WANAFUNZI wanne wa ualimu waliomfanyia ukatili wa kumchapa fimbo na kumpiga makofi mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya Kutwa ya Mbeya (Mbeya Day), Sebastian Chinguku (17), wamekamatwa na Jeshi la Polisi.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Paul Mtinika, walimu hao waliokuwa katika mafunzo ya vitendo katika shule hiyo ambao ni Franky Msigwa, Deo John na Evance Sanga wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Dar es Salaam (DUCE) na Sanke Gwamaka wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere walikamatwa wakati tukio hilo lililotokea Septemba 28, mwaka huu katika ofisi ya walimu shuleni hapo likiendelea kuchunguzwa.
“Walimu wamekamatwa kwa sababu Serikali ina mkono mrefu na uchunguzi unaendelea kufanyika,” alisema.
Mtinika ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Mbeya alisema wamebaini kuwa shule hiyo ina tatizo kubwa la utovu wa nidhamu.
Alisema walibaini tatizo hilo baada ya mgomo baina ya walimu na wanafunzi kutokea shuleni hapo jana.
Mtinika alisema mgomo huo ulipotokea Serikali iliingilia kati na kufanikiwa kuumaliza baada ya walimu kushindwa kufundisha huku wanafunzi nao wakishindwa kuingia darasani kuendelea na masomo.
“Leo (jana) asubuhi tulipata taarifa kwamba baada ya tukio la mwanafunzi Sebastian kutokea walimu wamegoma kuingia darasani huku wanafunzi nao walionekana kutokuwa na mwamko wa kuendelea na masomo hivyo ilitulazimu kufika na kulitatua tatizo hili,” alisema Mtinika na kuongeza:
“Ili kuinusuru hali hiyo Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Mbeya kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla ililazimika kuingilia kati kulimaliza.
“Ile shule ni kubwa ina wanafunzi 1,467 na walimu 70 na baada ya kuongea nao tuligundua kuna tatizo la utovu wa nidhamu na Sebastian aliyepigwa naye ni miongoni mwa wanafunzi wasiokuwa na nidhamu na tumewaambia wafuate taratibu za shule.”
Alisema kitendo cha tukio hilo kusambaa na kuzua mjadala juzi katika mitandao ya kijamii huku Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene, kuingilia kati na kuagiza hatua za kuwafukuza walimu hao na kuwakamata ndicho kilichosababisha walimu na wanafunzi wa shule hiyo kupatwa na mshtuko kushindwa kuingia darasani.
“Kwa hiyo tumezungumza na walimu na kuwakumbusha wajibu wao kwa wanafunzi huku wanafunzi nao tumewaambia kutambua wajibu wao pindi wakiwa shuleni likiwamo suala la nidhamu ambalo ndio silaha ya kila kitu,” alisema.
Mtinika alisema Serikali inafahamu changamoto wanazokutana nazo walimu lakini ni vema wakafuata taratibu za kisheria kwa sababu tukio hilo lilikuwa wazi na halizuiliki, ushahidi unajionyesha.
“Kama mwanafunzi ni mtovu wa nidhamu, taratibu zipo na adhabu za kupewa zimeorodheshwa hivyo hakukua na sababu ya kupigwa kama mwizi jambo ambalo halikubaliki nchini kwa sababu hata Katiba yetu imeelekeza,” alisema.
Kuhusu utekelezaji wa agizo la Simbachawene la kuitaka Mamlaka ya Nidhamu ya Walimu kumvua madaraka Mwalimu Mkuu wa Mbeya Day, Magreth Haule, kutokana na kushindwa kutoa taarifa ya tukio hilo, Mtinika, alisema mwalimu huyo ataendelea na majukumu yake kwa sababu linaendelea kuchunguzwa.
Kwa upande wake, Mwalimu Haule, aliyejitetea kuwa hakuwapo shuleni na alimkabidhi majukumu yote Makamu wake, Adonath Nombo, wakati tukio hilo linatokea na alisema kwa sasa hawezi kuzungumza chochote bali anasubiri kutekeleza maagizo yaliyotolewa hadi atakapopewa muongozo mwingine.
WALIMU WAFUNGUKA
Wakizungumzia sababu ya wao kushindwa kuingia darasani, baadhi ya walimu wa shule hiyo walisema mara kadhaa Serikali imekuwa mstari wa mbele kutatua matatizo yanayowapata wanafunzi huku wakiwasahau wao wanaofanyiwa vitendo viovu na wanafunzi.
“Hapa sitetei tukio la Sebastian, ila ninapenda kuieleza Serikali hasa viongozi wetu wa juu pale walimu wanapowasilisha matatizo ya wanafunzi au uongozi wa shule unapotoa adhabu kwa wanafunzi kama vile kuwasimamisha shule kwa muda kutokana na matatizo ya nidhamu basi wasiingilie,” alisema mwalimu mmoja ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe.
WANAFUNZI NAO WANENA
Gazeti hili lilifanikiwa kuzungumza na baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo ambao walisema tukio hilo liliwashtua kwa sababu hawakutarajia kama mwenzao angeweza kupatiwa adhabu ya namna hiyo.
“Ni kweli mwanafunzi ana makosa hatukatai lakini adhabu ya namna ile hakustahili kupewa kwa sababu sisi tulijua mwalimu amemalizana naye darasani kwa kumchapa viboko vitano kumbe, kipigo kiliendelea” alisema Mwanafunzi.
SEBASTIAN AFUNGUKA
Akizungumzia sakata hilo, Sebastian, alisema adhabu ya pamoja na wanafunzi wenzake aliitumikia kwa kuchapwa viboko vitano lakini alishangaa mwalimu aliyemtaja kwa jina la Franky kumuita pembeni na kuanza kumuuliza maswali ambayo yeye binafsi anadai alimjibu.
“Mwalimu Franky aliniita pembeni na kuniuliza kwamba unanikumbuka ? Mimi nikamjibu hapana, akaniuliza mara nyingine, tena kwa msisitizo unikumbuki kweli au ni kiburi? Nikamjibu sikukumbuki,” alisema.
Sebastina alisema baada ya hapo mwalimu huyo alimwambia kwamba anakumbuka siku ya mtihani alimwambia avue sweta lake lakini na siku hiyo alimdharau na alimwamuru amfuate ofisini.
“Alinipeleka ofisini, huku akiwa na walimu wenzake na kuanza kuniadhibu kwa kipigo ambacho nyinyi wenyewe mmekiona na mbali na hilo walimu hao walinishinikiza niandike barua ikiwa na maelezo kwamba mimi ndiye niliye wapiga walimu jambo nililolifanya kwa kuogopa kufukuzwa shule,” alisema.
Sebastian alisema wakati walimu wa kawaida wakilijadili suala hilo alionekana amekosa na kumlazimu kumtamfuta mwalimu ambaye ni jirani yake na kumweleza ukweli wa tukio lote.
“Mwalimu huyo alifanya upelelezi wake na kubaini kwamba mimi sikuwapiga walimu bali walimu ndio walinipiga mimi hivyo kuwaita na kunitaka mimi nichague adhabu ya kuwapa lakini niliwaeleza kwamba shule ina utaratibu wake juu ya walimu wa namna hiyo lakini mimi binafsi nimewasamehe,” alisema.
DUCE
Akizungumza na gazeti hili kwa sharti la kutotajwa jina lake gazetini mmoja wa wahadhili wa DUCE alisema utekelezwaji wa agizo la Profesa Ndalichako bado haujafanyika na hakuna kikao chochote cha kiofisi kilichofanyika jana kwa sababu kwa sasa chuo hicho kimefungwa.
“Mimi sio msemaji lakini naweza kusema haya mambo bado yanaongelewa kwenye korido hapa chuoni kwamba vijana hawa hawana makosa lakini bado hayajajadiliwa kiofisi, kwa bahati mbaya suala hili limetokea chuo kikiwa kimefungwa,” alisema mhadhiri huyo.
Alisema mbali na kuwa vijana hao kitaaluma wanaonekana hawajafanya kosa kubwa la kupatiwa adhabu yenye uzito huo lakini agizo la Profesa Ndalichako lazima litekelezwe kwa sababu kwa sasa limekaa kisiasa zaidi.
“Kumfukuza mtu chuo sio rahisi kama mnavyofikiria kuna taratibu zake, wale ni wanafunzi wamefanya kosa la kawaida ili wachukuliwe hatua taratibu zilipaswa kuanzia shule husika walipaswa waandike barua ije kwenye uongozi wa chuo,” alisema.
Alisema barua hiyo ilipaswa kuwasilishwa katika kikao cha Bodi ya Uongozi wa DUCE na badaye taratibu zingetolewa na adhabu zingefuatwa.
Alisema waziri hana mamlaka ya kumfukuza mwanafunzi chuo hivyo uamuzi uliotolewa umekaa kisiasa zaidi na msukumo wa mitandao ya kijamii.
HAKI ELIMU
Shirika lisilokuwa la kiserikali la Haki Elimu limesema tukio la Sebastian ni sehemu tu ya matukio mengi ya ukatili wanayofanyiwa wanafunzi shuleni.
Pia lilisema kuwa kuwa matukio hayo ya kikatili yamezifanya shule kutokuwa sehemu rafiki na salama kwa wanafunzi na hivyo kuwa na athari kubwa katika juhudi zao za kujifunza.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Haki Elimu, John Kalage, alisema kwa mujibu wa utafiti uliofanywa mwaka 2011 na Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) kuhusu ukatili dhidi ya watoto unaonyesha kuwa kuna viwango vya kutisha vya kikatili dhidi ya watoto katika shule nyingi nchini.
Alisema vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa wanafunzi ni pamoja na vitendo vya kingono na kihisia katika mazingira ya shule za Tanzania na kwamba walimu ndio vinara wa ukatili huo.
“Kwa mujibu wa utafiti huo nusu ya wasichana na wavulana ambao wamewahi kunyanyaswa kimwili (kufinywa, kuchapwa viboko na kupigwa mateke) waliwataja walimu kuwa ndio wanyanyasaji wakuu shuleni nchini Tanzania,” alisema Kalage.
Alisema wamesikitishwa na kitendo cha ukatili aliofanyiwa Sebastian.
BODI YA MIKOPO
KUSITISHWA KWA MIKOPO YA WANAFUNZI WALIOHUSIKA KATIKA TUKIO LA KUMDHURU MWANAFUNZI HUKO MBEYA
Katika hatua nyingine, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imesitisha mikopo ya elimu ya juu iliyokuwa ikitolewa kwa walimu-wanafunzi hao waliosimamishwa masomo kwa kuhusika katika tukio la Sebastiani.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana walimu hao wamepoteza sifa za kuendelea kupokea mikopo.
“Mikataba inayosainiwa na wanufaika wa mikopo inawataka wanufaika kuzingatia masharti kadhaa ikiwa ni pamoja na kuzingatia nidhamu na kufuata sheria na taratibu za vyuo na mamlaka halali,” ilisema taarifa hiyo na kuongeza:
“Kwa mujibu wa taratibu za kukopeshwa, wanafunzi hawa watatakiwa kuanza kurejesha kiasi walichokopeshwa mara moja. Bodi ya Mikopo inawakumbusha wanufaika wanaoendelea masomo kuzingatia masharti ya ukopeshwaji na kuheshimu sheria, kanuni taratibu na kuwa mfano mwema katika jamii.
“Mikopo na ruzuku zinazotolewa na Serikali ni kwa ajili ya kuwaandaa kuwa raia wema, waadilifu, na wachapa kazi ili kujenga uchumi imara na ustawi kwa wote.”
Habari hii imeandikwa na Upendo Fundisha (Mbeya), Khadia Hamis na Aziza Masoud (Dar es Salaam)