Na Adili Mhina, Mwanga
Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) imewapongeza walimu wa Wilaya ya Mwanga kwa kuendelea kufanya kazi kwa weledi na nidhamu licha ya changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Pongezi hizo zimetolewa mwishoni mwa wiki na Mkurugenzi wa Idara ya Ajira, Maadili na Maendeleo ya walimu kutoka TSC, Christina Hape alipofanya ziara wilayani hapo kwa lengo la kukutana na kuzungumza na walimu juu ya masuala mbalimbali ya kiutumishi.
Hape alieleza kuwa TSC inatambua changamoto mbalimbali za wilaya hiyo ikiwemo upungufu wa walimu pamoja na shule nyingi kuwa maeneo ya mbali ambapo miundombinu na huduma mbalimbali bado hazijafika.
Aliongeza kuwa, licha ya changamoto hizo, walimu wa wilaya hiyo wamekuwa mfano wa kuigwa kutokana moyo wa kufanya kazi kwa bidii na kwa nidhamu, kitu kinachofanya Mkoa wa Kilimanjaro kuendelea kuwa miongoni mwa mikoa inayofanya vizuri kitaaluma.
“Kwa kweli Mwanga mnajitahidi kufanya vizuri, tunatambua kuwa yapo maeneo ya milimani ambayo hata kufikika kwake ni changamoto. Nimeelezwa kuwa hata kufika hapa kwenye mkutano huu wapo baadhi yenu mliolala kwenye magari ili muweze kuwahi,”alisema Hape.
Aliongeza kuwa; “Pamoja na changamoto hizo mmeendelea kufanya kazi kwa kujituma na kwakweli hata kule makao makuu hatujapokea rufaa nyingi zinazohusu utovu wa nidhamu kwa walimu wa mwanga, naomba niwapongeze sana kwa hilo,” alisema.
Mkurugenzi Hape alifafanua kuwa, suala la upungufu wa walimu sio la wilaya hiyo peke yake bali maeneo mengi ya nchi kuna upungufu wa walimu na tayari serikali imeamua kuchukua hatua za haraka ili kukabiliana na tatizo hilo.
“Mtakumbuka kuwa hivi karibuni Rais wetu mpendwa Mama Samia Suluhu Hassan alizungumzia suala la upungufu wa walimu na kuagiza suala hilo tulishughulikie kwa haraka. Vilevile, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Ummy Mwalimu naye amesisitiza kuwa hataki kuona shule yenye walimu wawili au watatu,” alisema Hape.
Aliongeza kuwa maagizo ya viongozi hao kuhusu kutatua changamoto ya upungufu wa walimu inaifanya TSC pamoja na mamlaka nyingine zinazohusika kuchukua hatua za haraka kuhakikisha walimu wanaajiriwa ili kujaza maeneo yenye upungufu.
Pamoja na hayo, Mkurugenzi huyo alipongeza ushirikiano uliopo kati ya ofisi ya TSC wilaya pamoja na Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mwanga na kusema kuwa ushirikiano huo ndiyo unaofanya walimu wafanye kazi kwa moyo, nidhamu na weledi.
“Nishukuru ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji pamoja na ofisi ya TSC wilaya kwa kuwa mnafanya kazi kama timu moja, hakuna mivutano. Kaimu Katibu wa TSC, Maafisa Elimu pamoja na Maafisa Utumishi mnazungumza lugha moja katika kutatua kero za walimu. Hii imefanya hata katika masuala ya kupandisha madaraja sijasikia malalamiko kuwa kuna mwalimu amesahaukika,” alisema Hape.
Akitoa taarifa fupi ya utendaji wa TSC wilayani hapo, Kaimu Katibu Msaidizi wa TSC wilaya ya Mwanga, Catherine Kimaro alisema kuwa, wilaya hiyo ina jumla ya walimu 1120 wanaofundisha shule za Serikali. Katika idadi hiyo, walimu 558 ni wa shule za msingi na 562 ni wa shule za sekondari.
Kimaro alieleza kuwa, wilaya hiyo kwa sasa haina shauri lolote la nidhamu kutokana juhudi za ofisi yake za kutoa elimu kwa walimu mara kwa mara kuhusu miiko na maadili ya utendaji wa kazi.