31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Wakulima wa Pamba MOCS wanunua trekta mbili, kuachana na jembe la mkono

Na Derick Milton, Meatu

Katika kuhakikisha wakulima wake wanaondokana na kilimo cha jembe la mkono wakati wa kuzalisha zao la Pamba, Chama cha Msingi cha Ushirika Meatu Organic Cotton (MOCS –Amcos) kimenunua trekta mbili zenye thamani ya Sh milioni 86.

Kupitia mkopo wenye riba nafuu kutoka Benki ya NMB Chama hicho kimefanikiwa kupata trekta hizo, ambazo wakulima wake zaidi ya 300 ambao ni wanachama watanufaika wakati wa kuandaa mashamba yao.

Trekta mbili aina ya Swalaj 885 zilizonunuliwa na Chama cha Msingi cha Ushirika Meatu Organic Cotton (MOCS –Amcos) kwa thamani ya Sh milioni 86 baada ya chama hicho kupata mkopo wenye riba nafuu kutoka Benki ya NMB. (Picha na Derick Milton).

Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho, Mulisu Ngassa, akizungumza wakati wa kupokea trekta hizo katika hafla iliyofanyika Machi 24, 2022 Meatu amesema chama hicho ambacho kinahudumia wakulima wa vijiji 12 katika Wilaya hiyo kimefanikiwa kupata trekta hizo kupitia mkopo ambao umetolewa na Benki ya NMB.

Ngassa amesema wakulima wa AMCOS hiyo wamekuwa wakipata tabu, wakati wa kuandaa mashamba ambapo asilimia 99 wamekuwa wakitumia jembe la mkono wakati wa kilimo cha pamba na mazao mengine.

Amesema kutokana na hali hiyo, chama hicho kiliweka mipango katika msimu uliopita wa pamba ya kuhakikisha kinawasaidia wakulima wake, ambapo walipanga kununua trekta nne, lakini wamefanikiwa kupata mbili.

“Kupitia ushuru wa pamba, chama chetu kimekuwa na uwezo mkubwa wa mapato….kila msimu tumekuwa tunapata mapato ya zaidi ya Sh milioni 150…kupitia ushuru wa pamba,” amesema Ngassa.

Makamu Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa kutokana na kuwa na uwezo mkubwa kimapato, waliamua kutumia fursa ya mikopo yenye riba nafuu kutoka Benki ya NMB kwa kukopa fedha ambazo zimetumika kununua trekta hizo.

“Benki ya NMB imetupatia mkopo wa Sh milioni 77.8 ikiwemo na riba yake, ambapo mkopo huo tumepewa muda wa miaka mitatu kurejesha na kila mwaka tutakuwa tunarejesha kidogo kidogo.

“Mkopo halisi toka Benki ya NMB nimMilioni 64.5 na riba yake ni milioni 13 na tutarejesha milioni 77.8, awali Amcos ilitoa pesa taslimu kama malipo ya awali ya kununua trekta hizo milioni 21.5,” amesema Ngassa.

Aidha, kiongozi huyo amesema kuwa chama hicho kimejiwekea malengo makubwa, ambapo kimepanga kujenga Maghala ya kuhifadhia pamba 25 kila kijiji, pia kununua trekta 25 ambazo zitagawiwa kwa vijiji 25 ambavyo ni wanachama,” amesema Ngassa.

Meneja wa NMB Wilaya ya Meatu, Waziri Mchalala amewapongeza viongozi wa Amcos hiyo kwa kuchangamkia fursa ya mikopo yenye riba nafuu katika sekta ya kilimo huku akizitaka Amcos nyingine kuiga mfano huo.

“Benki ya NMB inataka kukuza sekta ya kilimo, ndiyo maana imepunguza riba hadi kufikia asilimia 10, tunawaomba wakulima wote katika mazao yote waje mikopo ipo na tutawakopesha kwa ajili ya kuendeeleza kilimo chao,” amesema Mchalala.

Akizungumza kwa niaba ya Mrajisi wa Vyama vya Ushirika Mkoa (Amcos) Kaimu Mrajisi Msaidizi, Billwater Mbilinyi amesema kuwa Ofisi yake imeendelea kuidhinisha matumizi ya fedha za Amcos ambazo zimekuwa na mipango ya maendeleo.

Amesema Amcos nyingi katika mkoa wa Simiyu, viongozi wake wameanza kubadilika na kuwa na mitazamo ya kuleta maendeleo kwa wakulima wao na kuacha tabia za wizi wa fedha za wakulima kama ilivyokuwa awali.

“Tumeidhinisha zaidi ya Sh milioni 200 kwa Amcos mbalimbali kutumia fedha kwa ajili ya maendeleo, ikiwemo Amcos hii, tunaendelea kuzisimamia Amcos zote ili ziwe na mtazamo kama huu na tuwatake wengine waige Amcos hii,” amesema Mbilinyi.

Akikabidhi Matrekta hayo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Meatu, Anthony Philipo amewataka viongozi wa Amcos hao kwenda kuyatumia matrekta hayo kwa kazi ilikusudiwa ya kuwasaidia wakulima na siyo kuanza kuyagombania.

Amesema Ofisi yake itakuwa inafanya ufuatiliaji wa karibu kuona kama yanatumika ipasavyo kwa kuwasaidia wakulima, huku akizitaka Amcos nyingine 71 kwenye halmashauri hiyo kuiga mfano wa Amcos hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles