Na Samwel Mwanga,Bariadi
WAKULIMA wa zao la pamba katika wilaya Bariadi mkoa wa Simiyu wametakiwa kulima zao hilo kwa kutumia vipimo vipya vya kisasa.
Vipimo hivyo ni sentimeta 60 kutoka mstari hadi mstari na sentimeta 30 kutoka shimo hadi shimo na kuacha mtindo wa zamani wa kurusha mbegu.
Hayo yameelezwa juzi na Balozi wa Bodi ya Pamba Tanzania (TCB), Aggrey Mwanri kwa nyakati tofauti alipokuwa akitoa semina elekezi ya namna ya kuongeza tija kwa kutumia vipimo vipya katika zao hilo kwa wakulima wa mbalimbali vya wilaya hiyo iliyofanyika mjini Bariadi.
Amesema kuwa mabadiliko hayo ya vipimo yatamwongezea mkulima idadi ya miche kutoka 22,222 ya awali alipokuwa anatumia vipimo vya sentimeta 90 kwa sentimeta 40 hadi kufikia miche 44,444 kwa kutumia vipimo vipya.
Amesema kuwa endapo wakulima watatumia vipimo vipya wakati wa kupanda zao la Pamba ifikapo mwaka 2025 wanatarajia kuzalisha kiasi kikubwa cha zao hilo na Tanzania inaweza kuwa ya kwanza barani Afrika kwa uzalishaji wa pamba.
“Kama wakulima wakifuata maelekezo na kanuni bora za kilimo cha zao la Pamba kwa kupanda shamba zima kwa kutumia vipimo na kuachana na mtindo wa kupanda mstari wa mbele kwa kufuata vipimo alafu wanaendelea kumwaga mbegu kama zamani hatutafikia malengo tuliyojiwekea,” amesema Mwanri.
Aidha, Mwanry ambaye amewahi kuwa kushika nyadhfa mbalimbali serikalini amesema Pamba ni zao muhimu la kimkakati na kibiashara huku pia likichangia takribani asilimia 10 hadi 20 ya pato la Taifa.
Amesema zao la pamba pia linaingiza fedha za kigeni sambamba na kutoa ajira kwa asilimia 40 ya Watanzania.
Kutoka na umuhimu huo, alisisitiza kuwa wakulima hawana budi kulima zao hilo kwa kufuata kanuni bora za kilimo ikiwemo kupambana na wadudu waharibifu kwa kutumia viuatilifu.
“Tunapoendelea kutoa elimu, tutaendelea kuwaelimisha wakulima juu ya matumizi sahihi ya viuatilifu pamoja muda mwafaka wa kupulizia dawa na vifaa maalumu vinavyotumika wakati wa kunyunyuzia dawa hiyo,” amesema.
Amesema kuwa Bodi ya Pamba tayari imeishachukua hatua mbalimbali ya namna ya kuwasaidia wakulima kupata viuatilifu vitakayowasaidia kupambana na wadudu waharibifu shambani.
Kwa upande wake, Ofisa Kilimo Mkoa wa Simiyu, Kija Kienze amesema kutokana na programu ya kuhamasisha kilimo cha Pamba mkoa huo umeanza kuwa na matarajio ya kunufaika tofauti na kipindi cha nyuma ambapo zao hilo lilianza kuzorota.
Nae, John Shilinde ambaye ni mkulima aliyepata elimu elekezi namna ya kuongeza tija kwenye zao la pamba amesema kuwa elimu hiyo itawasaidia kwa kiasi kikubwa kufanya mabadiliko katika zao hilo, na kuiomba bodi ya pamba kuendelea kutoa elimu namna ya kuendelea kutumia Vipimo vipya ili waweze kuacha kilimo cha mazoea.