzebio Mtasiwa, anasema tatizo hilo kweli lipo na kwamba miaka ya nyuma halikuwa kubwa kama hivi sasa.
Mtasiwa anasema: “Tukawa tunaangalia mwaka jana waliofanya mtihani ni 240, waliofeli 103 na mwaka juzi walifanya mtihani ni 270 waliofeli 30 kitu ambacho si kawaida, kwa hiyo tukashtuka nikaitisha kikao na walimu wakuu tukafanya tathmini, tukabaini kweli hali si nzuri lakini pamoja na kuweka tathmini tukaweka mikakati ya pamoja ili kujikwamua na hali hii,” anasema.
Naye Diwani wa Kata ya Imalinyi, Onesmo Liandala, anasema tatizo hilo lipo na linazungumzwa na wanafunzi wenyewe.
“Baada ya wanafunzi hawa kufeli kuliko tulivyotarajia, tuliitisha vikao na wazazi pamoja na wanafunzi waliofeli ambapo walikiri kuwa walishawishiwa na wazazi,” anasema Liandala.
Liandala anasema baada ya hapo alifatwa na mwanafunzi ambaye baba yake alimuhaidi ng’ombe iwapo atafanya madudu lakini alivyofanya hakupewa ng’ombe.
“Mtoto mmoja kati ya wale waliofeli alinifuata akaniambia baba yake alimuahidi ng’ombe kama atafeli, lakini hakumpa na akaniomba niwaambie wazazi wake wauze yule ng’ombe ili yeye aende shule.
“Nilimwambia mzazi wake akauza ng’ombe na kumpeleka sekondari,” anasema Liandala.