26.6 C
Dar es Salaam
Saturday, November 30, 2024

Contact us: [email protected]

Walemavu waisimamisha Dar

Asifiwe George na Mgeni Shabani (EWTC), Dar es Salaam
WATU wenye ulemavu jana wamelazimika kufunga makutano ya barabara za Kawawa na Uhuru kwa kulala katikati ya taa za kuongoza magari kwa zaidi ya saa sita kama njia ya kupinga hatua ya Manispaa ya Ilala kuwavunjia meza zao za biashara katika Soko la Mchikichini.
Wafanyabiashara hao walikusanyika katika eneo hilo, hali iliyowafanya madereva wa magari wanaotumia barabara hizo kusota kwenye foleni kwa muda mrefu.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Umoja wa Wafanyabiashara Walemavu, Kidumke Mohamed, alisema juzi walipofika katika maeneo yao ya biashara walishangaa kukuta zaidi ya meza 200 wanazofanyika biashara zikiwa zimevunjwa na mizigo yao ikichukuliwa na mgambo wa Manispaa ya Ilala.
Alisema hawajui kuwa ni nani aliyeharibu vitu vyao, wakati Serikali iliwaruhusu kwa barua ya maandishi kufanya biashara katika soko hilo huku wakisubiri kutafutiwa eneo lingine.
“Tumeamua kufunga barabara hii ili tuweze kupata suluhu kwa viongozi wa Serikali. Hasara tumepata na haujui la kufanya mpaka sasa zaidi ya kuwa masikini,” alisema Mohamed.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Walemavu Wilaya ya Ilala, John Mleba, alisema Serikali imeamua kuvunja sheria ya makubaliano ya maandishi kwa kuwavunjia maeneo yao ya biashara.
“Tatuwezi kuondoka hapa wala kuruhusu barabara kupita hadi pale litakapopatiwa ufumbuzi wa suala letu hili la eneo la biashara na mali zetu ambazo zimeharibiwa.
“…hapa hatutoki hadi Mkuu wa Mkoa, Said Meck Sadiki atakapokuja ili kutatua suala hili, yeye ndiye aliyeturuhusu kufanya biashara katika soko hili kwa makubaliano ya maandishi, sasa tunashangaa wametufanyia hivi bila kutupa taarifa.
“Wangetupatia taarifa mapema sisi tungeondoa vitu vyetu, lakini wameviharibu na vingine wamevibeba wakati sisi tunapata fedha za kujikimu kimaisha kupitia biashara hizi,” alisema Mleba.
Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Raymond Mushi, alifika katika eneo hilo kwa lengo la kutafuta suluhu ikiwemo kuwataka wafanyabiashara hao kufungua barabara lakini alijikuta akifukuzwa.
Baada ya dakika chache, Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Ilala, naye alijikuta akifukuzwa na wafanyabiashara hao.
Wakati wa barabara hiyo ikiwa imefungwa, wafanyabiashara hao waliruhusu kupita magari ya jeshi pamoja na yale ya wagonjwa.
Ilipotimu sasa tisa alasiri uongozi wa Manispaa ulikwenda tena kuwahisi viongozi hao ili waende kukaa kikao cha pamoja ili kutafuta suluhu la mgogoro huo.
Katika kikao hicho, DC Raymond Mushi alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa lengo la kubomoa vibanda hivyo ni kupisha utanuzi wa barabara ya watembea kwa miguu katika eneo hilo.
Alisema kutokana na hali hiyo, waliafikiana kwa njia ya maandishi kwa mara ya pili kuwa wenye uwezo warudi na watengeneze meza zao na kuendelea kufanya biashara na wale wasiokuwa na uwezo wasubiri uchunguzi wa kutathmini athari zilizotokea ili walipwe fidia ya vitu vyao vilivyoharibika.
Pamoja na kupewa ahadi hiyo, lakini waliitaka Serikali kuhakikisha kuwa ifikapo leo iwe imefanya tathmini ili waweze kulipwa fidia ya mali zao.
Baada ya kikao hicho cha mashaurino, ilipotimu saa 10:30 jioni, Mkuu wa Oparesheni Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Naibu Kamishna Simon Siro, aliwaamuru askari wa kuruhusu magari yaliyokuwa yamezuiwa na wafanyabiashara hao ili yaweze kuendelea na safari.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles