26.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Wakurugenzi hawatasimamia uchaguzi – NEC

Na Elizabeth Hombo

-DAR ES SALAAM

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imesisitiza vifungu vya sheria vilivyokuwa vikiruhusu wakurugenzi wa halmashauri za wilaya, miji na majiji kusimamia uchaguzi ambavyo Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imevitengua, havitatumika katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Kauli hiyo ya NEC imekuja wakati kukiwa na sintofahamu, hasa baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Dk. Aderladus Kilangi, kuwasilisha kusudio la kukata rufaa kupinga utekelezaji wa hukumu hiyo.

Katika hoja zake, AG alisema utekelezaji wa hukumu hiyo unasimama hadi pale rufaa ya Serikali itakapoamriwa.

Hata hivyo, akizungumza katika mkutano wa NEC na wahariri wa vyombo vya habari kuhusu uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura ambao uandikishaji wake unatarajiwa kuanza Julai, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Semistocles Kaijage alisema katika kutekeleza majukumu yao, vifungu hivyo vya Sheria ya Uchaguzi 7(1) na 7(3) havitatumika.

Mkutano huo ulifanyika jana katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha  Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.

Jaji Kaijage ambaye alikuwa akijibu swali aliloulizwa na mwandishi aliyetaka kujua msimamo wa NEC baada ya mahakama kuondoa vifungu hivyo, alisisitiza pasipo kueleza kwa kina kuwa “vifungu vingine vya sheria hiyo ambavyo havikulalamikiwa vitaendelea kutumika kama kawaida”.

Pamoja na hayo, Jaji Kaijage  hakufafanua ni nani ambao watasimamia uchaguzi baada ya wao kuamua kutotumia vifungu hivyo.

HUKUMU YA MAHAKAMA KUU

Mei 10, mwaka huu, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam katika hukumu yake iliyotolewa na jopo la majaji watatu – Dk. Atuganile Ngwala, Dk. Benhajj Masoud na Firmin Matogolo, ilibatilisha kifungu cha 7(1) cha Sheria ya Uchaguzi kinachoipa mamlaka NEC kuwateua wakurugenzi wa majiji, manispaa na miji kuwa wasimamizi wa uchaguzi kwa kuwa kinapingana na sheria mama, yaani Katiba.

Katika kesi hiyo iliyofunguliwa na mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Bob Wangwe, aliyekuwa akitetewa na Wakili Fatma Karume, pia mahakama hiyo ilibatilisha kifungu cha 7(3) kinachoipa NEC mamlaka ya kuteua mtu yeyote miongoni mwa watumishi wa umma kuwa msimamizi wa uchaguzi.

 Mahakama ilisema vifungu hivyo ni kinyume cha Katiba ya nchi ikibainisha kuwa wakurugenzi hao ambao si waajiriwa wa NEC, huteuliwa na rais aliyeko madarakani, ambaye hutokana na chama tawala na kwamba wengine ni wanachama wa chama cha mamlaka inayowateua jambo ambalo huathiri utendaji wao katika kutenda haki.

Alisema kifungu cha 7(1) kinasema kila Mkurugenzi wa Jiji, Manispaa na Halmashauri anaweza kusimamia uchaguzi wakati viongozi hao ni wateule wa Rais na si waajiriwa wa NEC wakati Katiba inasema NEC inapaswa kuwa huru na haki.

Jaji Ngwala alisema kutokana na hali hiyo, kifungu hicho kinakinzana na sheria mama ambayo inasimamia nchi. Pia kifungu cha 7(3) kinasema kuwa NEC inaweza kuteua mtu yeyote kuwa msimamizi wa uchaguzi bila ya kuainisha ni mtu wa aina gani.

Jaji Ngwala alisema, lakini Katiba inasema kuwa mtu yeyote anayekuwa msimamizi wa uchaguzi hapaswi kuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa.

Mei 13, AG Dk. Kilangi alisema Serikali imewasilisha katika Mahakama ya Rufani kusudio la kukata rufaa kupinga hukumu ya Mahakama Kuu kuwazuia wakurugenzi kusimamia uchaguzi kwa niaba ya NEC.

Dk. Kilangi alisema tayari Serikali kupitia kwa Wakili Mkuu wa Serikali (SG) imewasilisha taarifa ya kusudio la kukata rufaa kupinga hukumu hiyo.

Alisema kuwapo kwa hukumu hiyo hakuathiri chaguzi nyingine zijazo, zikiwemo ndogo, kwani baada tu ya kuwasilisha taarifa hiyo ya kusudio la kukata rufaa utekelezaji wa hukumu hiyo husimama, hadi pale rufaa itakapoamuliwa. 

WASIMAMIZI/WATENDAJI MAKADA 

Aidha Jaji Kaijage ambaye alizungumzia hofu ya kuwako kwa makada ndani ya NEC na wasimamizi wa uchaguzi, changamoto ya mawakala na  mchakato wa kuboresha daftari, alisema mtu yeyote ndani ya tume hiyo na wasimamizi wa uchaguzi  watakaothibitika kuwa ni makada wa chama chochote  cha siasa wataondolewa.

Jaji Kaijage alikuwa akijibu maswali kadhaa ya wahariri na waandishi yaliyoelekezwa NEC  kuhusu hofu ya kuwako kwa watendaji wa tume na wasimamizi wa uchaguzi  ambao ni makada wa vyama vya siasa na hivyo kuibua changamoto kila unapofanyika uchaguzi.

Katika hilo, alisisitiza kuwa  hawataruhusu kada wa chama chochote cha siasa kusimamia uchaguzi, lakini pia kuwa mtendaji wa tume.

“Sheria zipo wazi, mtu akienda kinyume atachukuliwa hatua, kama mtu atathibitika kwa ushahidi kuwa ni mwanasiasa, hapaswi kutekeleza majukumu ya NEC.

“Tukipokea malalamiko kwa wakati kama msimamizi ni kada wa chama fulani, kama mazingira yakionekana dhahiri atatafutwa mbadala,” alisema. 

UTEUZI WA MAPURI

Jaji Kaijage pia alilazimika kuzungumzia uteuzi wa Kamishna wa Tume hiyo, Omary Ramadhani Mapuri ambaye alipata kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Waziri wa Mambo ya Ndani na baadae balozi baada ya kuulizwa ni namna gani NEC inajitenga na malalamiko kwamba baadhi ya watendaji wake ni makada wa chama hicho tawala.

“NEC hakuna mwanachama hai wa chama chochote, kuna historia kwamba ulitoka hapa ukaenda pale, ulikuwa hivi na ukawa hivi, lakini hakuna utaratibu kwamba utabaki katika nafasi hiyo hiyo, hiyo ni historia tu.

“Mimi niwahakikishie tu kama kuna mtu alikuwa mwanachama wa chama fulani anabanwa na masharti ya Katiba, na wale ambao wamepata kuwa viongozi wa vyama vya siasa kuna fomu maalumu ya kujaza. Kuna kiapo ‘una-declare’  kuondoka, hakuna hata shabiki ndani ya tume, Katiba na sheria zinatubana,” alisema Jaji Kaijage. 

TATIZO MAWAKALA UCHAGUZI 

Katika mkutano huo, NEC ilieleza sababu zinazochangia changamoto na wakati mwingine vurugu nyakati za uchaguzi, hasa linapokuja suala la mawakala wa uchaguzi.

Jaji Kaijage alisema hilo linatokana na vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi kushindwa kuwasilisha kwa wakati majina ya mawakala wao.

Alisema taratibu zinataka vyama hivyo kupeleka majina ya mawakala ndani ya siku saba, lakini wao wamekuwa wakipeleka siku ya uchaguzi na hivyo msimamizi kukataa kupokea na mgogoro huanzia hapo.

Akitolea mfano uchaguzi mdogo wa Jimbo la Monduli, alisema mawakala wa chama kimoja cha siasa ambao hakuwataja, lakini ni Chadema, waliondolewa kwa sababu majina yao yalifikishwa nje ya muda wa kikanuni.

Alisisitiza iwapo vyama vya siasa vitazingatia sheria, kanuni na Katiba, migogoro kama hiyo na mingine haitakuwepo.

“Kwa siku za usoni hatutarajii kupata malalamiko kwa sababu tumewasisitiza wadau wetu wakuu, ambao ni vyama vya siasa, wafuate na kuheshimu  masharti na kanuni,” alisema.

Zaidi alisema tayari wamewashirikisha wadau wao hao mchakato wote wa uchaguzi kuanzia uandikishaji wapigakura hadi katika kamati mbalimbali zilizoundwa na NEC ambazo zina wawakilishi wa vyama vyao.

MASHINE 3,000 ZA BVR

Kuhusu kuandikisha wapigakura wapya Julai mwaka huu, NEC ilisema wanazo mashine za BVR 3,000 zitakazotumika kwa zoezi hilo.

Tofauti na Uchaguzi Mkuu uliopita wa 2015, zoezi linalotarajiwa kuanza sasa litawashusisha wale ambao wamefikisha umri wa miaka 18, waliopoteza vitambulisho, na wale waliohama vituo.

NEC ilisema kwa kuwa zoezi hilo litahusisha idadi ndogo wanaamini mashine hizo zitatosha.

Akizungumzia kuhusu vituo vya kuandikisha wapigakura, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Dk. Ramadhani  Kihamia, alisema vimeongezeka kutoka 36,549 mwaka 2015 hadi 37,407 2018 kwa Tanzania Bara na kwa upande wa Zanzibar kutoka 380 hadi 407.

Kuhusu asasi za kiraia kutoa elimu kuhusu mchakato huo, alisema zipo 24. Katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 zilikuwa 447.  

Pamoja na hilo, Kihamia alisisitiza kuwa takwa la kisheria la uboreshaji daftari la wapigakura mara mbili baada ya uchaguzi mwingine litatekelezwa.  

SABABU UCHAGUZI HURU/HAKI

NEC pia imeeleza hatua kadhaa walizochukua ambazo zitafanya uchaguzi ujao uwe huru na haki kuwa ni pamoja na mchakato shirikishi.

“Uchaguzi ni suala la Katiba na sheria, hatupaswi kuwa woga kwamba hauwezi kuwa huru na haki, sisi tunafanya chaguzi shirikishi. Kila hatua tume inashirikisha wadau wote,” alisema Jaji Kaijage.

Alizitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na mchakato wa kutunga kanuni, kuteua watendaji wa kusimamia zoezi la kuandiksha wapigakura kwa kufuata taratibu, kanuni, sheria ambao majina yao yatawekwa wazi  kwa mujibu wa kanuni ya 8 na 9 ya uchaguzi.

Alisema orodha ya majina hayo pia watapewa vyama vya siasa ili waweze kutoa maoni yao na wameelezwa hakuna aliye juu ya sheria.

Kuhusu mtu anayekiuka taratibu, alisema hatua zimewekwa wazi kwenye kifungu cha 89(A)  cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi na 88(A) ya Serikali za Mitaa kwamba mtendaji au ofisa atakayekwenda kinyume atakuwa ametenda kosa la jinai  na adhabu yake ni faini ya sh 500,000 na kifungo kisichozidi miaka miwili.

Alisema NEC ikipata malalamiko kwa wakati ama ya ukada au mengine yanayoweza kutengua uchaguzi na yakathibitika, watawaondoa wahusika.

Katika hilo, alisisitiza  kwa kuwa mamlaka zimeweka taratibu za kusikiliza rufaa, nafasi hiyo wanayo  kwa mtu yeyote kuwasilisha  mapingamizi, lakini alisisitiza mchakato huo uzingatie sheria na  kanuni. 

Pia alisema wakati wa mchakato wa uandikishaji, vyama vina nafasi ya kuweka mawakala wao.

Alisema hata katika Uchaguzi Mkuu kutakuwa na ushirikishwaji huo huo, ikiwa ni pamoja na kuwaingiza wawakilishi wa vyama vya siasa kwenye kamati mbalimbali ikiwamo ile ya maadili kuanzia chini hadi juu.

Alisisitiza kuwa sheria zimeweka uchaguzi unaozingatia uhuru na haki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles