24.4 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Wakulima wageukia kilimo cha alizeti

AMON MTEGA-SONGEA

BAADHI ya wakulima wilayani Songea, Mkoa wa Ruvuma, wameamua kulima mazao mbadala kama alizeti na soya ili kupunguza changamoto za soko zinazowakuta kwenye zao la mahindi. 

Akizungumza na MTANZANIA jana, mmoja wa wakulima maarufu Mkoa wa Ruvuma, Isaya Mbilinyi maarufu kwa jina la Mwilamba, alisema wakulima wengi mkoani hapa wameamua kupanua kilimo kwa kulima mazao mengine kama alizeti na soya kutokana na zao la mahindi kuwa na changamoto mbalimbali zikiwamo za kukosa soko. 

Mwilamba ambaye pia amelima ekari 40 za alizeti katika Kijiji cha Magima kilichopo Peramiho, Wilaya ya Songea, alisema pamoja na kwamba mahindi yanakabiliwa na changamoto za ukosefu wa soko la uhakika, bado zao hilo limekuwa likikabiliwa na changamoto za ukosefu wa pembejeo kuwa na bei ya juu tofauti na uhalisia wa masoko yaliyopo. 

“Mimi ni mkulima wa mahindi, hivyo natambua changamoto zilizopo kwenye zao hilo tofauti na mazao mengine kama alizeti na soya ambayo changamoto zake si kubwa.

“Alizeti na soya ni mazao ambayo hata mtu mwenye mtaji mdogo ana uwezo wa kuyamudu kutokana na kutokuwa na changamoto kubwa ya kuendesha kilimo hicho.

“Kwa hiyo, pamoja na kwamba mimi nimeamua kujielekeza kwenye alizeti, kuna wakulima wengi mkoani hapa wameamua kujielekeza kwenye kilimo cha mazao hayo kwa sababu hayana changamoto nyingi kama yalivyo mazao mengine yakiwamo mahindi,” alisema Mwilamba.

Kwa upande wake, Ofisa Kilimo, Mkoa wa Ruvuma, Andrew Tarimo, alisema ni kweli mazao mbadala kama alizeti na soya yana nafasi ya kuwainua wakulima wa mkoa huo kulingana na mazingira na hali ya hewa iliyopo mkoani hapa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles