26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 27, 2021

WAKULIMA WA ZABIBU WALIA NA GHARAMA ZA UMEME

Na RAMADHAN HASSAN-CHAMWINO


WAKULIMA wa zabibu mkoani Dodoma wamedai changamoto kubwa waliyonayo kwa sasa ni gharama za nishati za umeme kuwa juu.

Akizungumza juzi katika Kijiji cha Chinangali II, wilayani Chamwino kwa niaba ya wakulima wenzake, Mwenyekiti wa Umoja wa Wakulima wa shamba la zabibu la Chinangali II, Justin Shio, alisema changamoto wanayokabiliwa nayo ni mahitaji makubwa ya nishati ya umeme.

Alisema wamekuwa wakilima kilimo cha kisasa ambacho kinahitaji umeme mkubwa kwa ajili ya kupampu maji yanayokwenda shambani, hivyo changamoto kubwa kwao imekuwa ni gharama za kununua umeme huo.

Alisema changamoto nyingine wanayokabiliana nayo ni umbali wa kuvuta maji kutoka visimani hadi bwawani na kuyasukuma kutoka bwawani kwenda shambani.

Kutokana na hali hiyo, alisema uchunguzi maalumu uliofanywa na bodi ulibaini kuwa kuna udokozi wa mavuno ya zabibu za wanachama kuibwa na watu wasio waaminifu, hali inayosababisha mapato duni kwa wanachama.

“Baadhi ya wakulima kwa kushirikiana na wafanyabiashara huhujumu shamba kwa kukwepa kulipa ushuru, hali iliyosababisha kupungua kwa fedha za uendeshaji na kufanya shughuli kama umwagiliaji, ununuzi wa viuatilifu na upulizaji wa viuatilifu.

“Pia baadhi ya wakulima kutokufuata kalenda ya uendeshaji shamba kama ukatiaji, upuliziaji, uwekaji wa mbolea kunakopelekea mavuno kwa nyakati tofauti, mashambulizi ya wadudu na magonjwa kuwa magumu,” alisema.

Naye Diwani wa Kata ya Buigiri, Kenneth Yindi (CCM), aliwataka wakulima hao kuacha kilimo cha mazoea na badala yake kulima cha kisasa, ambacho kitawasaidia katika kukuza vipato vyao.

“Nimesikia hapa kuna jipu, kuna watu wamepiga fedha, nitafuatilia ili nijue ukweli upo wapi, kwani nia yangu ni kuwasaidia muweze kupata fedha, kwani zabibu inapatikana kwa wingi katika kata yangu,’’ alisema.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,388FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles